Ni dhahiri sarafu ya Tanzania imeelemewa na thamani ya Dola ya Marekani na sasa bei ya kubadili fedha inazidisha makali na maumivu kwa wananchi kwa kuwa kila uchao Shilingi inazidi kuporomoka kwa kasi kubwa.
Kulingana na taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu soko la kubadili fedha za kigeni katika benki nchini (IFEM) hadi mwishoni mwa wiki iliyopita Dola moja ya Marekani ilikuwa ikiuzwa kwa Sh. 1,824.02. Hiki ni kiwango cha juu kabisa cha kuporomoka kwa sarafu ya Tanzania tangu mwaka 2004 kilipokuwa cha chini zaidi cha Sh. 1,014.30 kwa Dola.
Mara kadhaa tumeandika tahariri katika safu hii mwaka huu tukielezea kuguswa kwetu na kuporomoka kwa thamani ya Shilingi; pia tumetoa rai kwamba ni wakati mwafaka kwa mamlaka za usimamizi wa sekta ya fedha kujitafakari hatua za kuchukua juu ya kuendelea kuzama kwa sarafu hiyo dhidi ya Dola ya Marekani. Kwa bahati mbaya hatujaona hatua za maana zikichukuliwa kuisaidia Shilingi.
Wapo watu ambao wamepuuza rai hii wakijikita kwenye dhana kwamba hizi ni nyakati za mfumo wa uchumi wa soko huria ambao huendeshwa kwa nguvu za soko, ugavi na mahitaji, lakini wamekwepa kutilia maanani ukweli kwamba kwa hali ya uchumi wa nchi hii kuacha Shilingi kusukwa sukwa na nguvu hizo, kuna hatari kubwa ya kiuchumi kwa taifa hili.
Tunajua dhahiri kwamba pamoja na serikali kuwa na mipango yake ya maendeleo inayoanishwa kwenye kila bajeti ya kila mwaka, utekelezaji wake kimsingi unategemea sana mwenendo wa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani, kama Shilingi inaporomoka kila uchao maana yake ni kwamba miradi mingi itakuwa ya ghali sana kutekelezwa na mingine haitatekelezwa kabisa, sisi ni taifa linalotegemea sana Dola ya Marekani kupita kiasi.
Tafsiri pana ya mahusiano ya thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani ni ama kuimarisha au kuyumba kwa uchumi wetu kama Taifa. Mporomoko wa Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani una maana ya kuzidi kupungua kwa uwezo wa sarafu yetu katika kununua bidhaa na ulipiaji wa huduma mbalimbali kutoka nje.
Kwa kifupi, wakati dunia kwa sasa ikishuhudia mporomoko mkubwa wa bei ya mafuta ya petroli, nafuu hiyo haitajiakisi kwenye uchumi wa ndani ya nchi kwa sababu nafuu hiyo itamezwa kutokana na ulegevu wa sarafu yetu. Kwa maana hiyo, njia pekee ya kuhakikisha kwamba Taifa linanufaika na kuporomoka kwa bei ya petroli katika soko la dunia ni kuhakikisha Shilingi inakuwa imara dhidi ya Dola. Itakumbukwa kwamba tangu kufunguliwa kwa milango ya uchumi, chini ya soko huria mwishoni mwa miaka ya 80, kumekuwa na maoni tofauti juu ya njia za kuilinda sarafu ya Tanzania dhidi ya mahitaji makubwa na yasiyokuwa ya msingi ya Dola ya Marekani.
Mathalani, wapo watu wamejenga hoja zenye nguvu kwamba kwa kiwango kikubwa tabia ya baadhi ya watoa huduma na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kupanga bei zao kwa Dola za Marekani, hakika kunaongeza shinikizo kwa sarafu ya nchi hii bila sababu.
Kubwa zaidi kumekuwa na uagizaji wa vitu kutoka nje ambavyo huhitaji Dola ya Marekani wakati kimsingi vitu hivyo havina maana, tija na wala havisaidii juhudi za taifa hili kupambana na umasikini mbali tu ya kuongeza mahitaji makubwa ya Dola na hivyo kuzidi kuikandamiza Shilingi kila uchao.
Kama Taifa tujiulize kweli kuna uhalali wowote wenye tija kuagiza nje ya nchini bidhaa kama samani ambazo ni kama maboksi tu?; mapambo na wanasesere wa plasitiki?; vifaa chakavu vya nyumbani kama vyombo, nguo kuukuu (mitumba), vitu ambavyo hakika havidumu hata mwaka mmoja, kwa kutumia Dola za Marekani ambazo kimsingi zingehitajika kwa ajili ya kuingiza vitu muhimu na ambavyo hakika haviwezi kupatikana hapa nchini?
Wendawazimu huu wa kuagiza vitu kutoka nje umeingia hata kwenye vyakula ambavyo vimejaa kiasi cha kuozea katika masoko yetu. Hivi ni kama mbogamboga, matunda na hata nyama ya ng’ombe na kuku; mayai na unga na bidhaa nyingine za vyakula. Matumizi ya Dola ya Marekani kuagiza vitu kama hivi hakika ni kuzidi kuiongezea mzigo sarafu yetu.
Kwa bahati mbaya, si serikali au mamlaka nyingine za usimamizi zimeona hatari inayotunyemelea kama taifa kwa kudekeza udhaifu huu wa kuhalalisha huria huu usiokuwa na tija wala ukombozi wowote dhidi ya umasikini wa nchi hii. Tunasikitika kwamba kadri siku zinavyosonga mbele sarafu yetu imegeuka nyuma na kuanza mbio kwa kasi kubwa kurejea nyuma.
Kama ambavyo tumekuwa tukipaza sauti, leo tunarejea wito wetu kwamba serikali na vyombo vyake wakitaka kuimarisha Shilingi kwa hatua tu za kiutawala, kikanuni na sheria inawezekana. Ni wajibu wa serikali kutambua hili na kuchukua hatua madhubuti za kusaidia Shilingi vinginevyo mipango yote ya maendeleo inayopangwa haitafikiwa.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment