Wednesday, 29 April 2015

SHILINGI HOI INAUA UCHUMI-MBATIA


Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia (pichani), ameitaka serikali na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuchukua hatua haraka na madhubuti kunusuru kuporomoka kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani ambayo imeporomoka kwa asilimia 21.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mbatia alisema sababu zilizochangia kuporomoka kwa Shilingi ni Bajeti tegemezi kwa wafadhili, mauzo kidogo kutoka ndani kwenda nje ya nchi, manunuzi makubwa kutoka nje kuja ndani na siasa zisizokuwa na hofu ya Mungu.
“Ndani ya mwezi mmoja Shilingi yetu imeporomoka kwa zaidi ya asilimia 20 hadi 21 kutoka Sh. 1,650 kwa Dola moja ya Kimarekani hadi Sh. 2,010 kwa takwimu za juzi, poromoko hili ni tishio kwa uchumi. Sayansi anuai inatuonyesha kwamba nguvu ya mporomoko wa kiasi hiki inaweza kutikisa vibaya mfumo wa uchumi kama hatua za kifedha hazitachukuliwa haraka iwezekanavyo,” alisema.
Mbatia alisema bajeti ya Taifa kwa kiasi kikubwa, zaidi ya asilimia 30 inategemea fedha za wafadhili wa miradi mbalimbali ambao wanapoamua kushikilia fedha zao, poromoko la Shilingi hutokea na inapokuwa kinyume wanashikilia fedha yao.
Alisema ni lazima BoT itoe matumaini kwa Watanzania kuhusu hali ya uchumi kabla hali haijawa mbaya zaidi.
“Uchumi ni kushirikiana katika kutumia rasilimali za dunia ili kuishi katika hali ya utu tuliokirimiwa na Mungu. Tunao wajibu wa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa dunia kwa sababu rasilimali tulizonazo juu ya ardhi na ndani ya ardhi, ushirikiano wa kibiashara ni sehemu ya maisha,” alieleza Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi.
Alisema ni lazima Tanzania ijitambulishe kwa Shilingi yake kwa kuhakikisha inalindwa isiporomoke dhidi ya Dola ya Marekani.
Mbatia alisema uwezo wa kuongeza mapato ya Tanzania kutoka mauzo ya nje ni mkubwa kwa kupitia sekta za uvuvi, utalii na usafirishaji wa anga na kwamba zinaweza kutumika ili kuongeza fedha kutoka nje na kukabili poromoko hilo.
“Kanuni kuu ya maisha ni mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe, naomba tujiulize kwanini tunatumia Dola katika shughuli zetu za kibiashara ndani ya nchi? Hii inaitwa ‘dollarization’, athari zake ni kubwa kwa uchumi na wananchi. Ni lazima tuwe na sheria ya kuzuia ‘dollarization’, na huu ndiyo muda mwafaka kwa usalama wa nchi yetu,” alisema.
Alisema kwa hali ilivyo nchini kwa sasa, Mtanzania anayepokea Sh. milioni moja, thamani yake ni Sh. 800,000, huku posho za viongozi wanaposafiri nje ya nchi kwa kutumia ndege kwa daraja la kwanza na pili kwa siku ni Dola 504 ambayo awali ingekuwa Sh. 600,000, lakini kwa sasa ni milioni moja kwa siku.
Alisema atapeleka hoja bungeni ya kuitaka serikali kuchukua hatua ikiwamo kuacha kuagiza samani na bidhaa nyingine ambazo zinaweza kupatikana nchini kutoka nje ya nchi.
Mbatia alisema hali inazidi kuwa mbaya nchini pale serikali inapokwenda kukopa kwenye taasisi binafsi za fedha na watu binafsi pia kufanya hivyo na kuzifanya taasisi hizo kuitunishia misuli serikali.
“Tuendako na hali ikiachwa kuwa hivi, nchi inaweza isitawalike, wafanyabiashara wakubwa wanaacha kuwekeza nchini na kuzalisha bidhaa za kuuza nje, bali wananunua nje na kuuza ndani kwa wingi,” alisema.
WAZIRI WA FEDHA 
NIPASHE ilipomtafuta Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, kujibu kauli  za Mbatia, alisema kiasi cha Dola kilichopo kwenye mzunguko siyo cha kudhuru uchumi na kwamba athari zinazojitokeza kwa Shilingi haiko Tanzania pekee bali imezikumba nchi nyingi ikiwamo Uganda na nyingine zinazotumia Euro na paundi.
Alisema kuporomoka kwa Shilingi kunasababishwa na kuimarika kwa uchumi wa Marekani na kudorora kwa biashara ya utalii ambayo ndiyo inayoingiza fedha nyingi za kigeni.
Mkuya alitaja sababu nyingine kuwa ni tishio la ugaidi na kuagiza bidhaa zaidi kutoka nje kuliko kuuza nje na wafanyabiashara wakubwa kuamini kuwa na Dola nyingi ndiyo faida kubwa.
“Kuonekana Dola ni nyingi sokoni na kupanda bei kunasababishwa pia na watu wengi wakiwamo wafanyabiashara wakubwa wanakwenda kwenye benki moja wakihitaji Dola nyingi, akikosa ataenda benki mbili hadi tatu, hivyo kuonyesha kuwa mahitaji ya Dola ni makubwa,” alisema na kuongeza:
“Tunachofanya kwa sasa kila siku kama kuna mwenye haja ya Dola anaipata kama ilivyo ili asionyeshe kuwa kuna mahitaji makubwa ya Dola.” 
Gavana wa BoT, Prof. Benno Ndulu, alipotafutwa, simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa. 

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!