Tuesday, 21 April 2015

NI MUHIMU KUTUMIA MADINI JOTO KUZUIA UDUMAVU WA AKILI

WATANZANIA wanatakiwa kuweka mikakati ya kuwapatia watoto chakula chenye majini joto ili kuwezesha Taifa kuwa na watu wenye uwezo mkubwa kiakili.


Rai hiyo ilitolewa na Ofisa Lishe wa Mkoa wa Iringa, Mwita Waibe wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa ajili ya waganga wakuu wa wilaya, maofisa lishe, maofisa mipango na wakurugenzi wa wilaya za mkoa wa Dodoma.
Waibe anasema Taasisi hiyo ya Chakula na Lishe imelazimika kutoa mafunzo hayo ili kuhamasisha wadau wa afya kutoa elimu kuhusu umuhimu madini joto kwa kuwa athari za ukosefu wa madini hayo zinaongezeka hasa kwa watoto.
“Ukosefu wa chumvi yenye madini joto katika vyakula ni miongoni mwa mambo yanayoathiri ukuaji wa akili kwa watoto nchini,” anasema Waibe. Waibe anasema athari za udumavu ni kubwa katika nyanja zote ikiwemo kiuchumi na kijamii. Anasema kuwa takwimu zilizopo zinaonesha asilimia 42 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchini wana udumavu na upungufu wa madini joto.
Udumavu umekuwa ni tatizo kubwa katika jamii, jambo ambalo pia huchangiwa na unyonyeshaji usio sahihi na kuwalisha watoto wadogo vyakula vyenye mchanganyiko wa nafaka nyingi, hali inayoathiri makuzi ya mtoto kiakili. Pia watoto wengi wanaozaliwa wamekuwa hawanyonyeshwi kwa usahihi na wengine huanza kupewa vyakula kama uji kabla ya kufikisha umri wa miezi sita.
Waibe anasema udumavu wa akili unasababishwa na kinamama wanapokuwa wajawazito kutotumia chumvi za madini joto na kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha watu wanafahamu umuhimu wa matumizi hayo ya chumvi. Chumvi yenye madini joto hujenga ubongo wa binadamu kwa siku 1,000 mtoto anapokuwa tumboni kama mtoto atajengeka ubongo vizuri atakuwa na akili nzuri shuleni na kuwa na uelewa mkubwa.
Pia anasema hali ya udumavu imekuwa ikitofautiana kutoka mkoa mmoja hadi mwingine na kusema kuwa watoto wanaotoka mikoa vyakula vyenye madini joto hufanya vizuri darasani na kushika nafasi za juu katika kazi. Watoto kutoka mikoa yenye vyakula vyenye upungufu wa na madini joto hudumaa kiakili hivyo huwa wa mwisho katika mitihani ya taifa na kushindwa kupata kazi za kuajiriwa maofisini.
“Mfano, watu wa mikoa ya kanda ya kaskazini wanapata vyakula vyenye madini joto na ndio wale wanaofanya vizuri katika hesabu, fikizia na wamekuwa wakifurahia shule na asilimia kubwa ya watu hao ni wataalamu walio nchi za nje,” anasema Waibe. Jamii inapaswa kuelimisha juu ya tatizo la upungufu wa madini joto ili waweze kuona umuhimu wa kuchukua hatua sitahiki.
Hatua mojawapo ni kuhakikisha wajawazito kutumia madini joto ili taifa lipate viongozi wazuri wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuleta mbinu za kutatua matatizo yanayolifanya Taifa kuendelea kuingia kwenye lindi la umasikini. Anasema madini joto yanapatikana kwenye chumvi lakini chumvi nyingi hazina madini hayo hivyo ni lazima kuwa makini wakati wa kununua chumvi.
“Chumvi ni kitu muhimu lakini kinapuuziwa na jamii kwa watoto ndio wanaotumwa kununua chumvi bila kujali kuwa hawawezi kujua chumvi yenye madini joto,” anasema Waibe. Waibe anawahimiza wadau wa afya kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutumia chumvi yenye madini joto na umuhimu wa kunyonyesha watoto kwa usahihi.
Anabainisha kuwa mtoto anatakiwa kunyonya maziwa ya mama miezi sita ya mwanzo bila kupewa chakula kingine chochote na baada ya miezi sita anaweza kupewa chakula na kuendelea kunyonya hadi atakapofikisha umri wa miaka miwili. Ni muhimu kuzingatia makuzi ya mtoto kiakili tangu akiwa mdogo kwa kuwa tatizo la udumavu wa akili linaleta athari kubwa kiuchumi na kupunguza ufanisi kwenye kazi.
Akitoa mfano, anasema watu wanaokabiliana na tatizo la udumavu wa akili wamekuwa chanzo cha kushuka kwa ufanisi katika kazi kutokana na kutokuwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka. Anasema asilimia kubwa ya walioathirika na udumavu wako maofisini na wanaleta madhara kwenye utendaji kazi kwa kuwa hukwamisha hata wale wanaowaongoza.
“Huwezi kufikia maamuzi sahihi kama umepata udumavu wakati wa kukua,” anasema Waibe. Waibe anasema tatizo la udumavu nchini ni kubwa na lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo viongozi hao ili waweze kulisimamia suala hilo katika maeneo yao. Udumavu umekuwa ukisababisha kupungua kwa ufanisi kazini na hata wanafunzi mashuleni kutokana na athari hizo kuwapata tangu wakiwa wadogo.
Waibe anasema watu wamekuwa na dhana potofu kuwa mtu akiwa na mwili mkubwa na mrefu hawezi kuwa mdumavu wa akili na wadumavu ni watu wafupi tu. “Udumavu wa akili huwapata pia watu warefu na wenye miili mikubwa ikiwa mtu huyo amekosa vyakula vyenye madini joto toka utotoni,” anasema Waibe.
Wengi walio na tatizo hilo wako maofisini na wanaleta shida kwenye ufanisi katika kutenda kazi zao na hata kuchukua maamuzi. “Udumavu haupimwi kwa urefu au unene na umekuwa na madhara makubwa kiuchumi kutokana na watu wenye tatizo hilo wamekuwa wakitekeleza majukumu yao chini ya kiwango,” Waibe anasisitiza.
Kulingana na mtaalamu huyo, asilimia 56 ya watu walioathirika na udumavu wako ofisini. Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge anasema yamekuwa yakitolewa maelekezo mengi juu ya masuala ya lishe lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua.
“Miaka mitatu au minne iliyopita waliajiriwa maofisa lishe ngazi za mkoa na mamlaka za serikali za mitaa lakini lipo suala la kuweka bajeti kuhusu utekelezaji wa masuala ya afya na lishe,” anasema Madenge. Anasema licha ya maofisa hao kuajiriwa bado elimu kuhusu lishe bora ni ndogo, utapiamlo bado upo, watoto wanazaliwa wadumavu.
Madenge anasema asilimia 56 ya watoto mkoani Dodoma wanakabiliwa na udumavu, jambo ambalo ni aibu kwa mkoa wa Dodoma. “Tuone tatizo hili la udumavu wa akili na kutekeleza programu ya lishe bora ili tutoke hapa tulipo na hilo litawezekana kama tukiwa na nia,” anasema Madenge. Anasema maofisa lishe wana mengi ya kufanya katika eneo lao na utekelezaji.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mwajina Lipinga anasema kaya zikiwa na uhakika wa chakula na kupewa elimu itasaidia katika suala zima la lishe. Anasema hata katika suala la mifugo linatakiwa kupewa umuhimu ili familia zipate lishe za nyama na maziwa kwa ajili ya kuboresha afya.
Ofisa kilimo mkoa wa Dodoma, Benard Abraham anasema ufanisi na tija katika mkoa huu ni mdogo kutokana na mkoa kuwa na mvua kidogo. Anasema wakulima katika mkoa wa Dodoma hupata wastani wa tani moja hadi mbili kwa ekari huku wale wa mikoa ya Mbeya na Rukwa huweza kupata hadi tani tano kwa ekari.
Anasema hali ya uzalishaji wa chakula imekuwa ikichangia hata jamii kuwa na lishe duni. Pamoja na hayo anasema elimu zaidi inahitajika ili kuweza kukabiliana na tatizo la udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano kutokana na kukosa madini joto na hata lishe bora.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!