Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amewataka wafanyabiasha wa Tanzania kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji katika visiwa vya Comoro.
Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma kilichopo chini ya Wizara hiyo, imeeleza kuwa, waziri huyo alitoa rai hiyo juzi wakati akihutubia kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Comoro.
Kongamano hilo liliandaliwa kwa ushirikiano baina ya Balozi za Tanzania na Comoro na sekta binafsi za nchi hizo mbili jijini Moroni, Comoro.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Membe alisema kutokana na kuimarika kwa ushirikiano kati ya nchi hizo, ni fursa ya pekee sasa Watanzania kuchangamkia nafasi za biashara na uwekezaji visiwani humo.
“Watanzania tunathaminiwa sana hapa kutokana na mchango wetu mwaka 2008 tulipokikomboa kisiwa cha Anjouan kutoka kwa Kanali Bacar, Serikali ya Umoja wa Visiwa vya Comoro imeimarika na uhusiano wetu umeshamiri,” alisema na kuongeza:
“Wanatukaribisha sisi kwanza kushirikiana kibiashara, tuchangamkie fursa hii,” alisema Membe ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kongamano hilo.
Pia alisifu jitihada za ofisi za ubalozi wa nchi hizo kwa kuitikia wito wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara kwa kuandaa kongamano hilo la kihistoria.
“Rais Kikwete alipofanya ziara yake hapa mwaka 2014, aliahidi kukuza uhusiano wetu na kutoa wito wa kushirikiana kibiashara kwa manufaa ya nchi zetu, nawapongeza sana Balozi Kilumanga na Balozi Fakih kwa kushirikiana na sekta binafsi na kutekeleza hili kwa wakati,”alisema.
Rais wa Visiwa vya Comoro, Ikililou Dhoinine, alisema yeye na serikali yake wanathamini mchango mkubwa wa Tanzania kwa watu wa Comoro.
Alisema atahakikisha uhusiano huo unakua kwenye nyanja zote zikiwamo sekta binafsi, serikalini na kwa watu wa nchi zote mbili.
Baada ya ufunguzi wa kongamano hilo, wafanyabiashara wa Tanzania walipata fursa ya kukutanishwa na wenzao wa Comoro kwenye makundi madogo madogo ili kuibua changamoto zinazokwaza biashara baina ya nchi hizo.
Katika ziara hiyo, Membe alipata fursa ya kutembelea fukwe za bahari ambazo ni vivutio vikubwa vya utalii kwenye nchi hiyo ya visiwa akiwa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Visiwa vya Comoro, Dk. Alanrif Said Hussane.
No comments:
Post a Comment