Tuesday 7 April 2015

MEMBE AWATAKA WATANZANIA KUJENGA UTAMADUNI WA KUSAIDIA WASIOJIWEZA




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kuwasaidia watu wasiojiweza waliopo kwenye jamii wakiwemo watoto yatima, walemavu, wazee na wajane.



Waziri Membe ametoa wito huo hivi karibuni alipotembelea Kituo cha Kulelea Watoto Yatima na Wazee cha Nyumba ya Furaha na Amani kilichopo Mburahati Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Membe alisema kuwa katika jamii za watu kumekuwa na makundi ambayo yanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa watu wengine ambao kwa namna moja au nyingine wamejaaliwa kipato kidogo na afya. Alisema kuwa ni wajibu wa watu wa aina hiyo kuwasaidia wale wanaohitaji kama vile watoto yatima, walemavu, wazee na wajane.
Waziri Membe ambaye alikuwa amefuatana na Mke wake, Mama Dorcas Membe aliguswa sana na historia ya baadhi ya watoto yatima aliowatembelea kituoni wakiwemo wale waliotupwa jalalani na kuokotwa wakiwa kwenye hali mbaya.


“Lipo kundi linalopata mateso na matatizo katika jamii zetu tunazoishi. Ni vizuri Watanzania tukajenga utamaduni wa kutembelea sehemu kama hizi ili kujionea wenyewe hali halisi. Kwa kweli ni hali ya kusikitisha kuona baadhi ya watoto walitupwa na kuokotwa jalalani na wengine tayari wakiwa wamepata majeraha ya kung’atwa na mbwa. Hivyo ni wajibu wetu sote kuwasaidia kwa chochote kidogo tunachojaaliwa kupata”, alisema Waziri Membe.


Aidha, Mhe. Membe aliwapongeza na kuwasifu Masista wa Shirika la Mama Theresa ambao ndio wasimamizi wa kituo hicho kwa kuwalea watoto, vijana na wazee wenye matatizo mbalimbali na kuwaomba waendelee kujipa moyo katika kazi hiyo kwani ni njia moja wapo ya kumtumikia Mungu.


Awali akimkaribisha Waziri Membe kituoni hapo, Sista Mkuu wa Kituo hicho, Sista Mary Bakhita, alisema kuwa wamefurahia sana ziara hiyo ya Mhe. Membe hususan katika Siku Kuu ya Pasaka kwani ni faraja kubwa kwao kwa Watoto na Wazee wanaolelewa kituoni hapo.


“Tumefarijika sana kula pasaka pamoja nawe Mhe. Waziri. Watoto na Wazee hawa wanajisikia vizuri pale wanapotembelewa na tunaomba uendelee na moyo huo huo”, alisema Sista Bakhita.
Wakati wa ziara hiyo Mhe. Membe na familia yake walitoa zawadi mbalimbali kwa kituo hicho ikiwemo vyakula, sabuni na fedha kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali kituoni hapo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!