KATIKA kuhakikisha vurugu dhidi ya raia wa kigeni zinakomeshwa nchini hapa, Serikali imetangaza kuwa, jeshi sasa litatumika kudhibiti ghasia zilizosababisha vifo vya watu saba, huku zaidi ya 5,000 wakitajwa kuyaacha makazi yao na kwenda kuishi katika kambi maalumu ili kuokoa maisha yao.
Hayo yamethibitishwa na Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini, Nasiviwe Mapisa-Ngqakula na kuongeza kuwa, ombi la kutumwa kwa wanajeshi kuingia mtaani limetokana na ombi la polisi waliotaka kuongezewa nguvu, hasa katika mikoa ya KwaZulu Natal na Gauteng.
Hata hivyo, hakutaja idadi ya wanajeshi watakaoingia mtaani kudhibiti vurugu za raia wa Afrika Kusini waliokata tamaa ya maisha na kuamini ugumu wao wa maisha unatokana na riziki zao kuchukuliwa na wageni.
Juzi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, aliwaambia Watanzania kuwa, pamoja na vurugu zinazoendelea Afrika Kusini, hakuna Mtanzania aliyepoteza maisha na kwamba licha ya kwamba baadhi yao wamejisalimisha katika kambi maalumu na wengine 21 wakiomba kurudishwa nyumbani.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania walioko katika mataifa mbalimbali wajenge tabia ya kujiandikisha katika balozi zao pamoja na kuunda umoja ili kuweza kupata taarifa panapotokea matatizo.
Hata hivyo, alisema serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya mazungumzo ya karibu na viongozi wa Afrika Kusini juu ya vurugu hizo na taarifa zimekuwa nzuri.
Membe amesema kunahitajika kujenga uchumi imara katika nchi za Afrika ili kuwezesha vijana wengi kuajiriwa na kujiajiri na kuachana na kukimbilia katika nchi hizi zenye uchumi wakati hawana ujuzi.
Membe amesema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC), Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Robert Gabriel Mugabe amelaani kitendo hicho.
Wakati wa ghasia kama hizo mwaka 2008 jumla ya watu 63 waliuawa. Serikali ya Afrika Kusini pia imetangaza kuwa zaidi ya watu 900 wameshaondoka Afrika Kusini na kurejea katika nchi zao ili kujinusuru na vurugu zinazoendelea hapa.
1 comment:
aziz bilal11:24
Apartheid regime siku ikiamua kurudi sijui hawa watu watakimbilia kwa nani tena
Post a Comment