Friday, 24 April 2015

DEWJI KUGAWA UTAJIRI WAKE

Mbunge wa Singida Mjini, Mohammed Dewji akizungumza na wananchi wa jimbo lake.
MFANYABIASHARA na mwanasiasa maarufu nchini, Mohammed Dewji (39) anatarajia kuanzisha taasisi yake ya Mohammed Foundation mwezi ujao, itakayotoa misaada mbalimbali kwa jamii na ametenga mabilioni ya fedha.


Dewji, Mbunge wa Singida Mjini anasema kuwa anatarajia kutumia sehemu ya utajiri wake wa Sh trilioni 2.1, kusaidia sekta mbalimbali za jamii.
Dewji ambaye kwa sasa anatajwa ndiye bilionea kijana zaidi Afrika kwa wenye umri wa chini ya miaka 40, kupitia mfuko wake huo amepanga kutumia Sh bilioni 170 kusaidia miradi ya elimu, afya, maji na mingine, kwa lengo la kuinua hali ya maisha ya watu wasio na kipato kikubwa.
“Nimepata fedha hizi nikiwa Afrika, nami sina budi kurudisha shukrani hapa hapa Afrika. “Ninajiona ni mwenye wajibu wa kushukuru na kurudisha kwa Watanzania wenzangu sehemu ya kile ambacho Mwenyezi Mungu amenijalia,” alisema Mohammed, maarufu kama Mo, alipokuwa anazungumzia dhamira yake ya kuanzisha taasisi hiyo.
Alisema taasisi yake itafanya kazi karibu kila kona ya Tanzania, na baadaye katika baadhi ya nchi za Afrika. Aliongeza kuwa, tangu akiwa mdogo alichukia umasikini, ndiyo maana siku zote licha ya kutaka kufanikiwa zaidi, amekuwa akijikita katika kusaidia wengine, akitolea mfano jimboni kwake Singida ambako amefanya mapinduzi makubwa katika sekta za elimu, kilimo, afya na maji tangu awe mbunge mwaka 2005.
“Kutoa fedha tu si njia pekee ya kusaidia, ndiyo maana nataka kutumia sehemu ya utajiri wangu na pia muda, kuhakikisha taasisi yangu inasimama imara na kufanikisha ndoto za kusaidia wengine,” alisema Dewji anayeongoza kampuni kubwa ya Mohammed Enterprises Ltd (MeTL) yenye utitiri wa biashara.
Kwa mujibu wa ripoti ya Jarida la Ventures Afrika Toleo la mapema mwaka huu, Dewji ndiye bilionea kijana zaidi Afrika na wakichanganywa mabilionea wote, wazee kwa vijana, anashika nafasi ya 24 kati ya mabilionea 55 Afrika, wakiongozwa na Aliko Dangote wa Nigeria.

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!