RAIS mstaafu wa Marekani, Bill Clinton na binti yake Chelsea, wanatarajiwa kutembelea miradi mbalimbali ya Taasisi ya Clinton iliyopo katika nchi kadhaa za Afrika, ikiwemo Tanzania.
Pamoja na Tanzania nchi nyingine watakazotembelea ni Kenya na Liberia na kumalizia ziara hiyo nchini Morocco. Aidha katika ziara hiyo, pamoja na kutembelea miradi hiyo, pia Clinton ataimalizia katika mkutano wa Clinton Global Initiative wa nchi za Afrika ya Mashariki ya Kati (CGI MEA), utakaofanyika Morocco.
Katika ziara hiyo, inatarajiwa kuwa masuala mengi yanayoshughulikiwa na taasisi hiyo ya Clinton yataibuliwa, ikiwemo uwezeshaji katika kukuza uchumi, mabadiliko ya tabia nchi, kuwezesha wanawake na wasichana na afya.
Rais Clinton na bintiye Chelsea watatembelea miradi iliyopo kwenye Clinton Climate Initiative, miradi ya maendeleo ya Clinton, mradi wa Full Participation na mradi wa afya wa Clinton.
Akiwa Tanzania, kiongozi huyo atatembelea zahanati ya Ngorongoro ya Nainokanoka kupitia mradi wa Afya wa Clinton (CHAI) ili kuona namna unavyoshughulikia suala la majadiliano ya gharama na manunuzi katika eneo la chanjo na namna unavyotumia teknolojia ya kisasa kutoa chanjo kwa watoto.
Aidha, atakutana na akinamama wanaopeleka watoto wao kupatiwa chanjo kupitia mradi huo, ambao umekuwa ukitoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Nimonia na magonjwa hatari, kama vile kuhara.
Pia akiwa Tanzania, Clinton na bintiye watatembelea mkoani Manyara na Karatu na kushuhudia namna akinamama waliowezeshwa wa Women’s Enterprise na Tanzania Solar Sisters wanavyoendeleza miradi ya umeme wa nishati ya jua.
Tangu kuwezeshwa na taasisi ya Clinton, akinamama hao wamekuwa wakiuza na kujiingiza kipato bidhaa kama vile taa na majiko yanayotumia umeme wa nishati ya jua.
Aidha, Clinton na bintiye pia watatembelea Kenya ambako watakagua namna Mradi wa CHAI unavyotoa elimu kwa familia ya namna ya kudhibiti ugonjwa wa kuhara
No comments:
Post a Comment