Idara ya Uhamiaji mkoani Pwani imenasa majina 15 ya watu wanaodaiwa kuwa wahamiaji haramu waliojiandikisha kwenye Zoezi la Vitambulisho vya Taifa.
Afisa uhamiaji mkoani Pwani, Grace Hokororo, ameiambia NIPASHE kuwa tayari wamepata majina hayo ambapo hatua inayofuata ni kuwakamata na kuwahoji ili kupata uhalali wa uraia wao.
“Tutachukua maelezo yao tukiridhika kuwa si raia wa Tanzania tutawachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani,” alisema.
Utafiti uliofanywa na kituo cha msaada wa kisheria na haki za binadamu cha TLF kilichoko mjini Mlandizi na uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa raia wa Kenya, Uganda na Burundi, waliingia kwenye mji huo na kujihusisha na uuzaji wa biashara ndogo ndogo ikiwemo kuuza kahawa na nguo.
Aidha raia hao zaidi 18, walidaiwa kujiandikisha katika zoezi la vitambulisho vya taifa linaloendelea mkoani Pwani bila kutambulika na mamlaka husika.
Katika hatua nyingine zoezi la kujiandikisha na kupiga picha viatambulisho vya uraia lilisitishwa kabla ya muda wake na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wa mjini Mlandizi ambapo NIPASHE ilishuhudia wananchi wakiwa katika vituo na maafisa wa NIDA hawakuwepo.
“Tulitangaziwa kuwa hili zoezi litaanza tarehe 15 kumalizika tarehe 22 machi matokeo yake likaisha tarehe 21 hali hiyo ilitufanya wengi tumeshindwa kujiandikisha kwa ajili ya kupata vitambulisho”, alisema Mama Mbisa mkazi wa Mlandizi.
Alipoulizwa kuhusiana kusitishwa kwa zoezi hilo Msemaji wa kitengo cha mawasiliano cha Mamlaka ya Viatambulishi vya Taifa (NIDA) Thomas Wiliam alisema hakuna zoezi lililositishwa kwani NIDA wanafanya kazi ya kusajili kila siku.
“, Hakuna zoezi lililositishwa, zoezi ni endelevu kwani kila siku watu wanazaliwa, wengine wako safarini na wote wanatakiwa kujiandikisha, hivyo natoa wito kuwa ofisi za wilaya za NIDA ziko wazi muda wote, ambaye hakupata fursa basi aende atahudumiwa,” alisema Wiliam
No comments:
Post a Comment