Monday, 16 March 2015

WAETHIOPIA 63 MBARONI.


JESHI la Polisi mkoani hapa linawashikilia raia 63 wa Ethiopia na maiti mmoja ambao walikuwa wakisafirishwa na dereva Mtanzania kutoka Moshi kwenda Mbeya kwa kupitia njia za panya.



Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma , David Misime amesema kwamba raia hao wa Ethioppia jumla yao ilikuwa ni 64 na kwamba mmoja alikuwa amekufa, wakati wanawatia mbaroni kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Kidoka.
Kwa mujibu wa Misime watu hao waliokamatwa katika tarafa ya Goma wilaya ya Chemba walikuwa wanasafirishwa na gari aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba ya usajili T 353 AYW lililokuwa likiendeshwa na Othman Mtekateka.
Aidha alisema aliyekutwa amekufa alitambuliwa kwa jina moja la Tajiru anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 – 30.
Imeelezwa kuwa juzi Jumamosi majira ya asubuhi katika kijiji cha Kidoka baada ya wananchi kuona watu wengi wasiofahamika wakiwa wamejificha katika vichaka na mashamba ya watu, huku wakionekana dhaifu, wengine wakila mahindi mabichi na huku wakiomba kwa wanakijiji waliokuwa wakipita maeneo jirani msaada wa chakula na maji ya kunywa kwa ishara, wananchi waliamua kulitaarifu Jeshi la Polisi.
Kamanda Misime alisema walipopewa taarifa walifika na kuanza msako wa kuwakamata na walipohojiwa walibainika kwamba ni raia wa Ethiopia na hawakuwa na vibali vya kuingia/kusafiria.
Aidha, katika msako huo alikamatwa dereva wa gari hilo aitwaye Othman Mtekateka (45) mkazi wa Ilala Jangwani jijini Dar es Salaam ambaye alikiri kuwa yeye ndiye aliyekuwa anawasafirisha watu hao akiwa na wenzake wanne ambao walitoweka baada ya gari kuharibika.
Alidai kuwa aliwapakia watu hao Machi 12, mwaka huu huko Moshi – Kilimanjaro akitakiwa kuwapeleka mkoani Mbeya kwa kupita njia za panya.
Alisema baada ya gari kuharibika Jumamosi usiku katika kijiji cha Kidoka waliwashusha na kuwapeleka porini kuwaficha kisha kuendelea kutengeneza gari na iliposhindikana waliwatelekeza porini na gari kulitelekeza kijijini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!