Monday, 16 March 2015
WAACHENI WAKRISTO WAJIAMULIE-PENGO
“MAASKOFU hatuna mamlaka ya kuwaamulia au kuwalazimisha waumini wetu wafanye uamuzi gani kuhusu Katiba. Kuwaamulia ni kuwadharau kuwa hawawezi kufanya uamuzi sahihi wao wenyewe na kuingilia uhuru wao.
“Waraka huu unaleta utengano katika taifa kuwa Wakristo tumechukua uamuzi dhidi ya Serikali na wengine....Tuwaache waumini wafanye uamuzi kwa tafakari yao binafsi bila shinikizo letu…”
Hayo ni maneno ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyoyatoa mwishoni mwa wiki.
Alisema hayo wakati akifungua Mafungo ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), yaliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam sambamba na kufanya Matendo ya Huruma kwa kutoa msaada kwa wahitaji wa Kituo cha Nyumba ya Amani na Furaha, Mburahati, jijini Dar es Salaam.
Alisema hayo alipokuwa anazungumzia wimbi la matamko ya kushawishi Wakristo kuipigia kura za ‘Hapana’ Katiba Inayopendekezwa, ambayo itapigiwa kura na Watanzania wote Alhamisi Aprili 30 mwaka huu.
Miongoni mwa taasisi zilizoibuka na kutoa matamko ni Baraza la Maaskofu nchini (TEC) na Jukwaa la Wakristo.
Kardinali Pengo alisema: “Wakati hili linajadiliwa nilikuwa Italia katika kusimikwa Makardinali na baadaye India, wengine wakavumisha nimelazwa…wengine nimefariki, lakini namshukuru Mungu hizo ni dua za kuniongezea maisha marefu na afya. “Nililetewa waraka nikausoma, umepitishwa baada ya tafakari kubwa. Nauheshimu, lakini nadhani tuwaache waumini wafanye uamuzi kwa UHURU baada ya kutafakari… Si sahihi tukaenda katika Katiba kama Wakristo kwa shinikizo la kupinga Katiba... “Wawe huru, anayepinga kwa hiyari yake, anayekubali pia kwa dhamira yake. Sidhani kama viongozi wa dini sasa tuna amri ya kulazimisha uamuzi juu ya Katiba...”
Katika kuonesha msisitizo juu ya kauli yake, alisema waumini wa Kikristo nchini sio watoto wadogo, kiasi cha kutojua kinachoendelea katika mchakato wa Katiba mpya, hivyo waachwe waamue wenyewe kwa kuwa wana akili timamu, badala ya baadhi ya maaskofu kutoa waraka unaowataka kuikataa Katiba Inayopendekezwa.
Alitumia fursa hiyo kusema viongozi wa kiroho wana kila sababu ya kutoa tamko kwa kuwa wao ni sehemu ya jamii na kufanya imani yao ya Kikristo, inaweza kuzaa matunda.
Kardinali Pengo alisema maaskofu waliotoa tamko hilo ni wajibu wao kutoa matamko, kwa kuwa wamekabidhiwa madaraka ndani ya kanisa na taifa na mambo wanayosema yanatakiwa yasipuuzwe, kwa kuwa wametenda baada ya kujadili kwa kina.
“Ni wakubwa na wamekabidhiwa madaraka ndani ya kanisa na taifa. Mambo wanayosema hatuwezi kuyapuuza kwa sababu wametamka baada ya kujadili kwa kina,” alisema Kardinali na kuongeza; “Tuna wajibu wa kufanya imani yetu ya Kikristo iweze kuleta matunda mema.”
Lakini, Kardinali Pengo alisema pamoja na maaskofu, kuwa na madaraka ndani ya kanisa, hawana mamlaka ya kuwalazimisha waamini kutenda jambo, kinyume na lililoko ndani ya dhamira zao.
"Ni muhimu waachiwe watende jinsi Mungu anavyowaongoza kwenye dhamira".
Msimamo wa Kardinali ni kuwaachia waamini wakapige kura baada ya kuisoma kwa kina Katiba Inayopendekezwa na kutafakari kwa kina na kupata maongozi ya Mwenyezi Mungu, na si kuwaamulia wafanye nini, wasifanywe kama watoto wadogo.
“Maaskofu hawana mamlaka ya kuwalazimisha kutenda kitu, kinyume na kilicho ndani ya dhamira zao. Haina sababu sisi maaskofu kuwaambia wapiga kura ifikapo tarehe ya kupiga kura wakapige kura ya hapana.
“Kwa nini tuwafanye kama watoto wadogo? Je waamini wetu ni watoto wadogo wasiojua kinachoendelea katika nchi yetu,” alisema Kardinali Pengo na kuongeza tumepata wapi haki hiyo? Ni muhimu watende mbele ya Mwenyezi Mungu jinsi dhamira itakavyowatuma.
Aliongeza kuwa, pamoja na umahiri wa matamko yote mawili, lakini yanawagawa Wakristo kwa kuwa wapo Wakristo tena Wakatoliki kwenye uongozi sasa wataasi imani yao wasimamie serikali au waasi serikali wasimamie imani yao, hivyo kwa kufanya hivyo watakuwa hawawatendei haki waamini wao.
Alisema yeye wajibu wake ni kuelezea na pale watu wanaposoma au kusikia wamwombe Mungu awaongoze kutumia na kutenda kadiri ya dhamira. Aidha, alisema msimamo wa Kanisa Katoliki ni kwamba hakuna mwenye uwezo wa kumwambia mtu apige kura ya hapana.
“Kama Mungu hafanyi hivyo hivyo binadamu amepata wapi mamlaka hayo?” alihoji Kardinali Pengo.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwasihi akinamama kutochoka kusali kuombea umoja wa taifa la Tanzania.
Akimshukuru Kardinali Pengo, Makamu Mwenyekiti wa WAWATA Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Rose Mpembe alisema Kardinali ameondoa hali ya kuchanganyikiwa au sintofahamu, iliyokuwa imetanda miongoni mwa waamini na kushukuru kuwa amewapa uhuru wa kufanya kile ambacho Mungu atawaongoza.
Katika matoleo hayo, WAWATA walitoa vitu mbalimbali vikiwemo shuka, sukari, unga wa sembe, sabuni, mchele, mataulo na fedha taslimu Sh milioni nne kwa ajili ya kununua maziwa ya watoto aina ya Lactogen, vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 13.8.
Katika mafungo hayo, Padri Henry Remisho wa kanisa hilo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi na mwanafunzi wa shahada ya falsafa (PhD) chuoni hapo, alielezea changamoto zinazokabili familia kwa sasa hasa kipindi hiki cha utandawazi na kuongezeka kwa mitandao ya kijamii.
Aliwaasa akinamama kuwapa watoto wao malezi yaliyo bora na kuepukana na suala la kwenda na wakati. Alisema kwa kutaka kwenda na wakati watawapoteza watoto wao na mwisho wataanza kutupia lawama kwa Mungu , jamii na serikali pasipo kujua kuwa chanzo ni wao wenyewe.
Alisema kupotea kwa tunu bora na maadili katika jamii ni kwa wazazi kutowajibika ipasavyo katika familia na hiyo inaleta dhoruba na maangamizi.
Hata hivyo, Padri Remisho alitoa somo kwa WAWATA jinsi wazazi wanavyoweza kufikia matarajio ya malezi kwa watoto wao, aidha kwa ubora au kwa kuwaharibu.
Alisema kuna wazazi telekezi, wazazi kiimla, wazazi katili, wadekezaji , ruksa na wazazi wenye mamlaka. Alisema kwa kutuumia njia hizo ndizo unaweza kuona ni kwa jinsi gani watoto wao wanaweza kuwa na mwelekeo mwema katika jamii.
Alisema anachukizwa sana na tabia ya `michepuko’ inayozidi kushika kasi katika familia za Watanzania. Tabia hiyo ya michepuko imeingia zaidi kwa wanandoa kiasi kimefanya familia nyingi kutelekezwa na watoto na mama kupata shida na machungu mengi.
Padri Remisho alisema atapeleka ombi kwa Kardinali Pengo aruhusu na kutoa mamlaka kwa viongozi wa jumuiya waweze kuwafichua wale wote wenye michepuko. Alibainisha sio kwenye sakramenti ya ndoa tu ni kwa sakramenti zote za utawa na upadri.
HABARI LEO.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment