Saturday, 28 March 2015

SIMBACHAWENE AIOMBA BENKI YA DUNIA KUISAIDIA TANESCO

00Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (mbele ) akiongoza kikao kilichokutanisha ujumbe kutoka Benki ya Dunia na watalaam wa Wizara ya Nishati na Madini ili kujadili maendeleo ya miradi ya nishati nchini inayofadhiliwa na Benki hiyo, changamoto zake na kupata mapendekezo ya kuboresha miradi hiyo.


……………………………………………………………………………….
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ameliomba Shirika la Fedha Duniani (WB) kulisaidia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) ili liweze kuimarisha miradi ya usambazaji wa umeme nchini hususan vijijini.
Simbachawene aliyasema hayo wakati alipokutana na ujumbe kutoka Benki ya Dunia na watalaam wa Wizara ya Nishati na Madini ili kujadili maendeleo ya miradi ya nishati nchini inayofadhiliwa na Benki hiyo, changamoto zake na kupata mapendekezo ya kuboresha miradi hiyo.
Alisema kuwa Tanesco inakabiliwa na changamoto ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya umeme hususan usambazaji wa umeme vijijini na kupelekea miradi mingi kutokamilika kwa wakati.
Akielezea maendeleo ya shirika hilo la umeme, Simbachawene alisema kuwa shirika hilo limeongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato kwa kubuni mikakati mbalimbali ya ukusanyaji wa mapato hayo na kupunguza hasara zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara.
Akielezea kuhusu upunguzaji wa bei ya umeme nchini, Simbachawene alisema kuwa Serikali imejenga bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam jambo litakalochangia upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika na kwa gharama nafuu ambalo ni moja ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
“ Ili kuhakikisha wananchi wananufaika na sekta mpya ya gesi, serikali ilibuni utaratibu wa kusomesha wataalam pamoja na wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi katika vyuo vikuu vinavyotoa fani za mafuta na gesi ili kuwa na wataalamu watakaosimamia kwa ufanisi sekta ya gesi na mafuta.,” alisema Simbachawene 
Aliongeza kuwa mara baada ya kuwa na wataalam waliobobea katika masuala ya gesi na mafuta, serikali itaunda taasisi itakayokuwa na kazi ya kutoa ushauri katika masuala ya gesi na mafuta hususan wakati wa uingiaji wa mikataba
“ Kwa mfano kuna uwekezaji mkubwa unaohitaji mamilioni ya Dola za Marekani, kwa mfano Ujenzi wa Viwanda vya Gesi ya Kimiminika (LNG), uwekezaji huu unahitaji timu ya wataalam watakaohakikisha kuwa maslahi ya nchi yanazingatiwa,” alisisitiza Simbachawene.
Aliongeza kuwa, mbali na kuzalisha wataalam, serikali kwa sasa inaandaa sheria kwa ajili ya sekta za gesi na mafuta ambapo mpaka sasa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali yamekusanywa na kujumishwa.
Akielezea kuhusu uwazi katika mikataba ya gesi na mafuta, Simbachawene alisema kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kunakuwepo na uwazi katika shughuli zake, moja ya mikakati hiyo ni pamoja na kujiunga na Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (EITI) ambapo taarifa mbalimbali za malipo na makusanyo katika sekta za madini na gesi zimekuwa zikikusanywa na kusambazwa kwa wananchi.
Aliendelea kusema kuwa, Serikali inafuata sheria zinazosimamia utoaji wa taarifa za mikataba. 
Wakati huo huo Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi, Philippe Dongier alisema kuwa Benki ya Dunia ipo tayari kushirikiana na Serikali kupitia Shirika la Tanesco ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme wa uhakika na nchi kutoka katika kundi la nchi masikini dunaiani na kuwa katika kundi la nchi zenye kipato cha kati.
Dongier alisema awali Benki ya Dunia ilijitosa kuisaidia Tanesco ili iweze kutoka kwenye utegemezi wa chanzo kimoja cha nishati ya umeme yaani maji na kutumia vyanzo vingi ikiwa ni pamoja na kupelekea ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi jijini Dar es salaam ambalo mara baada ya ukamilishwaji wake litapunguza gharama ya uzalishaji wa umeme na wananchi wengi kunufaika na nishati hiyo.
Pia Dongier alimpongeza Waziri Simbachawene kwa hatua ya serikali kujenga bomba la gesi na kasi ya uandaaji wa sera kwa ajili ya usimamizi wa sekta mpya za gesi na mafuta na kusisitiza kuwa Benki ya Dunia ipo tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa malengo yake yanatekelezwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!