Monday 2 March 2015

SH MILIONI 10 KUNUNULIA MBOGA NI KEBEHI"

Vyombo vya habari jana viliandika kuhusu mahojiano baina ya Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma na viongozi wawili wa umma, Andrew Chenge na Profesa Anna Tibaijuka ambao wametuhumiwa kukiuka maadili katika sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.

Chenge alifikishwa mbele ya chombo hicho akituhumiwa kutumia nafasi yake ya zamani ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kujinufaisha na mkataba wa kuzalisha umeme kati ya Serikali na kampuni binafsi ya IPTL ambayo inaliuzia nishati Shirika la Umeme (Tanesco).
Profesa Tibaijuka anatuhumiwa kukiuka maadili kwa kuingiziwa Sh1.6 bilioni kwenye akaunti yake akiwa kiongozi wa umma tofauti na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Chenge alizuia shauri lake lisijadiliwe baada ya kuomba Mahakama Kuu itoe tafsiri ya zuio la mahakama dhidi ya vyombo vya Serikali kujadili kashfa ya escrow.
Hata hivyo shauri la Profesa Tibaijuka lilijadiliwa na sasa, kwa mujibu wa taratibu litawasilisishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa hatua zaidi.
Kilichoshangaza na kuwaacha wengi midomo wazi ni jinsi Tibaijuka, mbunge wa Muleba Kusini, alivyojitetea kuhusu matumizi ya Sh10 milioni alizochukua kutoka kwenye akaunti yake baada ya kuingiziwa na mmiliki wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira. Alipoulizwa sababu za kuchota fedha hizo kwenye akaunti wakati anadai aliziomba kwa ajili ya shule yake, waziri huyo wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alijibu kuwa fedha alizotoa zilikuwa ni kwa ajili ya “kununua mboga”.
Mkurugenzi huyo wa zamani wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UNHabitat) anaweza kutoa maelezo mengi kufafanua suala hilo, lakini hayataweza kufuta dhana kuwa amefikia kiwango cha juu cha kebehi kwa Watanzania wengi ambao kwa viwango vya kimataifa, hata UNhabitat, wanaishi chini ya Dola 1 ya Marekani (yaani Sh1,820 za Tanzania). Kwa taifa ambalo asilimia 36 ya wananchi wake wanaishi chini ya hali ya umaskini, kauli hiyo siyo mzaha kwa wajumbe wa Sekretarieti ya Maadili, bali ni shambulio kubwa kwa wananchi ambao wamekata tama ya maisha, kwa vijana ambao wanashindia pombe kali za kwenye pakti kujisahaulisha machungu ya maisha; kwa wakulima ambao wanalazimika kula mizizi kutokana na njaa; kwa wafanyakazi ambao mishahara yao haitoshi kupanda magari wawahi kazini na kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata kibarua pia wanafunzi wanaokosa mikopo kujiendeleza na masomo ya juu.
Hawa wote wanaposikia kiongozi wa umma anachukua Sh10 milioni kwa ajili ya mboga, wanakata tamaa ya maisha zaidi kiasi kwamba huwezi tena kuwaambia wafanye kazi kwa bidii ili wapate mafanikio wakati wanajua wako wanaotumia kiasi kikubwa cha fedha kununulia mboga.
Profesa Tibaijuka siyo kiongozi pekee wa umma ambaye amewahi kutoa maneno kama hayo wakati akiwa akikabiliwa na tuhuma nzito. Akiwa anakabiliwa na tuhuma za kuhusika kwenye sakata la ununuzi wa rada kwa bei ambayo inaumiza uchumi wa nchi na taarifa kuwa aliweka Sh1.8 bilioni kwenye akaunti yake nje ya nchi, fedha zilizohusishwa na kashfa hiyo, Chenge alijibu kirahisi kuwa pesa hizo ni “vijisenti tu”.
Mapato ya viongozi wa umma yanajulikana na iwapo walipata kabla ya kuingia madarakani, wanatakiwa watangaze na kuboresha taarifa za mali zao kila wanapopata zaidi. Inapotokea vyombo vinavyowakilisha wananchi vinahoji kuhusu ongezeko la ghafla la mali, ni vizuri wakatoa maelezo yasiyokera na yasiyoongeza hasira kwa wananchi maskini.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!