BUNGE limetuma salamu kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari kwa kupitisha Muswada wa Takwimu wa Mwaka 2013, ambao pamoja na mambo mengine unataka mwandishi atakayefanya makosa kwenye kuripoti taarifa za takwimu kufungwa jela miaka mitatu ama kutozwa faini ya Sh milioni 10.
Muswada huo umepitisha wakati ambapo, Machi 31, mwaka huu Serikali inatarajiwa kuwasilisha muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa Mwaka 2015 na ule wa Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015, yote kwa hati ya dharura.
Tayari wadau wa habari wameshapinga kuwasilishwa kwa miswada hiyo kwa hati ya dharura wakisema wanataka washirikishwe ili wajue kilichomo ndani yake.
Awali muswada wa takwimu uliwasilishwa kwenye mkutano wa 17 uliofanyika Novemba mwaka jana, ambapo baada ya wabunge kupinga vifungu vinavyobana waandishi, Serikali iliutoa bungeni kwa maelezo kuwa inaenda kuurekebisha.
Jana Bunge lilivyokaa kama kamati ili kupitisha muswada huo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alihoji juu ya kifungu hicho kinachotoa adhabu kali na Serikali kusema imekifanyia marekebisho.
Hata hivyo, mbunge huyo alisema hakuna kilichofanyiwa marekebisho na kuwa adhabu bado inaendelea kuwa kali. Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), alihoji iweje Serikali iweke kinga kwa mtumishi wa Serikali anayetoa taarifa zisizo sahihi, lakini ikaacha kuweka kwa mwandishi anayepewa taarifa zisizo sahihi na ofisa huyo wa Serikali na kuziripoti.
Akijibu hoja hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema “ataenda kujieleza mahakamani ama polisi”.
Kabla ya kuondolewa bungeni Novemba mwaka jana, muswada huo pamoja na mambo mengine, ulikuwa ukipedekeza faini ya Sh milioni 10 au adhabu isiyopungua kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa chombo cha habari kitakachotoa taarifa za kitakwimu za uongo au zenye upotoshaji.
Chanzo:Mtanzania
No comments:
Post a Comment