Tofauti na nyota wengi wa michezo duniani ambao wakistaafu hugeuka ombaomba, nyota wa zamani wa kikapu wa Ligi Kuu ya Marekani (NBA), Michael Jordan amezidi kupaa juu kwa mafanikio (utajiri).
Nyota huyo wa zamani wa timu ya Chicago Bulls ametangazwa kuwa miongoni mwa mabilionea wapya.
Jarida la kibiashara la Forbes katika orodha yake mpya ya Machi 2015, limemtaja Jordan.
Kulingana na jarida hilo, Jordan anao utajiri wa zaidi ya dola bilioni moja ambazo amezipata kutokana na uwekezaji baada ya kung’atuka mchezo ambao umemjengea heshima kubwa duniani.
Hadi sasa, Jordan ambaye alikuwa na wastani wa pointi 30.12 kwa kila mchezo wakati akicheza mpira wa kikapu, rekodi ambayo haijavunjwa hadi sasa, ndiye mchezaji aliyelipwa kiasi kikubwa cha fedha, dola 90 milioni.
Mbali ya malipo hayo, mkataba wake na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike, ambako waliunda tangazo la Air Jordan umeendelea kumwingizia kiasi kikubwa cha fedha.
Mzaliwa huyo wa North Carolina, ambaye alitwaa mataji sita ya NBA, medali mbili za dhahabu za Olimpiki, ni sifa nyingine ambazo anajivunia.
Kwa sasa, ndiye mmiliki wa klabu ya Charlotte Hornets, ambayo inashika nafasi ya kumi kwenye Ukanda wa Mashariki katika ligi ya NBA, mafanikio ambayo yamemsaidia Jordan kupenya na kuingia kwenye orodha ya mabilionea wapya.
Timu hiyo imepanda thamani katika kipindi cha mwaka uliopita baada ya kuuzwa kwa klabu ya Los Angeles Clippers kwa dola 2 bilioni, mauzo ambayo yamepandisha bei ya bidhaa zote za NBA kwenye soko la hisa.
Hata hivyo, Steve Ballmer, mmiliki wa klabu nyingine ya NBA, Clippers, ambaye timu yake ina thamani ya dola 700 milioni yuko mbele ya Jordan.
Klabu hiyo ya Charlotte Hornets ilitathminiwa kwa dola 275 milioni mwaka 2010. Ballmer, ana utajiri wenye thamani ya dola 21.5 bilioni.
Hata hivyo, Jordan amebadili biashara yake tangu alipostaafu mpira wa kikapu miaka kumi iliyopita.
Wakati akicheza kikapu alikuwa kitambulisho halisi cha NBA ambako ligi hiyo iliingiza kiasi kikubwa cha fedha.
Kulingana na orodha mpya ya Forbes, Jordan ameingia kwenye orodha ya mabilionea 290 duniani.
Hao ni pamoja na wamiliki wa klabu za michezo kama vile, Micky Arison wa Miami Heat, Mikhail Prokhorov wa Brooklyn Nets au Stan Kroenke wa Denver Nuggets.
Jordan, mwenye umri wa miaka 52 ameungana na matajiri hao akiwa na umri mdogo.
Maisha yake;
Kuzaliwa: Februari 17, 1963
Umri: Miaka52:, Brooklyn,
New York City, Marekani
Urefu: Mita 1.98
Wake: Yvette Prieto (Ndoa 2013),
Juanita Vanoy (Ndoa 1989–2006)
Watoto: Jasmine Mickael Jordan,
Marcus Jordan, Jeffrey Michael
Jordan, Ysabel Jordan,
Victoria Jordan
Wazazi: Deloris Peoples,
James R. Jordan, Sr.
No comments:
Post a Comment