Sunday 1 March 2015

MAPYA YAIBUKA DAWA ZA KOREA KASKAZINI



Sakata la dawa za tiba asili na tiba mbadala zinazotolewa kwenye zanahati zinazomilikiwa na raia wa Korea Kaskazini, limechukua sura mpya kufuatia kuibuka taarifa zaidi zinazohusu huduma hizo.



Wiki iliyopita, gazeti hili lilichapisha habari kuhusu zahanati hizo zilizopo  Temeke, Kariakoo, Magomeni  jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, kwamba zinatoa dawa zisizokuwa na majina wala maelezo ya viambato.

Baadhi ya watu walioongea na NIPASHE wamethibitisha kupata huduma kwenye zahanati hizo ambapo walipewa matokeo ya ugonjwa wasiougua.

Moja ya vyanzo vya kuaminika kilieleza namna kilivyokwenda kwenye moja ya zahanati hizo na kupewa majibu ya kuwapo kiwango kikubwa cha ‘kilevi cha sigara’ na kutakiwa kutumia dawa ili apone.

Ingawa kuna uwezekano kwa mujibu wa tafiti za kisayansi, kwa mtu asiyevuta sigara kuathirika kutokana na
kufikiwa na moshi wake, lakini hali hiyo inachangiwa na ukaribu wa muda mrefu kati ya mvutaji wa sigara, jambo ambalo chanzo hicho kilikana.

“Sina rafiki anayevuta sigara na kwa umri wangu huu, hivi sasa muda mrefu ninakuwa nyumbani sasa nilishangazwa kuambiwa nina kiwango kikubwa cha ‘kilevi cha sigara’ mwilini,” alidai mtoa taarifa huyo ambaye cheti cha matibabu kinaonyesha kuwa na miaka 61.

Pia, uchunguzi wa gazeti hili ulifanikisha kupata majawabu ya mtu ambaye hakuwahi kuugua kifua na mapigo ya moyo kwenda kasi, lakini alipojaribu kubaini umakini wa zahanati hizo, alijibiwa kuwa na `magonjwa’ hayo kwa kiasi kikubwa.

Kisha, walimuuzia dawa zisizokuwa na majina wala maelezo ya viambato. Pia alipewa ratiba ya kurejea kwenye zahanati hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kupata  ushauri na dawa zaidi za kuponesha `magonjwa’ hayo.

Ilielezwa kuwa licha ya kuwapo viwango vya madini chuma vinavyotambuliwa kwa baadhi ya nchi zikiwamo za Asia kama ilivyo Korea Kaskazini, dawa hizo zilibainika kuwa na kiasi kikubwa cha madini chuma yanayoweza kusababisha athari za muda mrefu kwa mtumiaji.

Mtafiti wa dawa ya figo nchini, Dk. Danny Kyauka, anasema watu wengi wanakwenda kwenye zanahati hizo kutokana na kushamiri kwa utapeli unaofanywa na baadhi ya watu wanaojihusisha na tiba asili na tiba mbadala nchini.

Alisema, kutokana na hali hiyo baadhi ya Watanzania wanalazimika kushawishika kwenda kwa wataalamu wa tiba hizo kutoka nje ya nchi ikiwamo Korea Kaskazini.

“Watu wanapoteza imani na watoa huduma wa ndani baada ya kugundua wana ubabaishaji mkubwa,” alisema katika mahojiano na NIPASHE Jumapili nyumbani kwake Magomeni Mwembechai.

Dk. Kyauka, alisema amefanya utafiti wa tiba ya asili kwa miaka mingi hivyo anajua jinsi watu wasiokuwa waaminifu wanavyotumia vibaya tiba hiyo kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

HATUPELEKI DAWA NJE
Dk. Kyauka, alishauri serikali kuharakisha mchakato wa kusajili dawa za tiba asili na tiba mbadala nchini, ili zifikie hatua ya kusafirishwa kwa wingi nje ya nchi. Alitoa mfano wa dawa ya figo ya Billyd Formula Power (aliyoigundua), kwamba imeshindwa kusajiliwa baada ya kukosekana kwa chombo cha kufanya hivyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!