Mwakilishi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Kanda ya Kati, Charles Ambele, amesema uzimaji wa mitambo ya analojia ya utangazaji wa televisheni mkoani Kigoma, utafanyika Machi 31, mwaka huu.
Ambele aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waaandishi wa habari kuwa vigezo vinavyotumika kuzima mitambo ya analojia ni pamoja na kuwepo utangazaji wa mifumo ya analojia pamoja na kidijitali kwenye eneo husika, upatikanaji ving’amuzi na uwepo wa chaneli tano za kitaifa kwenye mfumo huo mpya.
Alisema elimu ya umma kupitia njia mbalimbali kuhusu kuhamia katika teknolojia ya mfumo wa utangazaji wa dijitali imekuwa ikitolewa kwa kiwango cha kuridhisha. Matangazo ya dijitali yamewafikia watu asilimia zaidi ya 20 kati ya asilimia 24 waliyokuwa wanapata matangazo ya televisheni ya analojia.
Aidha alisema utaratibu wa kuzima mitambo ya analojia utakuwa kwa maeneo yenye matangazo ya dijitali tu. Maeneo ambayo hayana miundombinu ya dijitali hayatazimwa kwa sasa hadi yapate dijitali.
Alisema mabadiliko hayo hayahusu matangazo kwa njia ya utangazaji wa satelaiti, waya, kebo na redio. “Tunawataka wananchi Mji wa Kigoma wasizitupe Tv zao za analojia bali wanunue ving’amuzi ili kupata matangazo ya dijitali”. Ambele alisema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeagiza watoa huduma za usambazaji wa ving’amuzi waliyoko Mkoa wa Kigoma, kuhakikisha kuwa kuna ving’amuzi vya kutosha.
Aidha, alisema serikali inatarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni wa mfumo wa analojia hapa ili kufanikisha zoezi hili.
Alisema kulingana na ratiba iliyotolewa na serikali Februari 2014 awamu ya pili ya uzimaji wa mitambo ya analojia ulianza kwenye miji ya Singida na Tabora, wakati ambapo miji mingine iliyofuata katika uzimaji wa mitambo ya analojia ambayo ni Musoma, Bukoba na Morogoro, Kahama na Songea ilihusuka katika uzinduzi wa mitambo ya dijitali ikizingatiwa kuwa haikuwa ya matangazo ya televisheni ya mfumo wa analojia.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment