Saturday 14 March 2015

JK. JANGA HILI SI UCHAWI


Rais Jakaya Kikwete amewataka waathirika wa mvua ya mawe na upepo mkali katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama, Shinyanga kutohusisha tukio hilo na imani za kishirikina.



 
Akizungumza mara baada ya kuwatembelea waathirika hao na kujionea uharibifu uliofanywa na mvua hiyo katika kijiji cha Mwakata juzi, Rais Kikwete alitaka familia zilizopatwa na athari kuachana na kuhusisha mvua hizo na ushirikina.
 
Alisema tukio hilo ni mabadiliko ya hali ya hewa, hivyo aliwataka wananchi kuondokana na imani za ushirikina na kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kupigiwa ramli ili kutafuta ‘aliyewaroga’.
 
“Poleni sana kwa tatizo hili ndugu zangu, janga hili ni janga la kitaifa ambalo limemgusa kila mtu, ila msilihusishe tukio hili na imani za kishirikina kwa kwenda kwa waganga wa kienyeji kumtafuta mchawi…waganga watawapotosha tu na kuanza kuuana kwa kukatana mapanga zaidi mnatakiwa muwe wavumilivu,” alisema Kikwete.
 
Aidha, Kikwete aliwataka wananchi hao kuamini pamoja na kupoteza watoto katika janga hilo, Mungu atawabariki na kuzaa wengine wengi zaidi.
 
Hata hivyo, alisema pamoja na mvua hiyo kuharibu makazi ya watu kwa kaya 468 kukosa makazi, lakini Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) litaanza kuwajengea nyumba mpya katika kipindi cha siku 90 zijazo ili waweze kurejea katika makazi yao na wanafunzi kuendelea na masomo.
 
Naye Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, alimuomba Rais Kikwete kuangalia uwezekano wa kuvifutia kodi vifaa vya ujenzi ili kutoa fursa kwa wananchi wa kipato cha chini kujenga nyumba imara kwa kutumia saruji.
 
Maige alisema nyumba nyingi za waathirika hao zilianguka kutokana na kujengwa kwa matofari ya tope.  
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!