Sunday, 29 March 2015

HAKUNA MPANGO WA KUANZISHA MAHAKAMA YA KADHI-KIKWETE



Rais Jakaya Kikwete amefunga rasmi mjadala wa Mahakama ya Kadhi na kwamba hakuna mpango wa kuianzisha.


Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana  jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na kamati ya amani ya viongozi wa dini mkoa wa Dar es Salaam.
Kauli hiyo ya Kikwete imekuja baada ya hivi karibuni,  viongozi dini za Kikristo chini ya Jukwaa la Wakristo Tanzania, kutoa tamko la kuitaka Serikali isitishe mchakato wa Mahakama ya Kadhi kwa kuondoa muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 02 wa mwaka 2014 unaopendekeza.
Pia waliitaka serikali pamoja na mambo mengine, kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislamu, Sura ya 375 (The Islamic Law (Restatement) Act, Cap.375) ambao ulitarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa 18 wa Bunge unaoendelea Dodoma, ikiwa ni ahadi ya Serikali iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Baada ya tamko la maaskofu mijadala mbali mbali iliibuka huku wengine wakiwaunga mkono na wengine wakipinga kitendo chao cha kuwataka waumini wa kikristo, kushiriki mchakato huo lakini wakati wa kura ya maoni wapige kura ya hapana.
Katika mkutano wake na viongozi wa dini, jana Rais Kikwete aliainisha mambo matatu ambayo ni amani, katiba mpya na mahakama ya kadhi ambayo angependa kuyatolea ufafanuzi.
Alisema kuhusu suala la mahakama ya kadhi, uamuzi wa serikali ni kutoanzisha mahakama hiyo..
 Aidha, alisema waislam hawazuiwi kuanzisha mahakama hiyo na watakapoamua kufanya hivyo serikali haitaiendesha.
KATIBA MPYA
Aliwataka viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao kushishiriki katika mchakato wa kuupigia kura.
Alisema matamko ya baadhi ya viongozi wa dini ya kuwahimiza waumini kuikataa katiba mpya, yamemshangaza na kumsikitisha.
“Hatukutegemea viongozi wakuu kutamka hivyo licha ya haki yao ya msingi ya kutoa maoni,” alisema.
Alisema katiba iliyopo sasa inatambua hali ya kuabudu katika vifungu vya haki ya mawazo, uchaguzi wa dini na imani na kutokuwa na dini.
Askofu  Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa alisema kuwa, alisema watanzania wajielimishe na kuisoma katiba.
 Naye, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salim, alisema viongozi wa dini wamejipanga kumaliza matatizo ya mauaji ya albino na mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!