Magonjwa ya mfumo wa njia ya mkojo na figo ni kati ya maradhi yanayowasumbua watu wengi duniani.
Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kukojoa mkojo wenye harufu mbaya au mkojo wenye rangi ya maziwa au damu.
Mgonjwa pia hupata maumivu ya kiuno na tumbo chini ya kitovu, kukojoa mkojo kidogo mara kwa mara na kupata hisia za maumivu wakati wa kujisaidia haja ndogo.
Kukojoa damu ingawa ni mojawapo ya dalili za ugonjwa huu, lakini mara nyingi husababishwa na ugonjwa wa kichocho au mawe katika kibofu au katika figo. Ugonjwa wa kifua kikuu katika mfumo wa mkojo pia unaweza kusababisha dalili hii. Dalili nyingine hasa kwa watoto ni mwili kuwa na homa kali kama ile ya malaria.
Utambuzi wa tatizo hili kwa wasichana na wanawake wengi unaweza kuwa mgumu hasa pale wanapojihusisha na ngono hatarishi.
Wanawake wengi wa rika mbalimbali kuanzia vichanga hadi watu wazima na vikongwe wanaweza wakakabiliwa na tatizo hili. Baadhi ya takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 10 ya wanawake wote duniani hupata tatizo la maradhi ya ngono kila mwaka.
Takimu zingine za afya ya jamii zinaonyesha kuwa, tatizo la ugonjwa wa uambukizo katika njia ya mkojo huwapata wanawake takribani mara kumi zaidi ya wanaume.
Wachunguzi wa masuala ya afya ya wanawake wanaongeza kusema kwamba wanawake wenye umri kati ya miaka 16 na 35 ndiyo wanaopata maradhi haya mara kwa mara.
Wengi wao hushindwa kuwaeleza madaktari kuhusu hali zao kuhusiana na tatizo hili kutokana na kuona aibu au kuwa na hofu ya kushukiwa kuwa ni wazinifu.
Katika utafiti uliofanywa na Ahamed Al-Badr na Ghadeer Al-Shaikh wa Saudi Arabia, ulibaini kuwa asilimia 60 ya wanawake hukabiliwa na tatizo hili.
Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la kitabibu la Chuo Kikuu cha Sultan Qaboos toleo la mwaka 2013, ulibaini kuwa wanawake wanene na wale wenye ugonjwa wa kisukari, wako katika hatari kubwa ya maradhi haya ya njia ya mkojo.
Utafiti huo unaongeza kusema kuwa tatizo huwa kubwa zaidi kadri umri wa mwanamke unavyoongezeka.
Dk. Jana Kubrin Dickter wa Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza cha Hospitali ya Kaiser Permanente Fontana iliyoko Marekani anasema “Ugonjwa wa uambukizo katika njia ya mkojo ni tatizo linalojitokeza mara kwa mara kwa wanawake waliokoma kupata damu ya hedhi”
Katika utafiti mwingine uliofanywa hapa nchini na kuchapishwa mwaka 2009 na A. Masinde pamoja na wenzake kutoka katika Kitengo cha Magonjwa ya Wanawake cha Hospitali ya Bugando Mwanza, ilibainika kuwa wanawake wengi wajawazito wanakabiliwa na tatizo hili. Na miongoni mwao wengi huwa hawaonyeshi dalili za moja kwa moja za maradhi haya.
Wanawake wengi wanaopata tatizo la uambukizo katika njia ya mkojo, hawana habari za kutosha zilizo sahihi juu ya vyanzo na madhara ya tatizo hili linalosumbua mamilioni ya wanawake duniani.
Hii huwafanya wengi wachelewe kupata huduma sahihi za matibabu, jambo ambalo huambatana na athari nyingi za kiafya na kiuchumi kwa familia zao na taifa kwa ujumla.
Magonjwa ya njia ya mkojo mara nyingi hutokana na uambukizo wa bakteria katika njia ya mfumo wa mkojo. Bakteria hawa hushambulia figo, mirija miwili inayotoa mkojo ndani ya figo kupeleka katika kibofu cha mkojo.
Mara nyingi uambukizo huo unaotokana na bakteria huanzia katika uke na kuingia ndani ya njia ya mkojo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba njia ya mkojo ya mwanamke kutoka ukeni hadi ndani ya kibofu ni fupi sana na inakaribiana na njia ya haja kubwa.
Ufupi wa njia hii huwezesha bakteria kuingia kwa urahisi zaidi katika kibofu cha mkojo na kusababisha uambukizo katika mfumo wa mkojo.
Baadhi ya bakteria wanaosababisha uambukizo katika njia hii kwa kawaida huishi ndani ya matumbo yetu na hutoka nje pamoja na kinyesi wakati tunapojisaidia haja kubwa.
Sababu zingine zinazochangia kutokea kwa ugonjwa huu ni pamoja na wanawake wengi kutozingatia usafi wa sehemu za siri hasa wakati wa kujisaidia.
Wasichana na wanawake wengi wanapomaliza kujisaidia haja kubwa, hujisafisha katika njia ya haja kubwa kabla ya kusafisha ukeni. Jambo hilo husababisha bakteria kuchukuliwa kwa mikono toka katika njia ya haja kubwa na kuwaingiza ukeni.
Kufanya tendo la ngono kwa muda mrefu au kushikashika viungo vya kike bila kunawa kwa maji safi na sabuni, kunaweza kuwa chanzo cha tatizo hili pia. Kufanya hivyo husababisha bakteria waingie kwa urahisi ndani ya kibofu na kuleta uambukizo.
Wataalamu wa masuala ya afya ya wanawake wanakadiria kuwa kati ya asilimia 75 hadi 90 ya maambukizi katika njia ya mkojo kwa wasichana na wanawake wanaoshiriki tendo la kujamiiana hutokana na kufanya ngono mara kwa mara.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa L.E.Nicolle wa mwaka 2008 uliochapishwa katika jarida la The Urologic Clinics of North America. Nicolle ni mtaalamu wa sayansi ya maikrobailojia katika Chuo Kikuu cha Manitoba, nchini Canada.
Jambo lingine linalowaweka wanawake wengi katika hatari hii, ni kunawa kwa maji yenye povu jingi la sabuni au kutumia sabuni yenye kemikali kali kusafisha ukeni. Sabuni zenye kemikali husababisha uvimbe ndani ya njia ya mkojo na husababisha athari katika njia ya mkojo.
Ukeketaji wa wanawake au wasichana, kuumia kwa uti wa mgongo, ulemavu katika maumbile ya njia ya mkojo pamoja na kutokupata choo vizuri pia ni baadhi ya sababu zinazochangia kutokea kwa tatizo hili.
Lingine linalosababisha ukubwa wa tatizo hili kwa wanawake ni ile tabia ya kutokunywa maji ya kutosha.
Tabia nyingine hatarishi kwa wanawake na wasichana ni kukaa na mkojo kwa muda mrefu bila kwenda kujisaidia hasa wawapo safarini.
Mkojo unapokaa katika kibofu kwa muda mrefu hutoa nafasi kwa bakteria kuzaliana kwa wingi na kusababisha kibofu kishindwe kufanya kazi zake vizuri.
Kukaa na mkojo kwa kipindi kirefu pia huwapa nafasi bakteria kupanda juu katika mirija inayotoa mkojo ndani ya figo na kufanya mashambulizi.
Kukaa kwa muda mrefu na vitambaa vya kukinga damu ya hedhi bila kubadilisha pia huchangia kwa kiwango kikubwa kutokea kwa tatizo hili.
Baadhi ya wanawake hutumia vitambaa ambavyo si salama kwa afya kiasi kwamba huwawia vigumu kuepuka tatizo hili kila mara wawapo katika siku za hedhi.
Magonjwa ya njia na mfumo wa mkojo kwa wasichana na wanawake kwa ujumla ni chanzo kikubwa cha upotevu wa mapato ya familia kutokana na ununuzi wa dawa na kulipia gharama za matibabu na pengine kulazwa hospitalini mara kwa mara.
Mwanamke anayelazwa hospitalini kutokana na matatizo yatokanayo na maradhi katika njia ya mkojo anatazamiwa kukaa hospitalini kati ya siku nne hadi sita akiendelea kupata matibabu.
Hiki ni kipindi kirefu hasa katika nyakati hizi ambapo hali ya maisha inazidi kuwa ngumu kiuchumi. Lakini pia magonjwa mengine yanayoshambulia mfumo wa mkojo yanaweza kushambulia mfumo wa uzazi wa mwanamke na kusababisha matatizo kama vile ugumba, kuharibika kwa figo au shinikizo la damu na kiharusi.
Ni vema jambo hili likaeleweka vyema miongoni mwa wasichana na wanawake kwa ujumla ili tahadhari zichukuliwe mapema.
Pale msichana au mwanamke anapogundua kuwa ana ugonjwa katika njia ya mkojo, asichelewe kupata huduma za tiba.
Hospitali nyingi nchini zinao wataalamu wanaoweza kutibu tatizo hili kwa ufanisi mkubwa endapo mgonjwa atawahi kupata tiba. Lakini tatizo hili linaweza kuzuilika endapo wanawake watazingatia kanuni za afya na usafi wa mwili kikamilifu.
No comments:
Post a Comment