Wednesday, 25 February 2015
WAHIMIZWA KUTOA USHAHIDI
WANANCHI wametakiwa kutoa ushahidi mahakamani kwa watu wanaofanya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kama ndiyo njia pekee ya kukomesha matukio hayo.
Mkurugenzi wa Mashtaka na Makosa ya Jinai Zanzibar, Ibrahim Mzee alisema hayo wakati akipokea vifaa vilivyotolewa na shirika la watoto Save Children Fund kwa ajili ya kusaidia mwenendo wa kesi mahakamani.
Alisema matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku na kuzua malalamiko makubwa kwa wazazi mbele ya vyombo vya sheria ikiwemo Mahakama na Polisi.
Hata hivyo, alisema usiri wa wazazi kushindwa kuripoti matukio ya vitendo vya udhalilishaji na ubakaji vinavyofanyika katika jamii na familia vimechangia kuendelea kuwepo kwa vitendo hivyo.
“Moja ya tatizo kubwa linalotukabili sasa ni wazazi kutoshirikiana na vyombo vya sheria katika kukabiliana na matukio hayo ya ubakaji kwa sababu bila ya ushahidi huwezi kumtia mtu hatiani,” alisema.
Ofisa Mwandamizi wa Shirika la Save Children Fund Joyce ameitaka jamii zaidi kufichua wabakaji ili kuweza kutiwa hatiani mbele ya vyombo vya sheria kwa sababu watoto wamekuwa wakiathirika kwa kiwango kikubwa.
“Tunaiomba ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka na makosa ya jinai kuzifuatilia kwa karibu kesi za watoto zinazohusiana na udhalilishaji wa kijinsia na ubakaji ambazo zimekuwa zikiongezeka,” alisema.
Aliyataja matukio yanayoongoza kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ni mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment