RAIS wa Marekani, Barack Obama amesema kuwa nchi yake hapigani vita dhidi ya Waislamu bali inapigana vita dhidi ya magaidi wanaouchafua Uislamu.
Rais huyo amefafanua kuwa taifa la Marekani linawapinga watu wanaotumia dini ya Kiislamu kuupotosha umma na kuendeleza itikadi kali ambazo zinaleta machafuko ulimwenguni.
Rais Obama aliyasema hayo katika mkutano wa siku tatu unaoendelea huko mjini Washington ambapo amesema dunia inatakiwa kukabiliana na makundi ya aina hiyo.
Aidha Rais Obama amewahimiza viongozi wa nchi za Magharibi na viongozi wa dini ya Kiislamu duniani kote kuungana na kupambana na itikadi kali pamoja na wanamgambo wa Kiislamu wanaoendeleza itikadi kali wanaodai kuuwakilisha Uislamu.
Wakati huo huo, Rais Obama ameeleza kuwa manung'uniko waliyonayo vijana lazima yashughulikiwe ili kuondokana na hisia za makundi yenye misimamo mikali ya kiitikadi.
Rais Obama amesema juhudi zaidi zinahitajika kupambana na makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali kama dola la Kiislamu (IS) na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda ili kuyazuia makundi hayo kuwasajili wapiganaji zaidi na kueneza itikadi kali kwa waumini wengine.
Pia rais huyo ametoa wito kwa viongozi wa Kiislamu kuangazia dhana potofu kuhusu dini hiyo ili usambazwaji wa itikadi hizi zenye madhara zisiwepo tena.
Wawakilishi kutoka zaidi ya nchi sitini wanahudhuria mkutano huo ambao umekuja kufuatia mashambulio ya makundi ya Kiislamu katika nchi za Denmark, Ufaransa na Australia.
MAJIRA.
No comments:
Post a Comment