Saturday 14 February 2015

NSSF YASAIDIA MIL 3/- UJENZI WA MAABARA LUPANGA

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (Nssf) limetoa hundi ya shilingi milioni tatu kusaidia ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari ya mazoezi ya Lupanga, Kilakala Manispaa ya Morogoro.


 
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya hundi hiyo, Meneja uendeshaji wa Nssf, Morogoro, Mrisho Mwisimba, alisema kwa kutambua umuhimu wa masomo ya Sayansi, wameamua kutoa kiasi hicho baada ya kuombwa msaada huo wakati wa mahafali ya kidato cha nne mwaka jana.
 
Alisema kuwa Nssf kama mdau wa maendeleo katika Mkoa wa Morogoro imekuwa ikisaidia jamii kwa kutumia faida inayopata kutoka kwa wanachama wake ikiwa njia mojawapo ya kupata ukombozi katika nyanja za kiuchumi, afya na kijamii.
 
Alisema Nssf inatambua umuhimu wa elimu ya Sayansi kwa kuwa ndiyo chanzo cha maendeleo endelevu ya taifa lolote duniani katika kukuza maendeleo ya viwanda na miundombinu.
 
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Shule hiyo, Shangwe Mgheni, alisema kuwa kupitia mchango huo, watakamilisha chumba cha tatu cha maabara baada ya kukamilisha vyumba vingine viwili.
 
Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuwapatia vifaa vyote vya maabara.
 
Naye Mwalimu mkuu wa kitengo cha masomo ya Sayansi cha shule hiyo, Samuel Kaombwe, aliwataka wazazi kote nchini kuwashawishi watoto wao kuyapenda masomo ya Sayansi kwakuwa ulimwengu wa sasa ni wa Sayansi na Teknolojia.
 
Alisema kuwa iwapo kutakuwa na idadi kubwa ya wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi itasaidia nchi kuendelea kupata maendelea ya haraka na hivyo Taifa  kuondokana na umasikini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!