skip to main |
skip to sidebar
MWANAMKE MBARONI AKIUZA BINADAMU
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia mwanamke mmoja, Sophia
Chambo (30), mkazi wa Mtaa wa Polisi, Kata ya Lizaboni Manispaaya Songea, akituhumiwa kujihusisha na biashara ya kuuza binadamu kwa wafanyabiashara kwa ajili ya zindiko.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma,Mihayo Msikhela, alisema Februari 17, mwaka huu saa nane mchana, Sophia alikwenda kwa mtu mmoja (jina linahifadhiwa) kwa sababu za kiusalama kuwa akitaka afanikiwe afanye zindiko kwa kutumia maiti.
Kamanda, Msikhela alisema pamoja na mtuhumiwa huyo kutoa ushauri huo, bado alimtaka wafanye biashara na yeye, kwani angeweza kumletea mwili wa mama yake mdogo (jina tunalo) mkazi wa mtaa wa Ruvuma ambaye alikuwa na ugomvi naye.
Alisema alitaka alipwe sh.milioni 10 ili akamletee maiti ya mama huyo ikiwa kwenye gunia.
Alisema mtu huyo alikataa kupelekewa maiti na badala yake alimtaka apelekewe mtu mzima akiwa hai na kwamba kazi ya kumuua ataifanya yeye kwa makubaliano ya sh. milioni 6.5.
"Ndipo mtu huyo alitoa taarifa Polisi, hivyo kufanikiwa kuweka mtego na kumnasa Sophia," alisema Kamanda na kuongeza kuwa; "Siku ya pili Februari 18, mwaka huu asubuhi Sophia alikwenda nyumbani kwa mama yake mdogo ambaye anaishi Mtaa wa Ruvuma na kumlaghai kuwa kuna mtu alimwona Iringa na angependa kumwona ili aishi naye.
Mama yake mdogo alimwambia kuwa hajawahi kusafiri kwenda mkoani Iringa na kukutana na mwanamume. Kamanda, Msikhela, alisema baada ya Sophia kukwama kwa mbinu yake hiyo, alitumia uongo mwingine kwamba kuna matajiri wanataka mtu wa kumwajiri, ndipo mama yake mdogo huyo alikubali.
Bila kujua kinachoendelea alikubali kupelekwa kwa mtu aliyejifanya mnunuzi wa binadamu Mtaa wa Lizaboni. Alisema walipofika eneo la tukio walimkuta mnunuzi akiwa tayari anamsubiri Sophia ili aweze kumkabidhi huyo mama yake mdogo ili alipwe sh. milioni 6.5, bila ya kujua kwamba alikuwa anaingia kwenye mtego wa Polisi.
Kamanda, Msikhela, alisema upelelezi wa tukio unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili. Alisema wananchi waache kujihusisha na biashara ya binadamu kwani ni makosa kisheria.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia, Erick Bruno (30) kwa tuhuma za kumnyonga hadi kufa mpenzi wake, Daja Dungu (35) wakati walipokuwa kwenye nyumba ya kulala wageni (jina tunalo) Manispaa ya Morogoro.
Akizungumzia kutokea kwa tukio hlo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alisema tukio hilo lilitokea Februari 23, mwaka huu saa 6.30 usiku katika karakana ya Kichangani ambapo mtuhumiwa alikodisha chumba namba nane, akiwa na na mwanamke huyo.
“Februari 23, mwaka huu saa tisa na nusu mtuhumiwa alifika kwenye nyumba hiyo akiwa ameambatana na huyo mwanamke kwa lengo la kufanya ngono baada ya muda kukasikika kelele za kuomba msaada,” alisema Paulo.
Paulo alisema baada ya kelele hizo mlinzi wa nyumba hiyo aliwaita watu na kumtaka mtuhumiwa afungue mlango, lakini alikataa kwa kudai kuwa hakuna kitu kilichotokea, ndipo juhudi za kuufungua mlango zilifanyika na kumkuta mwanamke huyo akiwa amefariki.
Aidha, Paulo alisema Polisi bado haijafanikiwa kupata chanzo cha tukio hilo na kuwa upelelezi unafanyika ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.
Kamanda Paul, alisema mtuhumiwa anashikiliwa Polisi kwa upelelezi zaidi na mara baada ya kukamilika atafikishwa mahakamani
No comments:
Post a Comment