Tuesday 17 February 2015

MBARONI AKIDAIWA KUMUUA BABA YAKE


Mkazi wa Kitongoji cha Nyamorege kilichopo Mtaa wa Forodhani mji mdogo wa Sirari Wilaya ya Tarime mkoani  Mara, Marwa  Kihiri Mwita,  anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi Kihiri  Mwita kinyama kwa kumpiga na koleo kichwani na ubavuni.


Vilevile inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alijeruhiwa kwa kucharangwa kwa panga na baba yake huyo kabla ya kumjeruhi kwa kumpiga na koleo kichwani na ubavuni baada ya kuzuka ugomvi baina yao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Forodhani  Sirari,   Nyangoko Paulo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Ijumaa ya wiki iliyopita jioni katika  kitongoji hicho.
Paulo alisema kuwa ugomvi huo uliibuka baada ya baba kumtuhumu  mwanaye kuwa  anatabia ya wizi.
Alisema inadaiwa kuwa baba huyo alimweleza mwanaye huyo kuwa aliwahi kufanya wizi kitendo kilichosababisha kutozwa faini ya ng'ombe.
Paulo alisema inadaiwa kuwa baada ya baba kutoa tuhuma hizo, mwanaye alitoroka na kuwa nje ya familia kwa zaidi ya miaka mitano.
Alisema aliporudi nyumbani kwao, baba alikerwa na kuanza kumfukuza kwa panga ili asiingie ndani kwake huku akisisitiza aende  akaishi kwa wahalifu wenzake.
Mwenyekiti alisema baba akirusha panga na kumkata mkononi, mwanawe alichukua koleo na kumpiga nalo kichwani na ubavuni.
Alisema majirani walijitokeza kumuokoa na kuwakimbiza Hospitali ya Wilaya Tarime ambako alikufa kabla ya kuanza kupatiwa matibabu.
Polisi Tarime Rorya  wamethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kumshikilia mtuhumiwa huyo kwa mahojiano kisha atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
AUAWA DUKANI
Nao; Hassan Maulid (32), Hamad Hussein (25), Rashid Yusuph (21) na Abdallah Swalehe (25), wakazi wa Kijiji cha Porobanguma Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mfanyabiashara, Asheli Magina (40) kisha kumpora pikipiki na bidhaa mbalimbali baada ya kumvamia dukani alikokuwa amelala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema kuwa mtuhumiwa Maulid maarufu kwa jina la  Salama,  alikuwa akitafutwa na jeshi hilo kwa kuhusishwa na  mauaji ya  Ijumaa Said (30), mkazi wa kijiji cha  Monjore – Banguma kwa kumchoma kwa kisu.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, Said aliuawa Januari 19, mwaka huu majira ya  saa 12:30 jioni katika kijiji cha  Porobanguma baada ya kuibuka ugomvi kati yao.
Akizungumzia kuhusu mauaji ya Magina ambaye alikuwa mfanyabiashara na mkulima wa kijiji cha Bubutole,  alisema yalitokea Februari 11, mwaka huu usiku kwa kucharangwa mapanga kichwani na mikononi baada ya kumvamia nyumbani kwake wakati amelala dukani.
Alisema baada ya mauaji hayo, watuhumiwa hao wanadaiwa kupora pikipiki na bidhaa mbalimbali dukani hapo ambavyo thamani yake haijajulikana.
Misime alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na pikipiki hiyo T. 449 CQP aina ya SUNLG na bidhaa hizo mali ya marehemu huyo.
Alisema watuhumiwa hao pia walionyesha panga linalodaiwa kutumika katika mauaji ya Magina.
Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa mauaji hayo kukamilika. 

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!