Wednesday, 25 February 2015

KARANI WA BENKI ANAYEUZA FIGO YAKE ILI APATE MTAJI

Si ajabu kusikia mtu amejiua kwa sababu tu ya ugumu wa maisha. Wengi wanafikia uamuzi huo baada ya kuhisi hawana msaada mwingine wa kupunguza makali ya maisha. Hata hivyo, kujiua siyo njia sahihi ya kupambana na changamoto.

Hali imekuwa tofauti kwa kijana Armstrong Bangili aliyeahirisha uamuzi wake wa kutaka kujinyonga na sasa anafikiria kuuza figo yake. Anasema anaishi maisha ya tabu tangu alipofukuzwa kazi katika benki moja mwaka 1998.
Kabla ya kutekeleza ‘jaribio la kujiua’ wiki iliyopita, Bangili alisoma Gazeti la Mwananchi, toleo la Januari 3. Alipokutana na habari ya Andrew Chimulimuli kutoka Morogoro aliyetangaza kuuza figo yake kwa Sh90 milioni.
Anasema alipata tumaini kuwa hata yeye anaweza kuuza figo yake na kuondokana na umaskini unaomkabili kwa sasa. Hata hivyo, anakiri kuwa hana elimu yoyote juu ya athari za kutoa figo au jinsi ya kuishi baada ya kutoa figo.
“Nimeamua kuuza figo ili nipate pesa za kufanya biashara. Figo yangu naiuza kwa Sh50 milioni tu, bei yangu ni poa kabisa, siyo kama huyu jamaa,” anasema Bangili huku akionyesha makala ya Chimulimuli ambayo ilimbadili mawazo.
Bangili mwenye umri wa miaka 45 anasema amekuwa akiishi kwa kuombaomba miaka yote, jambo linalowakera watu na yeye pia. Anaeleza kuwa amejaribu kutafuta kazi maeneo mbalimbali lakini amekosa.
Anabainisha kuwa akipata fedha hizo ataanzisha mradi wa kilimo cha mbogamboga na ufugaji wa nyuki. Anaamini kuwa ana uwezo wa kuendesha shughuli hiyo na kujiongezea kipato zaidi ndani ya muda mfupi.
“Yaani nikipata hiyo hela nitanunua shamba la ekari tano huko Bagamoyo au Tegeta, nitaanzisha kilimo cha mbogamboga na kufuga nyuki. Baada ya miaka mitatu mbona nitakuwa bilionea!” anasema huku akicheka.
Kijana huyo anayeishi Sinza, Dar es Salaam anaonekana kudhoofu mwili akisema hiyo inatokana na kula mlo mmoja na wakati mwingine kutokula kabisa. Anasema mbali na kuwa ndugu zake hawana uwezo, pia wamemchoka kwa sababu wamemsaidia kwa muda mrefu.
Bangili anatoka kwenye familia ya watoto wanne, akiwa ndiye mkubwa. Anasema wadogo zake wengine wana maisha yao na wanajimudu kwa kipato kidogo wanachokipata.
Mara nyingi amekuwa akipokea msaada kutoka kwa waumini wa Kanisa la Waadventisti wa Sabato, lakini anasema sasa amechoka kuombaomba, anahitaji kuwa na kazi ya kumuingizia kipato.
“Nataka nikipata pesa nioe, umri nao umekwenda. Nashindwa kuoa kwa sababu sina pesa za kumtunza mwanamke,” anasema Bangili ambaye ana elimu ya kidato cha nne.
“Nimekata tamaa kabisa ya kuishi, nyumba ninayoishi nililipiwa kodi na rafiki yangu niliyesoma naye Shule ya Sekondari Kinondoni Muslim. Wazazi wangu walifariki muda mrefu, nilitaka kuuza nyumba ili nipate mtaji, shangazi akanikataza.”
Mkurugenzi wa Taaasisi ya Figo nchini, Jaji Frederick Werema aliwahi kukaririwa na gazeti hili akishangaa kuona baadhi ya watu wakiuza figo zao, jambo ambalo alisema ni kinyume cha sheria.
“Kuuza figo ni kosa la jinai, lakini siyo hivyo tu, kutoa figo lazima ufuate taratbu za kisheria na za kitabibu,” alisema Jaji Werema miezi kadhaa iliyopita.
Athari za kutoa figo
Taasisi ya Utafiti wa Figo ya Uingereza inabainisha kuwa mtu anayeishi na figo moja anaweza kuishi kama wengine endapo atalinda mwili wake dhidi ya nguvu ya msukumo wa damu. Inashauriwa mtu huyo asishiriki kwenye michezo kama vile mpira, mieleka, ndondi au mchezo wa kuteleza kwenye barafu ili kujiepusha na hatari ya kudhurika.
Taasisi hiyo inaeleza katika jarida lake la mtandaoni kuwa watu wengine huzaliwa wakiwa na figo moja na wengine hutoa ili kuwasaidia wapendwa wao ambao figo zao zote hazifanyi kazi.
Jarida hilo linafafanua kuwa baadhi ya watu wanapata matatizo baada ya kutoa figo zao ikiwa ni pamoja na shinikizo la damu. Hata hivyo, athari hizo zinaelezwa kujitokeza muda mrefu baadaye.
Jarida hilo linasisitiza uangalizi wa karibu kwa watoto waliotolewa figo moja likisema athari wanazoweza kupata ni kuongezeka kwa protini nyingi kwenye mkojo, pia figo zao kushindwa kufanya kazi wanapofikia umri wa utu uzima.
Jarida jingine la kuchangisha figo ili kuokoa maisha ya watu wenye matatizo (Give a Kidney) la Uingereza, linabainisha hatua kadhaa za kufuata kabla figo haijatolewa na mtindo wa maisha ya kuishi baada ya kuondolewa kwa figo moja.
Linaeleza kuwa kabla ya kutolewa figo, mhusika anachukuliwa vipimo vingi ikiwamo afya ya mwili na akili. Vipimo hivyo hulenga kuchunguza kama mtoa figo yupo kwenye hali nzuri kiafya kwa kuwa na uzito unaohitajika, pia kutokuwa katika msongo wa mawazo. Mtoa figo anapewa msaada ya kisaikolojia ili aishi vyema baada ya kutoa figo. Jarida hilo linaeleza kuwa wengi wanaotoa figo huathirika kisaikolojia kwa hofu ya kifo.
Vipimo vingine ni mkojo pamoja na damu. Vipimo hivyo huchunguza kama mtoa figo ana maambukizi mengine ya magonjwa, kiwango cha protini kwenye mkojo na kundi la damu la mtoa figo.
Kadhalika, mtoa figo anapigwa picha ya X-Ray kuchunguzwa kama mapafu na moyo wake viko katika hali nzuri. Pia, anachunguzwa kama figo zake zote ziko sawa. Baadhi ya watu huzaliwa wakiwa na figo moja, pengine bila wao wenyewe kujua.
Jarida hilo linabainisha kuwa mtu mwenye figo moja au mbili ambazo hazifanyi kazi vizuri, hana sifa ya kuchangia figo. Pamoja na vipimo vingine, mtu anaruhusiwa kutoa figo yake baada ya daktari kujiridhisha kuwa atakuwa salama.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!