Friday 20 February 2015

IDADI YA WANAOKEKETWA SINGIDA INATISHA

Takwimu zilizotolewa na Hospitali ya mkoa wa Singida kuwa asilimia 20.3 ya wanawake wanaojifungulia katika hospitali za mkoa huo wamekeketwa, zinabainisha tatizo hilo bado ni kubwa na mikakati zaidi yahitajika ili kukabiiana nalo hata kulitokomeza kabisa.

Hali hiyo huhatarisha maisha ya wanawake na watoto wakati wa kujifungua kwa sababu ya uwezakano mkubwa wa kupasuka kwa kushindwa kutanuka na kusababisha damu nyingi kuvuja.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake mkoani Singida, Suleiman Muttani,  akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, kwenye kongamano la kitaifa la Kupiga vita Ukeketaji wa Wanawake lililofanyika mkoani hapa, alisema wanawake wamekuwa wakifanyiwa ukeketaji  kwa viwango mbalimbali ikiwemo kukata na kunyofoa sehemu za siri za  wanawake.
"Baadhi wanakatwa sehemu zote, kufungwa mashavu ili njia iwe ndogo kwa kile kinachosemwa kwa ajili ya kuwafanya wanaume wapate starehe za kimwili wanapokutana nao," alifafanua.
Utekelezaji wa kufanikisha ukeketaji, Dk. Muttani alisema kuwa,  huwashirikisha  watu zaidi ya wanne au watano hivi, ambao humkamata msichana au mwanamke kwa nguvu  wakati ngariba  akitumia vitu vyenye ncha kali kukeketa sehemu za siri za mwanamke na zoezi hilo hukamilishwa kati ya dakika 10 hadi 20 na kumuacha muathirika akivuja damu nyingi hata kuhatarisha maisha yake.
" Baada ya zoezi hilo waathirika hupakwa mavi ya ng'ombe, magadi na vitu vingine ambavyo huhatarisha maisha ya wahusika ikiwemo kupoteza damu nyingi hata kusababisha vifo," aliliambia kongamano hilo lilioandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na kuwashirikisha wadau toka mikoa inayoongoza kuathiriwa na tatizo hilo ikiwemo Mara, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Singida na Dodoma.
Alivitaja vifaa vinavyotumika kufanya ukeketaji huo kuwa ni vipande vya chupa, visu, viwembe na  mawe yenye ncha kali ambavyo vyote vinaweza kuwa ni njia ya kueneza maambukizi ikiwemo UTI na Ukimwi, kwa sababu hutumiwa kwa watu wengi ambao hali zao za kiafya hazijulikani, ikiwa pamoja na watekelezaji wa zoezi hilo
Dk. Muttani alisema kuwa, ukeketaji hutekelezwa kwa wasichana na wanawake wote kuanzia watoto wadogo wanapozaliwa wakiwa na umri wa miaka 4 - 10, wakati wa balehe, wakati wa mimba hata wakati wa kujifungua wakunga wa jadi huifanya kazi hiyo.
Aliitaka jamii kubadilika na kuacha ukeketaji ili kuwanusuru wasichana na watoto wasipate madhira hayo mabaya kiafya..
Taarifa ya Shirika la Afya Duniania (WHO) inabainisha kuwa wanawake ambao wamefanyiwa ukeketaji wapo katika hatari kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi, pia kuna ongezeko kubwa la asilimia 31 la kujifungua kwa njia ya operesheni pia takriban asilimia 55 ya wazazi katika kundi hilo wapo katika hatihati ya kupoteza watoto wao wakati au mara tu baada ya kujifungua.Hali hiyo ni mzigo kwa sekta ya afya ambayo ina changamoto nyingi nyingine
Kila mwaka hapa Tanzania, ingawa hakuna takwimu halisi kuonyesha ukubwa wa tatizo hilo, wasichana na wanawake hufariki kwa kutokwa  na damu nyingi ikiwa ni matokeo ya kufanyiwa ukeketaji. Maelfu zaidi huteseka kimyakimya kwa maumivu yasiyovumilika huku watu wengi hawatambui maumivu na vifo hivi vinavyoweza kuzuilika.
Ukeketaji ni kosa kwa mujibu wa sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 (SOSPA).
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA Tanzania), Dk Natalia Kanem katika hotuba yake iliyosomwa na mwakilishi wake Tausi Hassan alisema kuwa inasikitisha kuona nchini Tanzania vitendo vya ukeketaji vinaongezeka kufanyika kwa watoto wenye umri mdogo takriban ongezeko la asilimia 10 la ukeketaji kati ya mwaka 2004 hadi 2010 watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja.
“Ongezeko hilo linatuonyesha kuwa wazazi wanachangia kuongezeka kwa vitendo hivyo kwa watoto wasiokuwa na hatia na wasioweza hata kujitetea dhidi ya ukatili huo. Pia imefahamika kuwa hapa Singida magadi yanatumika sana kufanya ukeketaji,” alisema.
Ukeketaji alisema kuwa, lipo ndani ya mioyo yetu hivyo ni muhimu kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa hakuna mtoto wa kike anayefanyiwa vitendo hivyo vya ukatili mbele ya macho yetu.Kwamba mtoto wa kike asiyekeketwa hawezi kuolewa mapema kwa sababu ataendelea na masomo hadi elimu ya juu na hivyo kushiriki kiuchanhgia kuleta maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Ujumbe wa Kimataifa wa Siku ya Kupinga Ukeketaji mwaka 2015 umewalenga wahudumu wa afya “ Uhamasishaji na ushirikishwaji wa wafanyakazi wa Afya ili kuharakisha kutokomeza ukeketaji”
Katika baadhi ya nchi,ukeketaji unafanywa na wahudumu wa afya, mathalani  msichana mmoja kati ya watano wamekeketwa na watoa huduma waliopatiwa mafunzo na katika nchi nyingine idadi hii inafikia .kati ya wasichana watatu hadi wanne
“Wataalamu wa afya hususan walio katika zahanati na vituo vya afya mara nyingi wanaweza kuwa na shinikizo kubwa la kufanya ukeketaji.Lakini endapo watahamasisha kupinga shinikizo hilo wanaweza kuwa sehemu ya ufumbuzi.”alisema na kuihimiza jamii kuchukua hatua za kupinga na kukomesha ukeketaji.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii na Jinsia na Watoto,Sophia Simba aliyekuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo aliwataka wafanyakazi wote wa sekta ya afya kama wapo wanaojihusisha na vitendo vya ukeketaji kuacha mara moja vinginevyo wakibainika sheria itachukua mkondo wake.
“Waachane na vitendo hivyo na watumie ushawishi walionao katika jamii wanazofanyia kazi na kuhamasisha wenzao katika jamii zingine kukomesha vitendo vya ukeketaji katika maeneo yote.Pia tunatoa wito kwa wafanyakazi wote wa afya kulinda afya ya uzazi na ujinsia ya wasichana wote ambao tayari wamekeketwa,” alisema.
Alisema serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto inafanya jitihada kubwa kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kupitia sera na mikakati mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TAMWA, Valerie Mssoka alisema kuwa chama chake kimekuwa kikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji kwa kuwaimarisha waandishi wa habari kwa mafunzo ili kuwafanya wachunguze, kufanya utafiti na kuandika matukio mbalimbali ya ukatili ili kuifanya jamii ichukue hatua ya kuachana na vitendo hivyo pamoja na kuwaadhibu wahusika hata kuleta mabadiliko ya kuifanya jamii kuwa huru isiyo na ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, John Henjewele akichangia katika kongamano hilo, alilitaka jeshi la Polisi kuchukua tahadhari kubwa wanapowapangia kazi katika dawati la jinsia polisi wanaotoka katika maeneo yanayokumbatia mila za ukeketaji.
"Polisi hao wanapofikishiwa waathirika wamefanyiwa ukeketaji hawachukui hatua yoyote kwa sababu ni waumini wa mila hiyo na wanafanya kila wawezalo ili kuitetea mila hiyo na hivyo kukwamisha juhudi za serikali za kupambana na mila hiyo potofu," alisema.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, SSP Simon Haule, alisema kuwa taarifa za kiintelijensia zimebaini kuwa, baadhi ya mangaliba wanatumia njia za siri zaidi kuwakeketa watoto wangali wachanga kwa kuwafunga kamba au uzi katika sehemu za siri na kuzifanya sehemu hizo zikatike zenyewe taratibu na kwamba njia hizi hutumika zaidi katika kijiji cha Mtinko mkoani hapa.
"Kwa kuwa njia hizi ni siri sana...tunajitahidi kutoa elimu na kutengeneza mtandao kwa njia ya jamii wanapoona hali yoyote kama hiyo, watoe taarifa haraka ili hatua zichukuliwe kwa muathirika apate tiba na watuhumiwa wakamatwe na kufikishwa mahakamani," alisema.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Parseko Kone akifunga kongamano hilo la siku mbili, aliitaka jamii kushirikiana katika kuhakikisha kuwa vitendo vya ukeketaji vinatokomezwa kabisa kwa kubadili tabia na mitazamo badala ya kuendelea kukumbatia mila hiyo ambayo ina madhara makubwa kwa wasichana na wanawake kwa ujumla

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!