Sunday 8 February 2015

ALBINO VIJIJINI HATARINI KUPATA KANSA YA NGOZI



WATU wenye ulemavu wa ngozi (albino) wanaoishi vijijini, wana hatari ya kupata magonjwa ya saratani ya ngozi, kutokana na kutokuwa na elimu ya afya bora na utunzaji wa ngozi.



Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Ngozi mkoani Dodoma, Ludovick Kowo, katika warsha ya mafunzo ya afya bora na utunzaji wa ngozi kwa albino wilayani Kongwa.
Alisema kutokana na ukosefu wa elimu ya utunzaji wa afya ya ngozi kwa walemavu waishio vijijini, walemavu hao wana hatari kubwa ya kupatwa na saratani ya ngozi na kuongeza kuwa ukosefu huo wa elimu, unatokana na umasikini.
Pia alisema walemavu walio wengi, hawana elimu ya kutosha ya utunzaji wa afya zao, hali inayochangiwa na ukosefu wa kipato cha kuwasaidia katika kujikwamua na hali ngumu na ununuzi wa dawa hizo.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Kufadhili Asasi za Kiraia (FCS), Kowo alisema Sh milioni 45 zimetolewa kwa ajili ya utoaji wa elimu ya afya bora na utunzaji wa ngozi.
Alisema ufadhili huo utaziwezesha wilaya mbili ikiwemo ya Kongwa na Mpwapwa na kata 12 kupata elimu itakayowasaidia kuepukana na magonjwa hayo, ambayo yamekuwa tishio na kusababisha vifo.
Mwenyekiti huyo amezitaka taasisi na mashirika na serikali, kuwezesha walemavu kwa kuwapa mitaji, itakayowawezesha kuunda vikundi vya ujasiriamali ili waondokane na hali ngumu ya maisha.
Alilitaka shirika hilo kutoa kipaumbele katika utoaji wa elimu ya afya, kwa kuangaliza zaidi walemavu wanaoishi vijijini, ambako wana changamoto nyingi za maisha kuhusu namna ya kukabiliana na utunzaji bora wa afya zao.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!