Monday, 26 January 2015

PELEKENI WATOTO WA KIKE SHULE-MWINYI



RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ameitaka jamii ya kifugaji na waokota matunda kote nchini, kufanya mapinduzi makubwa ya elimu kwa mtoto wa kike wa jamii hiyo na kuondokana na mila potofu za kuwazuia watoto hao kwenda shule.



Mbali ya hilo, aliwaonya wazazi wa watoto hao, kuacha tabia ya kuwazuia watoto wao kwenda shule na kuwalazimsiha kuolewa, hatua ambayo alisema inamsikitisha na kumhuzunisha. Alisema kuwa tabia hiyo inapaswa kukomeshwa kwa karne hii.
Mwinyi alisema hayo juzi katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 20 ya shule ya wasichana ya jamii ya kifugaji na waokota matunda ya Maasai wilayani Monduli mkoani Arusha, iliyo chini ya Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati.
Alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania, kufanya kila linalowezekana kuelimisha na kuhimiza wafugaji na waokota matunda kupeleka watoto shule na kuondoka na mila potofu za kuwaozesha watoto hao na jukumu hilo lisiachiwe serikali pekee yake.
Mwinyi alisema iwapo kila Mtanzania atawajibika kwa hilo na kwa nguvu kubwa, ana uhakika mapinduzi makubwa ya elimu yatakuwepo kwa jamii hiyo na kizazi kijacho mila hizo zitakuwa historia na kujenga watoto wa kike wenye uwezo mkubwa.
Alisema Mei 27 mwaka 1995, alipokwenda katika shule ya Maasae kuifungua, ilikuwa na darasa moja, lakini kwa sasa amekuta msitu wa majengo makubwa ya madarasa, mabweni, nyumba za walimu na maabara. Mwinyi alisifu na kushukuru wale wote waliofanikisha uendelezaji wa shule hiyo.
Alisema kuwa wanapaswa kutiwa moyo wa kujitolea na kuwaomba kuendelea na moyo huo bila ya kurudi nyuma. Alisema kutokana na hali hiyo, ana uhakika kuwa kuna matumaini makubwa kuwa Taifa litafika malengo yaliyokusudia ya kupiga vita umaskini na ujinga kwa jamii zote.
Mwinyi alisema kiwango kilichopo sasa cha watoto wa kike 1,200 waliopo katika shule hiyo, tofauti na awali ni kiwango kinachoridhisha.
Lakini, alitaka idadi hiyo kuongezeka zaidi ili mapinduzi ya elimu kwa jamii hiyo yaweze kwenda kwa kasi ya hali ya juu, tofauti na miaka ya nyuma.
Aliwashukuru wahisani walioanzisha mapinduzi hayo na kushukuru wale wote wanayoendeleza mapinduzi hayo, kwani wanapaswa kuungwa mkono kwa asilimia kubwa bila ya kusita kwa maslahi ya vizazi vijavyo.
“Tunataka tufanye mapinduzi makubwa ya elimu kwa mtoto wa kike wa kifugaji na waokota matunda na tupige vita wazazi wa jamii hiyo wanaokataza mabinti zao kwenda shule na kuwalazimisha kuolewa kwani wanaturudisha nyumam,” alisema.
“Hii karne sio ya mtoto wa kike kuacha kwenda shule, ni aibu kubwa, hii shule tuitumie vizuri, nilikuja nilikuta sifuri sasa nimekuta msitu wa majengo, pongezi sana kwa wale waliofanikisha hili,’’ alisema.
Alisifu uongozi wa KKKT kwa kujenga umoja huo katika shule hiyo na kutaka kuendeleza hilo kwa maslahi ya nchi.
Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa alimpongeza Rais mstaafu, Mwinyi, kuwa ni kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele kuendeleza elimu katika kipindi cha uongozi wake, hivyo anapaswa kupongezwa na kila mkazi wa wilaya ya Monduli.
Lowassa alisema katika uongozi wake, aliwahi kutoa Sh milioni 40 na kutoa ardhi ya ekari 700 kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu, hivyo jitihada hizo zinapaswa kukumbukwa na kupongezwa kwa asilimia kubwa.
Alisema katika kumwomba kuja katika jubilee ya miaka 20 ya shule hii, hakusita na kuungana na wakazi wa Monduli katika kusherehekea maadhimisho hayo kwa pamoja.
Lowassa alisifu uongozi wa KKKT chini ya Askofu Solomoni Masangwa kwa kutoa kila taarifa ya misaada wanayopewa, kwani huo ndio ustarabu kwa kutolea maelezo kile unachopewa ili kumshawishi anayekupa kuwa na imani na wewe hivyo aliwataka kuendelea na moyo huo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda alisema serikali imefurahishwa na jitihda za KKKT katika kuendeleza elimu mkoani Arusha na kulitaka kanisa hilo kuendelea na moyo huo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!