Tuesday 27 January 2015

Nimesomesha mke, kapata kazi sasa ananitesa ile mbaya!


Mpenzi msomaji, kama nilivyosema katika makala iliyopita na zinginezo, kinababa wengi wananyanyaswa sana na wake zao, ingawa wenzi wao hawa wamewafanyia mambo mengi mazuri yaliyowajenga na kuwainua katika hali zote (kiafya, kichumi na hata kuheshimika).



Mtu unajiuliza; sasa ni kwanini kinamama hawa wanaoinuliwa na waume au wenzi wao, wengi huishia kuwanyanyasa au kuwakandamiza? Je, huwa ni ufinyu wao wa fikra, wametumwa au wanafanya makusudi?

Baada ya kituko cha wiki iliyopita jamaa kalazimika kuacha kazi alee mtoto eti ili mkewe aende kazini, hebu sikia tena hiki ufungue macho yako mawili utafakari!

Da Flora, hongera sana kwa safu yako ya Maisha Ndivyo Yalivyo. Ni kweli  kabisa kuwa wanawake wengi wanawanyanyasa waume zao. Safu yuko ni uwanja wa wanaume nao kutoa hisia zao maana imezoeleka kuwa wanawake ndiyo hunyanyaswa.

 Ukiendelea na mada hiyo ya wanaume nao waseme utayasikia mengi. Mimi nina kisa cha rafiki yangu alimsomesha binti tangu sekondari hadi chuo kikuu ilhali yeye ni darasa la saba lakini kilichomsibu ni Mungu tu ajuaye. 

Mwanamke aliamua kumwacha na kwenda kuolewa na mwanaume mwingine.
Hata mimi anti nina mke nimemsomesha kuanzia certificate hadi Masters lakini cha moto nakipata. Mke hasikiki, jeuri anayonifanyia natamani  kuachana naye, ni kisa kirefu. Leo nilitaka tu kukupongeza kwa safu yako ya Maisha Yalivyo. Hongera sana(usiweke jina wala namba yangu gazetini).

Mpenzi msomaji, kijana huyu alionekana anayo mambo mazito moyoni mwake, hivyo nikamsihi avunje ukimya huo aweze kupata ushauri mzuri. Nilimwahidi kumpigia simu lakini kabla sijafanya hivyo, akaendeleza kwenye ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani yafuatayo;-

Asante anti Flora, kisa changu ni kirefu sana. Itoshe tu kusema nanyanyasika sana! Nimemuoa mke wangu akiwa kamaliza fomu 4. Nimemwendeleza amehitimu shahada ya uzamili (masters), lakini sasa najuta kumsomesha tangu atoke chuo ana vituko vinavyoashiria anataka talaka. Hana msaada wowote hapa nyumbani hachangii chochote licha ya kuwa na mshahara mkubwa kuliko mimi.

Pale tunakoishi tumepanga, alipokuwa chuo nilijitahidi nikaweka msingi kwenye site yetu nikitaraji akirudi tutaunganisha nguvu  tuanze kunyanyua ujenzi. Nilipomwambia akajibu yeye ana jukumu la kumalizia nyumba ya mama yake na kumsomesha mdogo  wake.

Aidha, amekuwa hachangii chochote hata chumvi hanunui. Majukumu yote yako kwangu ada za shule, chakula, kodi ya nyumba, umeme, maji, pesa ya nauli na matumizi ya watoto yote ni mimi. 

Kwa kweli nakonda kwa mawazo kwani bado nampenda mke wangu na suala la kumuacha linaniuma sana kwani niliwekeza kwake nikitarajia tutaishi vizuri na pia nawahurumia wanangu naona watateseka na bado ni wadogo. nifanyeje?”, ndivyo anavyomalizia ujumbe wake msomaji wetu huyu.

Lakini muda mfupi baadaye msomaji huyu akaleta ujumbe mwingine uliosomeka namna hii; Asante kwa kujali SMS zangu Mungu akubariki. Stori yangu ni ndefu yaweza kukutoa machozi. 

Kama sasa (muda huu niandikapo ujumbe huu) nimetoka kazini mke hajafika ukimpigia simu hapokei hata kama watoto wanasema baba mpigie mama nimsalimie, amefikia hatua ya kurudi nyumbani saa 4:30 usiku akidai alikuwa kwenye chama. Hivi kweli ant Flora vyama vyenu wanawake vinawafanya msahau majukumu yenu ya nyumbani? Hata kama hampiki?”. Anamalizia ujumbe wake.

Mpenzi msomaji, maelezo ya jamaa huyu yalivinuta nikakuta nampigia simu. Nilimpa ushauri mmoja muhimu kwa kuanzia ambao naye kumbe alishaufikiria na kuanza kuufanyia kazi. Kuitisha kikao cha ndugu pande zote mbili wazungumze.

Inaonekana dhahiri kuwa jamaa anampenda sana mkewe na nia ya kuishi naye maisha anayo. 

Lakini mke huyu hayuko huko kabisa na hasa baada ya kuona kasomeshwa, kashazaa watoto wake na anachokiona ni kutafuta maisha huru yasiyobughudhiwa na mume.

Katika mazungumzo nilitaka nijue chanzo cha mke huyu kumfanyia visa mume aliyempenda hata kumuinua kielimu, sehemu kubwa zikiwa ni gharama zake(mume). Nilimuuliza kama anaijua vyema familia ya mkewe hasa baada ya kuniambia kuwa bibie amejishikamanisha sana na mamake na ndiye mshauri wake mkuu.

Lakini kijana huyu ananiambia kuwa mama yake binti baada ya kufiwa na mume wa kwanza, alishaishi na wanaume watatu katika nyakazi tofauti na wote alizaa nao watoto kisha kuachana. 

Hapa nikagundua kuwa ipo roho ya mitala(waume/wake wengi) inamshikilia mamake huyu ambayo ni rahisi pia kuathiri watoto wake.

Na binti huyu aliyemuegemea mamake badala ya mume, inaonekana dhahiri kuwa hiyo roho imeshamvaa na siyo ajabu anafanya visa ili aachwe lakini asipokuwa makini hata akiolewa na mwanaume mwingine, hatadumu naye kama ilivyotokea kwa mama yake. Maombi pekee ndiyo yanaweza kuivunja roho hii ya mitala ambayo hurithi kizazi hadi kizazi isipovunjwa.

Mbali na hili nilimshauri kijana aitishe kikao cha wanafamilia pande zote mbili kwa ajili ya usuluhishi kusikia malalamiko ya pande zote. Hata hivyo, akaniambia tayari amemjulisha mjomba wa binti ambaye ni kiongozi mkubwa katika dini ambaye ataitisha kikao hicho kupata ufumbuzi. Hakika Maisha Ndivyo Yalivyo.


NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!