WATU 200 wakiwemo watoto 12 wameambukizwa virusi vinavyosababisha Ukimwi baada ya kutibiwa na muuguzi asiyekuwa na leseni nchini Cambodia.
Muuguzi Yem Chrin, anayedaiwa kusababisha athari hiyo kwa miaka 20 kwa wakazi wa kijiji cha Roka ambacho ni maarufu kwa kilimo cha mpunga, amekamatwa na polisi na kukiri kutumia sindano moja na kiwembe kimoja kwa wagonjwa wengi, hali iliyosababisha wagonjwa wengi kuambukizwa virusi hivyo.
Miongoni mwa waathirika hao ni watu 16 kutoka familia moja, pamoja na kiongozi wa dini ya Budha mwenye miaka 82. Chrin mwenye taaluma ya uuguzi, amekuwa akiwatibu watu katika Kambi ya Wakimbizi baada ya kuanguka kwa utawala wa Khmer Rouge, ambao uliua takriban watu milioni mbili na sasa anashikiliwa karibu na Battambang.
Kutokana na kusababisha watu wengi kupata virusi vya Ukimwi, sasa anashitakiwa kwa kosa la mauaji kwa kukusudia baada ya kusambaza virusi vya Ukimwi na kufanya kazi bila kuwa na leseni.
Siri hiyo ilibainika Agosti mwaka jana, baada ya mjamzito mmoja kugundulika ameathirika virusi vya Ukimwi, ambapo wafanyakazi wa hospitalini hapo walishindwa kuelezea namna mjamzito huyo alivyoambukizwa.
Wiki chache baadaye, mjamzito mwingine akagundulika kuwa na virusi vya Ukimwi hatua iliyosababisha Serikali kuingilia kati na kuagiza wanakijiji wote wapime virusi vya Ukimwi.
Hata Waziri Mkuu alikataa kuamini kuwa wajawazito hao walikuwa kielelezo sahihi cha kuwepo kwa hali isiyo ya kawaida ya maambukizi hayo na kusema anaamini watu hao hawajaathirika kwa virusi vya Ukimwi.
Lakini baadaye watu walizidi kupima na wengi wakaonekana kuathirika na kufanya vituo vya afya kugubikwa kwa vilio huku wengine wakikumbatiana. Bibi Chem Mao (55), ni miongoni mwa waliochanganyikiwa kukutwa na virusi vya Ukimwi na kujikuta akitaka kujiua lakini wajukuu zake walimzuia asichukue hatua hiyo.
Hata hivyo Chhay Yao (76) ambaye watu 16 kwenye familia yake wameathirika na virusi hivyo vya Ukimwi, anapinga muuguzi huyo kuwaambukiza wakazi wa kijiji hicho kwa makusudi. “Siamini kama yeye ndiye sababu ya watu kupata virusi vya Ukimwi, ni mtu safi na si mtu mbaya kama wanavyodhani serikali.
Tukiwa na fedha huwa tunampa ili atutibu lakini tukikosa anatuambia tumlipe baadaye,” anasema. Kwa mujibu wa mtoto wa muuguzi huyo, Chrin Reaksa, baba yake alihamia kwenye kijiji hicho ili aishi kwenye kambi ya wakimbizi lakini wanakijiji walimfuata ili awasaidie.
Baada ya muda, alianzisha kituo cha afya na kutoa tiba na wanakijiji walimfuata na wamekuwa wakisema wakati wote amekuwa mwepesi kuwasaidia.
Anasema kabla ya tukio hilo la watu wengi kuathirika, maofisa wa serikali hawakuwahi kumuuliza leseni yake na walikuwa wakitambua kazi anayoifanya.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment