Monday 26 January 2015

MLEMAVU WA NGOZI AFICHWANDANI MIAKA 13 KUKWEPA WAUAJI


“Wazazi angu waliwahi kunificha kwa kufungiwa ndani bila kutoka nje kwa takribani kipindi cha nusu mwaka …hawakuwa na lengo baya…dhumuni lao kubwa lilikuwa ni kunihifadhi nisitekwe na wale wauaji wa maalbino…mama alikuwa ananiambia Shigela mwanangu, usije ukatoka nje unaweza kutekwa na kuuawa,” anaanza kueleza Shigela Lyaki (13) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino) anayeishi Mkoani Simiyu.



Lyaki ni mzaliwa wa kijiji cha Nyanguge , kata ya Ngulyati Mkoani Simiyu anasema, mtu anaweza asiamini kile kilichomtokea ila hiyo ndio hali halisi ya maisha yake.

 Amepitia katika kipindi kigumu maishani Haikuwa kazi rahisi kupata fursa ya kuzungumza na Shigela na wazazi wake hadi kuelewana kwa sababu hawajui kuzungumza lugha ya Kiswahili isipokuwa kisukuma tu.

Pia Iliniwia vigumu sana kupata kile nilichokitaka hadi nilipomtafuta mkalimani wa kunitafsiria kile walichokuwa wakinieleza hasa mtoto Shigela niliyemkusudia.

Shigela anafafanua kwa Kisukuma kisha kutafsiriwa kuwa “ elikanza lingi nakabhonaga  Nsoni (minala) ya kwisyumbya nulu kwigusha hamo na bichane kunguno ya bombilimilu bone ubho nabyalwa nabho na makanza gangi bhakanimelaga nachene niigwa kibyi (sagala)”
Akimaanisha kwa lugha ya Kiswahili kuwa “Shigela anasema wakati mwingine anaona hata aibu kujichanganya ama kucheza na wenzake kutokana na ulemavu aliozaliwa nao, kwani mara nyingi wanamtania na huwa anajisikia vibaya sana.

Alieleza amekuwa akilindwa na mama yake kama dhahabu kwa hofu ya kukatishwa maisha yake kutokana na mazingira aliyonayo.Anasema hadi kufikia umri alionao, hana furaha hata kidogo na tayari amepoteza matumaini katika maisha yake kwa sababu hajapelekwa shule kutokana na hofu kubwa ya kutekwa.

Shigela anasema, elimu ndio kila kitu kwake, kwani ni mkombozi wa wanyonge, ingawa hadi sasa mkombozi mwenyewe hajampata na hajui cha kufanya ili aweze kuipata elimu sawa na watoto wenzake ambao hawana ulemavu kama wake.

“Kitu ambacho ningeweza kujivunia katika maisha yangu ni elimu ambayo ingekuwa ni mkombozi wa maisha yangu kwa mimi ambaye ni melmavu wa ngozi (albino)…Lakini nitaipataje elimu huku maisha yetu ni ya shida na yako mashakani kutokana na kuishi kwa hofu ?”alihoji Shigela.

Mama mzazi wa Shigela aitwaye Malga Luganganya (38) Mkazi wa Kijiji cha Nyanguge anaeleza kuwa, anajisikia vibaya sana na wakati mwingine hujifungia ndani na kulia kutokana na hofu aliyokuwa nayo ya jinsi ya kumlinda mwanawe asije akakutana na balaa la kutetwa.

“Wakati mwingine mimi mzazi nimuonapo mwanangu na hali aliyonayo ya ulemavu naumia sana …lakini sina jinsi kwani ni mipango ya Mwenyezi Mungu…Hebu angalia sasa mwanangu hadi sasa ana umri wa miaka 13 hajaanza shule nami nahofia usalama wake akiwa shuleni “ alisema Malga.Mama huyo muda wote alionekana kuwa na huzuni huku akisita kuzungumzia suala hilo.

Anasema ilifikia wakati walikuwa wakisikia utekaji wa maalbino umeshamiri , yeye na mume wake ambaye sasa ni marehemu waliamua kumfungia Shigela ndani kwa muda wa nusu mwaka wakihofu kutekwa na kuuawa kwa mwanawe.
Anasema hali hiyo, ilizidi kumjengea hofu kubwa kuhusu usalama wa mwanawe na kumsababishia hata asitoke nyumbani kwenda kutafuta riziki ili aweze kupata muda wa kumuangalia mwanawe vizuri.

Mama huyo anaeleza kuwa, taarifa za mauaji ya albino ambayo yalivuma kati ya mwaka 2009/2010 ndiyo yaliyomjengea hofu kubwa na kumlazimisha amfungie mwanae ndani kwa kipindi cha nusu mwaka

“Imefikia wakati sasa mimi mwenyewe sitoki kwenda kokote hata kusalimia ndugu na endapo nikitoka,ninakuwa na hofu kubwa huku nyuma wanaweza kumchukua…naishi kwa hofu kubwa mno ukizingatia kijijini kwetu kumepakana na barabara kubwa iendayo jijini Mwanza,” anafafanua.

Kuhusiana na suala la shule, mama Shigela anasema kuwa, kumpeleka shule mwanawe sio kama hataki bali ni kutokana na umbali ulioko kutoka anakoishi hadi shuleni , sambamba na hali duni aliyonayo .

Tangu nifiwe na mume wangu mwaka jana aliniachia watoto wanane, maisha yangu yamekuwa ya tabu sana, kwani hata wakati mwingine wanakosa kabisa chakula … na ndio maana hata kumpeleka Shigela shule sina uwezo kabisa,” alisema
Luganganya anaendelea kueleza kuwa, mwanawe ni mtoto mchapa kazi sana, anayejituma , na anayetamani kusoma na mara nyingi huwa anamsumbua ampeleke shule kama watoto wengine wa jirani na kwao.

Anaendelea kusema kuwa, mwanae Shigela kama angepata bahati ya kupelekwa shule anaonekana kupenda shule na kuwa angesoma kwa bidii na kuja kuwa na kazi yake baadae ambayo ingesaidia familia.

Mbali na hayo, Shigela anadai kusomeshwa ,kupatiwa nguo ikiwa ni sambamba na kupatiwa chakula kwani hivyo vyote ni vigumu kuvipata kama ilivyo kwa familia nyingine.

Mama  anasema mbali na hofu kubwa aliyonayo juu ya kijana wake , Shigela huwa anapenda sana kulima shamba lililoko nje ya nyumba yao ili kujipatia chakula, kwani huwa hapendi kushinda na njaa

“ Hakuna kitu ambacho kinamnyong’onyesha mwanangu kama kukosa chakula…inafikia wakati akikosa chakula na endapo tukilala bila kula anashinda akilia na kulima kwa bidii ilimradi ajipatie mazao,” alifafanua.

Nae Emanuel Lyaki (32) ambae ni kaka wa mtoto huyo kwa mama mwingine, anasema kuwa mama yake anakuwa na hofu kubwa sana ya kumuachia mwanawe na ndio maana anashinda nyumbani akimlinda.

“Na mimi huwa nakaa roho mkononi kwa kuhofia usalama wa ndugu yangu…na endapo itatokea siku akapotea au kutekwa …mama yangu mdogo hatanielewa …na hadi sasa nipo njia panda sijui cha kumsaidia ndugu yangu kwani mama hataki kumuachia,”Alisema.

Juma John(36) jirani wa familia ya Shigela anasema waliwahi kumshauri mama yake Shigela ampeleka shule ,lakini alionekana kuwa mkali hata kuwakasirikia majirani zake.

Kimsingi anaiomba serikali imuangalie kwa macho ya huruma mtoto huyo, ili aweze kupata hifadhi itakayoambatana na kupatiwa elimu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Nyanguge, Kija Kitanda anasema kuwa, wao kama serikali ya kijiji wanayo taarifa ya huyo mtoto pia kama kamati ya kijiji ilishindwa kumshawishi mama yake mtoto aliyekuwa hamuamini mtu yoyote juu ya mwanawe.

Kitanda anaeleza kuwa, ni miaka miwili sasa walishatoa taarifa kwenye uongozi wa kata, lakini cha kushangaza hadi sasa hakuna suluhisho lolote lile la kumsaidia mtoto Shigela.

Anasema kuwa “ katika kijiji hiki hakuna ulinzi shirikishi hivyo ni hatari sana kwa Shigela kutokana na mazingira anayoishi…hata nyumba anayoishi nayo haina ulinzi.

“ alisema.Kitanda Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alionyesha wasiwasi wake juu ya usalama wa mtoto Shigela, hasa kwa kipindi hichi tunachoelekea katika uchaguzi mkuu mwakani.“nina wasiwasi sana na usalama wa huyu kijana…maana tunaelekea kipindi cha uchaguzi mkuu ambacho ndicho matukio kama hayo hujitokeza sana,”.

Ameiomba serikali imsaidie haraka iwezekanavyo ili kumlinda na kumnusuru Shigela, kwani yupo kwenye hatari kubwa sana inaweza kusitisha au kukatisha maisha yake.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Erasto Sima, alipouliza juu ya mtoto huyo alionekana kushangaa kwamba hakuwa na taarifa yoyote ile ingawa aliahidi kwenda kumtembelea na kuangalia uwezekanavyo.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

aziz bilal02:04


1


Loo inasikitisha sana na inatisha kuona mtoto anakutana na haya mambo,hata mimi kinyantuzu kimenitoa nje sikukielewa kabisa .

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!