Tuesday 27 January 2015

MENGI AWATAKA MATAJIRI KUSAIDIA WALEMAVU


Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ametoa wito kwa matajiri nchini kutumia sehemu ya utajiri wao kuwasaidia watu wenye ulemavu.
 
Alitoa wito huo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya chakula cha mchana alichowaandalia watu wenye ulemavu ikiwa ni sehemu yake ya kuwasadia watu wa kundi hilo kila mwaka.
 
Dk. Mengi, aliwasihi Watanzania matajiri kukumbuka kwamba utajiri walionao unatoka nchini, hivyo watumnie sehemu ya utajiri wao kuwasaidia watu wenye ulemavu.
 
“Wafanyabiashara wajitahidi kupeleka sehemu ya faida zao kwa wenye uhitaji. Kuna vitu vichache ambavyo nataka kuwakumbusha wenzangu. 
 
Kwa mfano, mimi ni mfanyabiashara wa soda…..sehemu ya faida ya mauzo ya soda inatokana na huyo mtu mwenye ulemavu….ifike mahali mfanyabiashara aseme ‘nitafute njia ya kumrudishia mtu mwenye ulemavu,” alisema.
 
Katika jitihada zake za kuendelea kuwawezesha watu wenye ulemavu, Dk. Mengi alitangaza shindano la kubuni wazo la biashara huku kila mmoja miongoni mwa washindi kumi watakuwa wakizawadiwa Sh. milioni 10 kwa ajili ya kuwasaidia kuinua hali zao kiuchumi.
 
Pia, aliwataka Watanzania kuendelea kuombea amani kwani vitendo vya uvunjifu wa amani vinapotokea, wanaoathirika wakubwa ni kundi la watu wenye ulemavu.
 
Naye  mjumbe wa bodi ya Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Abdallah Omari, alisema watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto kubwa ikiwamo ya kuendelea kuongozeka idadi ambayo hadi sasa inafikia takribani milioni 7.5.
 
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi likiwamo tukio la hivi karibuni la kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa msichana mkazi wa Wilaya ya Kwimba, Mwanza.
 
Changamoto nyingine ni  pamoja na kukosa uwezo wa kujiendeleza kielimu kutokana na kukosekana kwa mtaji.
 
Alimpongeza Dk. Mengi kwa kuyasaidia makundi ya watu wenye ulemavu ikiwamo kuanzishwa kwa  vikundi vya Vicoba na kwamba vikundi saba tayari vimewezeshwa.
 
“Dk. Mengi ni mmoja wetu katika harakati zetu. Katika nyakati tofauti, amekuwa akifikiria jinsi ya kuwakomboa watu wenye ulemavu. Kwa mfano ameanzisha vitu mbalimbali kusaidia walemavu….Tumeanzisha vikundi 48 vya Vicoba,” alisema.
 
Alipongeza moyo wa Dk. Mengi akisema wapo wengi ambao wana utajiri mwingi,  lakini hawajawahi kujitokeza kufanya hivyo kwani hadi sasa takribani ni miaka 20 amekuwa akiwasaidia.
 
Kwa upande wake, kampuni ya Kamal Group, iliahidi miguu ya bandia 200 wiki hii kwa ajili ya kuwasaisaidia watu walioko kwenye kundi hilo. 
 
Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Sameer Gupta, alisema wataendelea kutoa msaada huo kila mwaka ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia watu wenye ulemavu nchini.
 
Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Chawata) John Mlabu, alishukuru kwa msaada huo huku akiwataka watu wenye ulamavu ambao watapewa miguu hiyo ya bandia, kuitumia kama ilivyokusudiwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!