
Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa 30 ya Tanzania. Mkoa huu upo Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, unapakana na Nchi za Kenya na Uganda kwa upande wa Kaskazini, Mkoa wa Kagera kwa upande wa Magharibi, Mikoa ya Mwanza na Simiyu kwa upande wa kusini na Mkoa wa Arusha kwa upande wa Mashariki. Kijiografia, Mkoa huu upo kati ya Latitudo 10 0’ na 20 31’ kusini mwa Ikweta na kati ya Longitudo 330 10’ na 350 15’ Mashariki mwa mstari wa Greenwich.
Kuitawala Mkoa umegawanyika katika Wilaya 6 ambazo ni Musoma, Bunda, Butiama, Serengeti, Tarime na Rorya. Aidha, Mkoa wa Mara umegawanyika katika Halmashauri 7, Tarafa 20, Kata 154, Vijiji 487 na Mitaa 57.
Historia ya Mkoa wa Mara inaanzia mwaka 1916 wakati huo eneo la kiutawala la sasa la mkoa (North Mara na South Mara) likijulikana kama Wilaya Ndogo ya Musoma (Musoma Sub District), Major J.M. Coote, akiwa Afisa Mfawidhi (officer Incharge) wa Utawala wa Kiingereza kuanzia tarehe 1/1/1917. Ikumbukwe kuwa wakati huo Musoma Sub District (Wilaya Ndogo), ilikuwa ni sehemu ya Wilaya ya Mwanza na hapakuwa na Mikoa. Kufuatia mabadiliko ya kiutawala yaliyofanywa wakati wa utawala wa Mwingereza, Wilaya Ndogo ya Musoma iligawanywa na kuwa Wilaya za North Mara na South Mara zikitenganishwa na mpaka wa asili wa mto Mara. Wakati huo Wilaya hizo zilikiwa sehemu ya Lake Province ikijumuisha Mikoa ya Mwanza, Kagera Shinyanga na Simiyu ya sasa. Baada ya Uhuru, majimbo yote yalibadilishwa kuwa Mikoa, hivyo Lake Province ikawa Lake Region hadi mwaka 1963, ilipoanzishwa Mikoa ya sasa ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Mara na hivi karibuni Simiyu.
Mkoa wa Mara (pamoja na Mikoa ya Kigoma, Mwanza, Moshi na Ruvuma ulianzishwa tarerhe 01/05/1963 kwa maelekezo ya Waraka Na. VPC.9/50/02 wa tarehe 07/03/1963) na kuifanya mikoa kuwa 13 kwa wakati huo. Bw. M.T. Spearing – Afisa Mfawidhi aliteuliwa kukamilisha taratibu (logistics) za kiutawala.Tangu wakati huo Makao Makuu yakawa Musoma mpaka sasa. Mkuu wa Mkoa wa kwanza alikuwa Mhe. Oswald Mang’ombe Marwa kati ya mwaka 1963 hadi 1965. Hadi sasa Mkoa umeongonzwa na Wakuu wa Mikoa 13 akiwemo Mkuu wa Mkoa wa sasa Mhe. John Gabriel Tuppa aliyeanza Septemba 2011. Katibu Tawala wa kwanza wakati huo akijulikana kama “Administrative Secretary – Mara”, alikuwa ni Bw. M.T. Spearing kati ya mwaka 1963-1964. Hivi sasa Mkoa umeongozwa na Makatibu Tawala 19 akiwemo Katibu Tawala aliyestaafu mwaka 2012 Bw.Clement F. Lujaji. Kati ya mwaka 1975 na 2010 zimeanzishwa Wilaya mpya za Serengeti (1974), Bunda (1978), Rorya (2007) na Butiama iliyotangazwa (2010).
Mkoa wa Mara ni chimbuko la Viongozi mashuhuri akiwemo Rais wa Kwanza na Muasisi wa Taifa hili Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye alizaliwa tarehe 13/04/1922 katika kijiji cha Butiama. Alifaliki akiwa katika matibabu kwenye hospitali, London Uingereza, tarehe 14/10/1999 na kuzikwa Mwitongo katika kijiji cha Butiama. Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye muasisi wa Chama cha TANU 1954 – 1977, kilichoongoza harakati za Uhuru. Aidha, Mwalimu alikuwa Muasisi wa Chama Cha Mapinduzi kilichoanzishwa tarehe 05/2/1977 baada ya Vyama vya siasa vya TANU na AFRO SHIRAZI kuungana. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa ni Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Viongonzi wengine wa kitaifa ambao ni wazaliwa wa Mkoa huu ni Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee Timoth Apiyo aliyekuwa Katibu Mkuu wa kwanza Ofisi ya Rais, Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi, Mhe. Wilson Mkama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa sasa Mheshimiwa Amina N. Makilagi, Mheshimiwa Charles Nyirabu Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania, Jaji Fredrick Werema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sasa. Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Waziri wa sasa, Mhe. Stephen M. Wasira Waziri wan chi ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Mhe. Gaudensia Mugosi Kabaka, Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Dkt Makongoro Mahanga, Naibu Waziri Wizara ya Kazi na Ajira kwa sasa. Mawaziri Wastaafu, Mhe. Prof Philimon Sarungi, Waziri, wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Balozi I.M Bhoke Munanka, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mhe.Dkt Wanyancha James Mnanka, Naibu Waziri, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Mhe.Dkt Deogratius Mwita, Naibu Waziri wa Nchi (TAMISEMI).
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wa sasa, Lt.Col.(Mst) Issa Machibya. Wakuu wa Mikoa wastaafu, Joseph W. Butiku, na Balozi Nimrod M. Lugoe. Wakuu wa Majeshi Wastaafu Jenerali David Msuguri, Jenerali Mwita Kyaro na Jenerali Joseph Waitara. Mabalozi Wastaafu, Balozi Joshua Opanga, Balozi James Ndobho na Balozi Alex Mganda.
Eneo la Mkoa ni kilometa za mraba 30,508 sawa na asilimia 3.1 ya eneo la Tanzania Bara. Kati ya eneo hilo lote la Mkoa kilometa za mraba 10,942 ni eneo la maji sawa na asilimia 36 na kilometa za mraba 19,208 sawa na asilimia 64 ni eneo la nchi kavu.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Taifa ya mwaka 1958, eneo la mkoa wa sasa lililokuwa linawakilishwa na Wilaya za North Mara na South Mara lilikuwa na watu 194,939. Sensa zilizofuatia zilionyesha kuwa mwaka 1967 ulikuwa na watu 544,125, mwaka 1978 watu 723,827, mwaka 1988 watu 946,418, mwaka 2002 watu 1,368,602 na mwaka 2012 ni watu 1,743,830. Kwa kufuata sensa hiyo, Mkoa ulikuwa na ongezeko la asilimia 2.5 kwa mwaka.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa wastani wa pato la mkazi kwa mwaka limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka. Mwaka 2000 wastani wa pato la mkazi ilikuwa sh.222.704/=, mwaka 2006 sh.461,860/=, mwaka 2007 sh.494,014/=, mwaka 2009 sh. 600,388/= na mwaka 2012 sh.642,528/=. Kukuwa kwa pato kumetokana na jitihada za makusudi zilizofanyika katika kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Aidha, pamekuwepo na mazingira mazuri yaliyowezesha sekta binafsi kuwekeza katika maeneo mbalimbali kama viwanda, utalii, biashara na uchimbaji madini.
Makabila makuu ya Mkoa Mara ni Wakurya, Wajaluo, na Wajita. Wakurya ni kabila kuu la Wilaya za Tarime na Serengeti ambapo Wajita ni kabila kuu la Wilaya ya Musoma na Bunda. Wajaluo ni kabila kuu la Wilaya ya Rorya. Makabila mengine yaliyopo Mkoani ni Wazanaki, Wangoreme, Wasuba, Waikizu, Waisenye, Waikoma, Wakwaya, Waruri, Washashi, Wanata na Wasweta. Historia inaeleza kuwa wakati wa ukoloni, Wilaya za North Mara na South Mara ambazo ndizo zinaunda Mkoa huu wa sasa, zilikuwa na tawala za machifu (Chiefdoms).
WILAYA YA MUSOMA
Wilaya ya Musoma ni miongoni mwa Wilaya 6 za Mkoa wa Mara. Wilaya hii ilichukuwa jina la mji wa Musoma (Misoma) awali uliokusudiwa kuanzishwa Nyambage (Niavangi) kwa mapendekezo ya Bw. Schulz (Mjerumani) kwa Waraka Kumb. Na.612 wa tarehe 26/09/1911. Wakara huo ulioandikwa na Bw. Schulz wa Wilaya Ndogo ya Musoma (Royal Sub District) kwenda Wilayani Mwanza (The Royal District Office). Ujenzi wa mji ulianza rasmi mwaka 1912, kama ilivyopendekezwa na Bw. Schulz. Kumbukumbu za zinaonesha majina ya Misoma na Niavangi yalitumika kwa jina la mji wa Musoma na eneo la nje ya mji la Nyambage. Chimbuko la jina la Misoma ni neno la Kijita Umusoma likiwa na maana ya rasi (mitchell point) kwa Musoma.
Wilaya hii ilianzishwa wakati wa utawala wa ukoloni wa Mwingereza, ikijulikana kama South Mara, ikiwa ni sehemu ya iliyokuwa Wilaya Ndogo ya Musoma (Musoma Sub District). Kiutawala kiongozi wa Wilaya kwa wakati huo alijulikana kwa cheo cha Afisa Wilaya (District Officer) kwa kuwa cheo cha Mkuu wa Wilaya kilikuwa hakijaanzishwa. Bwana S.B. Jones alikuwa Afisa Wilaya wa kwanza. Mkuu wa Wilaya ya (District Commissioner) wake wa mwisho alikuwa Bwana P.J. Hookins kuanzia tarehe 24/09/1960 hadi alipoteuliwa Bwana Osward Marwa Mang’ombe mwaka 1962 kuwa Mkuu wa Wilaya (Area Commissioner) wa Kwanza Mzalendo. Tarehe 01/05/1963 Bw. Osward Marwa Mang’ombe aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara wa kwanza. Katika mabadiliko yaliyofanywa na Serikali baada ya Uhuru Wilaya ziliundwa upya katika vipindi vya mwaka 1962 na 1963. Tangazo la serikali Na 179 la tarehe 26/4/1963 kuhusu kuundwa kwa Wilaya liliendeleza jina la South Mara ikawa na Tarafa 8 na kata 28 ikijumuisha Tarafa 1 na Kata 6 za Musoma Mjini (Musoma Township Authourity). Kufuatia mabadiliko haya, Bw. A. Msonge aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya (Area Commissioner) kuanzia kipindi cha mwaka 1963 hadi 1965. Bw. J.C. Kiliembe aliteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Halmashauli ya Wilaya (Executive 0fficer) cheo ambacho sasa kinajulikana kama Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya.
Mwaka 1971 vikao vya TANU katika ngazi ya Wilaya na Mkoa vilipendekeza majina mapya ya Wilaya na Halmashauri kuwa:
South Mara iwe Musoma
South Mara District Council iwe Musoma District Council
Mapendekezo yaliidhinishwa na Serikali kwa barua Kumb Na. C/L.40/Vol.IV/50 ya tarehe 08/09/1971
Musoma Township ilitangazwa kwa Tangazo la Serikali Na. 38 la mwaka 1942. Pia ikawa Musoma Township Authourity tarehe 01/02/1960 kwa Tangazo la Serikali Na. 115 la mwaka 1955.
Mabadiliko yaliyofanywa na serikali baada ya Uhuru yaliipa mamlaka hiyo hadhi ya Mji kwa Tangazo la Serikali Na. 222 la tarehe 24/05/1963.
Mwaka 1974 Wilaya iligawanywa kuwa Wilaya mbili za Musoma na Serengeti. Kwa mabadiliko hayo Tarafa za Nansimo, Kenkombyo na Serengeti zilitolewa Wilaya ya Musoma na kwenda Wilaya ya Serengeti hivyo Wilaya ya Musoma ikabaki na Tarafa 4, Kata 27 na Vijiji 106. Mwaka 1978 ilipoanzishwa wilaya ya Bunda, miongoni mwa mabadiliko yaliyofanywa wakati huo ni Kata ya Ngoreme ambayo awali ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Musoma kugeuzwa kuwa tarafa na kuhamishiwa Wilaya ya Serengeti.
Katika mwaka 2012, Wilaya ya Musoma iligawanyika katika Wilaya mbili za Musoma na Butiama. Wilaya ya Musoma ina Mamlaka za moja ya Manispaa ya Musoma na Wilaya ya Butiama ina Halmashauri ya Butiama na Musoma. Manispaa ya Musoma ina Tarafa 1, Kata 13 na Mitaa 57.
Eneo la Wilaya ni kilometa za mraba 630. Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 1958 Wilaya ya Musoma ilikuwa na watu 141,527 (wanaume 65,327 na wanawake 76,200). Sensa zilizofuatia zilionyesha kuwa mwaka 1967 ilikuwa na watu 335,609, mwaka 1978 ilikuwa na watu 263,129, mwaka 1988 ilikuwa na watu 316,632, mwaka 2000 ilikuwa na watu 438,066.
WILAYA YA TARIME
Wilaya ya Tarime ni miongoni mwa Wilaya 6 za Mkoa wa Mara. Wilaya hii ilianzishwa mwaka 1930 wakati wa utawala wa ukoloni wa Mwingereza, ikijulikana kama North Mara, ikiwa ni sehemu ya iliyokuwa Wilaya Ndogo ya Musoma (Musoma Sub District). Kiutawala, kiongozi wa Wilaya kwa wakati huo alijulikana kwa cheo cha Afisa Wilaya Wilaya (District Officer) kwa kwa kuwa cheo cha Mkuu wa Wilaya (District Commissioner) hakikuwepo.
Cheo hicho (District Commissioner) kilianzishwa Septemba 1940. Bw. Anthony Sillery alikuwa Kaimu Afisa Wilaya wa kwanza tarehe 3/1/ 1930. Mkuu wa Wilaya (District Commissioner) wake wa mwishom alikuwa Bw. A. Abel aliyeanza mwaka 1960 hadi alipoteuliwa Bw. Shabani Mohamed tareha 29/03/1962 kuwa Mkuu wa Wilaya (Area Commissioner), akiwa mzalendo wa kwanza Tanganyika kuteuliwa katika wadhifa huo kwa waraka Na. BM/CM/Vol.1/M wa tarehe 03/04/1962 na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali la “Tanganyika Standard” tarehe 30/3/1962. Lameck M. Lima aliteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Halmashauli ya Wilaya (Executive officer) cheo ambacho sasa kinajulikana kama Mkurungenzi Mtendaji wa Wilaya, katika mabadiliko yaliyofanywa na Serikali baada ya Uhuru, Wilaya ziliundwa upya katika vipindi viwili vya mwaka 1962 na 1963. Tangazo la serikali Na. 179 la tarehe 26/4/1963 Wilaya za North Mara na South Mara ziliundwa upya zikiwa na muundo tofauti na ule wa awali ziliongozwa na Area Commissioner badala ya District Commissioner. Pamoja na kuundwa kwa wilaya mpya bado kuliendelezwa jina la North Mara ikiwa Tarafa 8 na Kata 34. Mwaka 1971 vikao vya TANU katika ngazi za Wilaya na Mkoa vilipendekeza majina mapya ya Wilaya kuwa na Halmashauri ya Wilaya kuwa:
North Mara District iwe Tarime District.
North Mara District Council iwe Tarime District Council.
Mapendekezo yaliridhishwa na Serikali kwa barua Kumb. Na. C/L.40/Vol.IV/50 ya tarehe 08/09/1971. Chimbuko la jina Tarime linatokana na jina la Mlima Tarime.
Kiatawala Wilaya ya Tarime iligawanywa katika tarafa za kichifu (chiefdoms) na kata (Subchiefs) kwa kuzingatia mkao wa koo ili kurahisisha shughuli za kiutawala. Kazi hii ilifanywa kati mwaka 1947 na 1957 na Bwana Ingram aliyekuwa Mkuu wa Wilaya wakati wa utawala wa Mwingereza. North Mara District Council ilianzishwa tarehe 01/04/1962 baada ya kuidhinishwa na Bunge ikiwa na Tarafa 8 na Kata 34.
Tarehe 01/07/2007 Wilaya ya Tarime iligawanywa kuwa Wilaya mbili (2) za Tarime na Rorya. Katika mgawanyo huo, tarafa 4 (Nyancha, Girango, Luo Imbo na Suba), kata 21 na Jimbo la chaguzi la Rorya zilikwenda Wilaya mpya ya Rorya. Tarime ikabaki na tarafa 4 (Inchage, Inchugu, Inano na ingwe) na kata 20 pamoja na Jimbo moja (1) la Uchaguzi la Tarime. Mwaka 2007 ilianzishwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Tarime na mwaka 2013 Mamlaka ya Mji Mdogo ya Tarime ilipanda hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji.
Wilaya hii ina kilometa za mraba 1,791.504 kati ya eneo hilo kilometa za mraba 270 ni eneo la hifadhi ya mbuga ya Akiba ya Lamani (Game Reserve). Eneo linalotumika kwa shughuli za kilimo, ufugaji na makazi ya watu ni kilomita za mraba 1,521.504.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 1958, Wilaya ya Tarime wakati huo ilijulikana kama North Mara ilikuwa na watu 145,441. Sensa zilizofuatia zilionyesha kuwa mwaka 1967 ilikuwa na watu 188,536, mwaka 1978 ilikuwa na watu 253,010 mwaka 1988 watu 33,888, mwaka 2002 watu 490,731 kwa maoteo ya mwaka 2010 watu 359,032 kati ya hao, wanaume ni 170,450 na wanawake ni 188,582.
WILAYA YA SERENGETI
Wilaya ya Serengeti ni miongoni mwa Wilaya 6 za Mkoa wa Mara. Wilaya hii ilianza rasmi mwaka 1974 baada ya Wilaya ya Musoma kugawanywa. Mugumu ilifanywa kuwa Makao Makuu ya Wilaya ambapo Mhe. A. Nyemela aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya wa kwanza na Bw. B. Salim aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya wa kwanza. Wilaya hii ilipoanzishwa ilikuwa na tarafa 4 za Rogoro, Serengeti, Nansimo na Kenkombyo pamoja na Majimbo mawili ya Uchaguzi ya Serengeti na Nyamuswa. Mwaka 1978 ilianzishwa Wilaya ya Bunda, kutokana na kugawanyika huko, Kata ya Ngoreme ambayo ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Musoma ikawa tarafa ya Ngoreme katika Wilaya ya Serengeti na tarafa za Serengeti, Nansimo na Kenkombyo zikaunda Wilaya ya Bunda, hivyo Wilaya ya Serengeti ikabaki na tarafa 2 za Rongoro na Ngoreme.
Mwaka 1990 kata ziliongezeka kuwa 18 na vijiji 75. Mamlaka ya Mji wa Mugumu ilianzishwa mwaka 2005 kufanya wilaya kuwa na kata 18 pamoja na vijiji 71. Kwa sasa ina tarafa 4, kata 28 na vijiji 91.
Wilaya ya Serengeti ina kilometa za mraba 10,375 kati ya eneo hilo kilometa za mraba 7,258.05 (Mbuga za wanyama za Serengeti 7,000, pori la Akiba la Grumeti, 68.37 na pori la Akiba la Ikorongo. 189.68) ni eneo la hifadhi ya mbunga za Taifa na kilimeta za mraba 2,456 ni eneo wazi la hifadhi (WMA). Eneo pekee ambalo hutumika kwa shughuli za kilimo, ufugaji na makazi ya watu ni kilometa za mraba 659.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi, mwaka 1978 Wilaya ya Serengeti ilikuwa na watu 207,688 ikijumuisha wakazi wa wilaya ya Bunda kabla haijaundwa. Sensa zilizofuata zilionyesha kuwa mwaka 1988 ilikuwa na watu 111,710, mwaka 2002 ilikuwa na watu 176,609, mwanaume 84,263 na wanawake 92,346 na mwaka 2012 Kwa maoteo ya mwaka 2010 wilaya hii ina watu 227,698 kati ya hao, wanaume ni 110,536 na wanawake ni 117,162.
HISTORIA YA WILAYA YA BUNDA
Wilaya ya Bunda ni miongoni mwa Wilaya 5 za Mkoa wa Mara, ilianzishwa kama wilaya ndogo ikiwa chini ya mamlaka ya Wilaya ya South Mara kwa maelezo ya barua kumb. Na. VPC.R.70/17 ya tarehe 23/4/1964. Wilayah ii ilifanywa wilaya kamili kwa Tangazo la Serikali Na. 178 la tarehe 21/01/1978, baada ya kugawanywa Wilaya ya Serengeti. Kutokana na mgawanyo huo, Tarafa za Serengeti, Nansimo na Kenkombyo zilitoka Wilaya ya Serengeti kuunda wilaya ya Bunda.
Hivyo wilaya ya Bunda ikawa na tarafa 3, kata 27, vijiji 72 na jimbo moja la Uchaguzi la Nyamuswa. Mwaka 2006 ilianziswa tarafa ya Chamuroho na kufanya wilaya kuwa na Tarafa 4, kata 28 na vijiji 106. Mwaka 1990 jimbo jipya la uchaguzi la Mwibara lilianzishwa na kufanya Wilaya kuwa na Majimbo 2 (Bunda na Mwibara) ya Uchaguzi.
Kwa upande wa kaskazini inapakana na Wilaya ya Musoma, Wilaya ya Serengeti kwa upande wa mashariki, Wilaya za Magu na Ukerewe za Mkoa wa Mwanza kwa upande wa kusini na magharibi.
Wilayah ii ina eneo la Kilometa za mraba 3,088; kati ya hizo Kilometa za mraba 200 ni eneo la maji ya Ziwa Victoria na Kilometa za mraba 2,888 ni nchi kavu. Eneo linalofaa kwa kilimo na ufugaji ni kilometa za mraba 2,408. Sehemu iliyobaki ya kilometa za mraba 480 iko ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti na pori la Akiba Ikorongo.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi, mwaka 1988 wilaya ya Bunda ilikuwa na watu 190,386. Mwaka 2002 ilikuwa na watu 259,827 (wanaume 124,310 na wanawake 135,517). Kwa matokeo ya mwaka 2010 wilaya hii ilikadiriwa kuwa na watu 348,270 kati ya hao, wanaume ni 178,915 na wanawake ni 169,355.
WILAYA YA RORYA
Wilaya ya Rorya ni miongoni mwa Wilaya 5 za Mkoa wa Mara. Wilayah ii ilianza rasmi tarehe 01/07/2007 baada ya kugawanywa kutoka Wilaya ya Tarime ikiwa na Tarafa 4 (Suba, Luo Imbo, Girango na Nyancha) Kata 21, vijiji 80 na Jimbo 1 (Rorya) la Uchaguzi. Asili ya jina la Wilaya hii ni mlima Rorya.
Mkuu wa Wilaya wa kwanza ni Mhe. Lt Kanali (Mstaafu) Benedict K. Kitenga na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya wa kwanza alikuwa Bw. Jacob A. Kayenga kati ya 1.07.2007 na 19.11.2009.
Wilaya ina ukubwa wa kilometa za mraba 9,345.496 ambazo zimegawanyika kama ifuatavyo:
Eneo la maji (Ziwa Victoria) kilometa za mraba 7,252 sawa na 77.6%
Eneo la ardhi (Nchi kavu) kilometa za mraba 2,093.496 sawa na 22.4%
Wilaya inapakana na nchi ya Kenya kwa upande wa Kaskazini, Wilaya ya Tarime kwa upande wa Mashariki, Wilaya ya Musoma kwa upande wa Kusini na Nchi ya Uganda kwa upande wa Magharibi.
Mgawanyo wa Wilaya Kiutawala:
Kiutawala,Wilaya inaundwa na Tarafa nne (4), Kata ishirini na moja (21) na Vijiji themanini (80).
Idadi ya Watu:
Kwa maoteo ya mwaka 2010, Wilaya ya Rorya ilikadiriwa kuwa na wakazi 280,075 kati ya hao, wanaume ni 134,646 na wanawake ni 145,429.
Hali ya Uchumi wa Mkoa wa Mara
Uchumi wa Mkoa wa Mara unategemea kilimo ambacho huchangia kiasi cha 60% ya pato la Mkoa. Sekta nyingine ni ambazo huchangia kwenye uchumi wa Mkoa ni mifugo, madini na uvuvi. Hata hivyo mazao ya kilimo yamekuwa yanatagemea sana upatikanaji wa mvua. Kutokana na hali hii Mkoa umeweka jitihada za makusudi katika kujenga miundombinu itakayosaidia kilimo cha umwagiliaji kwa kuvuna maji ya mvua kwa njia ya Malambo na makinga maji. Matokeo ya juhudi hizi ni kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali hususan mpunga.
Mpango wa kuondoa umaskini
Ujinga, umaskini na maradhi ni maadui watatu wa maendeleo ambao mara baada ya kupata uhuru mwaka 1961,
Tanzania ilitangaza vita dhidi ya maadui hawa.
Katika azma ya kutokomeza umaskini Mkoa umeweka kipaumbele katika kubuni na kutekeleza mipango inayolenga kuwaendeleza wananchi wake, hivyo kuwapunguzia umaskini. Mipango hii inahusisha serikali, wananchi wenyewe, taasisi mbalimbali,
sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na wahisani mbalimbali.
Tanzania ilitangaza vita dhidi ya maadui hawa.
Katika azma ya kutokomeza umaskini Mkoa umeweka kipaumbele katika kubuni na kutekeleza mipango inayolenga kuwaendeleza wananchi wake, hivyo kuwapunguzia umaskini. Mipango hii inahusisha serikali, wananchi wenyewe, taasisi mbalimbali,
sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na wahisani mbalimbali.
Ili kuinua ubora wa maisha ya wananchi,
Mkoa umeweka mikakati mbalimbali yenye lengo la kuongeza wingi na ubora wa huduma za afya, elimu, maji, mawasiliano na uchukuzi, kuendeleza kilimo na ushirika.
Mkoa umeweka mikakati mbalimbali yenye lengo la kuongeza wingi na ubora wa huduma za afya, elimu, maji, mawasiliano na uchukuzi, kuendeleza kilimo na ushirika.













No comments:
Post a Comment