Thursday, 20 November 2014

WENGI WANAPENDA HARUSI SIO NDOA!


NI Jumanne nyingine njema na inayompendeza Mwenyezi Mungu katika uumbaji wake. Mimi niko mzima wa afya njema ndiyo maana namwagika tena kwenye safu hii. Mada yetu wiki iliyopita ilisema; Mwanamke wa kumuoa hana sifa ya kuwa mke. Wengi walinipigia simu wakipongeza, wengine wakinikandia kwamba si kweli. Akisha kuwa mpenzi anaweza kuwa mke na akaendelea kuwa mpenzi.




Nilichobaini, kama mtu alisoma kwa umakini alinielewa vizuri, lakini kama alipita juujuu ndiyo wenzangu na mimi, wale waliokuwa hawakubaliani nami. Wiki hii mada yetu inasema; wengi wanapenda harusi kuliko ndoa.

Mada hii imeegemea kwenye tabia za ndoa za siku hizi, nyingi zinavunjika kila kukicha tofauti na zamani.

KWANZA TUTAMBUE HILI
Kabla sijaanza kuchimba napenda kuwapa elimu wasomaji wangu ambao hawatofautishi kati ya ndoa na harusi. Nimekuwa nikiwasikia baadhi ya watu wakisema, ‘mwezi ujao nitafunga harusi’ wakimaanisha watafunga ndoa.

Napenda kufafanua kuwa, ndoa ni kile kitendo kinachofanywa na viongozi wa dini kuwaunganisha wawili walioamua kuishi kama mke na mume. Harusi ni sherehe zinazotokana na kufungwa kwa ndoa. Au niseme harusi ni sherehe ya ndoa. Watu wanaweza kufunga ndoa lakini wasifanye harusi lakini hakuna anayeweza kufanya harusi bila kufunga ndoa. Tupo pamoja!?

JIBU LA UTAFITI 
Nilipata bahati ya kufanya utafiti mbalimbali kwa baadhi ya watu walionizidi umri. Wengi wao walisema sababu zinazofanana, kuwa wengi wanapenda harusi kuliko ndoa, na mimi nikabaini kuwa ni kweli.

KWA NINI?
Hapa ndipo kwenye kiini cha yote. Utafiti ulionesha kuwa, wawili wanapokutana na kuanzisha uhusiano huweka malengo kwamba lazima siku za usoni wafunge ndoa. Maana yake hapa, waje kuwa mke na mume.

Lakini utafiti umebaini kuwa, siku zikifika na wachumba hao wanapochukua uamuzi wa kufunga ndoa huitisha vikao vya kifamilia na maandalizi huanza mara moja ambapo vikao vya harusi huanza kwa ajili ya sherehe ya ndoa.

MAANDALIZI MAREFU KWA SHUGHULI FUPI
Vikao vya harusi huweza kuchukua hata miezi mitatu wakati mwingine kwa ajili ya harusi ya siku moja tu!! Hii ni ajabu sana.

Ni kipindi hicho ambapo bibi harusi atakuwa akipanga kushona gauni la maana, kuvaa viatu vizuri, kutafuta saluni yenye jina kubwa mjini kwa kupamba maharusi. Kichwani huwaza jinsi atakavyomeremeta siku ya harusi yake ukumbini. Wakati mwingine huwaza kuwa, harusi iwe kubwa sana, waalikwa wale na kunywa na kusaza kwani ndiyo ufahari na kuwaumiza akina Jane, Anna na Fatuma ambao harusi zao hazikuwa na chakula kizuri, vinywaji kiduchu na MC hakuwa maarufu.

Nimewahi kushuhudia bibi harusi akipungua mwili kwa sababu ya mawazo ya siku ya harusi yake. Hasa linapokuja suala la kukwamakwama kwa baadhi ya mambo.
Bwana harusi naye huwa kwenye mawazo hayohayo, kwamba anatamani suti atakayovaa watu wamuulize aliiagizia kutoka wapi. Atawaza atakavyokuwa siku ya harusi yake kule ukumbini.

MAWAZO KUHUSU NDOA WEKA PEMBENI
Katika nyakati hizo, hakuna anayewaza kwamba sasa anaingia kwenye maisha ya ndoa. Maisha ambayo mke atatakiwa kujua wajibu wake kwa mume na mume kujua kwa mke. Maisha yanayohitaji uvumilivu wa ndoa kuliko uvumilivu wa kung’olewa jino.
Matokeo yake watu wanaingia kwenye ndoa wakiwa hawana mawazo wala utayari. Hii husababisha ugomvi kidogo ndoa chali!! Na watu watasema harusi yao ilikuwa kubwa lakini ndoa haikudumu!

NINAWALAUMU VIONGOZI WA DINI
Katika mazingira haya, nisiwe mnafiki, mimi lawama zangu zote nazitupa kwa viongozi wa dini wenye mamlaka ya kufungisha ndoa.

Nawalaumu kwa sababu wao ndiyo wanaopaswa kutoa elimu ya ndoa kwa wahusika. Kwamba wanapouliza ‘uko tayari kuishi na mwenzako katika tabu na raha?’ wazitaje hizo tabu maana wanandoa wengi wanajua tabu zinazotajwa hapo ni kula mlo mmoja kwa siku, kutonunuliwa kanga mwisho wa mwezi au kula ugali na maharage wakati majirani wanakaangiza nyama!

Kumbe tabu ni pamoja na kufumania laivu, mke kupewa mimba na mwanaume mwingine au mume kuleta mtoto wa nje ya ndoa, mume kuwa mlevi wa kupindukia hadi kulala baa na mambo mengine mazito katika ndoa ambapo inabidi kuvumiliana.

Kama viongozi wa dini wangekuwa wanayasema haya katika msisitizo wa hali ya juu ingekuwa rahisi wachumba kuchukua muda mrefu kuiwaza ndoa wanayokwenda kuishi kuliko kupenda harusi kwa kutoa mapesa mengi ili siku hiyo waonekane wa tofauti.

GPL

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!