KATI ya watu 4,879 mkoani hapa waliopima afya zao kwa hiari katika kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septembam waka huu, 305 wamebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).
Akizungumza katika kikao cha utekelezaji wa shughuli za Ukimwi zilizotekelezwa na Kamati ya Kudhibiti Ukimwi mbele ya Baraza la Madiwani juzi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Gervas Ndaki, alisema kati ya waliojitokeza kupima na kupata ushauri nasaha, wanaume walikuwa 2,417 na wanawake 2,467.
Ndaki, alisema kati ya watu 305 waliopima kwa hiari na kukutwa na maambukizi, wanaume walikuwa 124 na wanawake 181.
Alisema huduma ya kuzuia maambukizi ya vvu/ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, wajawazito 1,036 walijitokeza na kupata ushauri nasaha na kupima, kati yao wajawazito 10 sawa na asilimia moja walikutwa na maambukizi.
Ndaki, alisema mapambano ya ukimwi yanaambatana na huduma za tiba sahihi ya magonjwa ya ngono.
Alisema kuwa moja ya njia ya kupambana na maambukizi mapya ni tohara kwa wanaume na waliojitokeza walikuwa 539 ambao walitahiriwa na kati ya hao waliokutwa na maambukizi ya vvu walikuwa saba.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi, aliwataka watendaji kuweka mkazo katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi, kwa kuwasisitiza wananchi kwa kuwapa elimu kuondokana na maambukizi mapya.
No comments:
Post a Comment