Monday 17 November 2014

WATU 13 MBARONI KWA MAUAJI KITETO

Kiteto. Polisi mkoani Manyara wanawashikilia zaidi ya watu 13 wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya wakulima na wafugaji yaliyotokea wiki iliyopita katika Kata za Matui na Kiperesa wilayani hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki amesema bado wanaendelea na uchunguzi kabla ya kuchukua hatua ya kuwafikisha mahakamani watu hao.
“Hatuwezi kutaja idadi kamili wala majina yao ila ni zaidi ya watu 13 tunawashikilia, wanadaiwa kuhusika na tukio hilo la mauaji na baada ya uchunguzi wetu wahusika tutakaowabaini tutawafikisha mahakamani,” alisema.
Hata hivyo, jana na juzi hali ilikuwa shwari katika eneo hilo huku wakazi wilayani humo wakishuhudia helikopta ya polisi ikiwa na makamishna kutoka Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam ikizunguka angani kuendelea na ulinzi.
Naye, Mkuu wa Mkoa huo, Eraston Mbwilo akizungumza kwenye kikao cha ushauri cha mkoa, alisema chanzo cha mgogoro wa ardhi na mauaji hayo ya Kiteto yanasababishwa na baadhi ya watu kuhodhi ekari za ardhi bila ya kuwa na vibali.
“Hili suala la baadhi ya watu kudai kuwa Kiteto imegeuka kuwa Somalia siyo kweli, mgogoro wa Emboley Murtangos unasababishwa na baadhi ya watu kujimilikisha ekari nyingi za ardhi kiholela,” alisema Mbwilo na kuongeza:
“Unamkuta mtu anamiliki ekari zaidi ya 500 kiholela, huu ni ukiukwaji wa sheria, vijiji vina utaratibu wa kugawa maeneo, kwa nini wasiufuate?” alihoji.
Alisema kwa sasa hali ni shwari katika eneo hilo na wanaendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa jamii ya wakulima na wafugaji ili kuhakikisha kuwa mauaji na vurugu hizo havitokei tena.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!