Tuesday 4 November 2014

WAREMBO WALIVYONYONGWA DAR



DUNIA hii basi tena! Ni tukio la kusisimua ukilisoma mwanzo hadi mwisho lakini ni la kikatili sana! Ni lile la ndugu wawili warembo, dada na mdogo wake kukutwa wamekufa kwa kunyongwa ndani ya nyumba aliyokuwa amepanga mmoja wao huku muuaji akidaiwa alivaa taulo lenye weupe wa kufifia akitokomea zake.



Nuru Tumwaga enzi za uhai wake.
ENEO LA TUKIO
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea hivi karibuni kwenye Mtaa wa Mji Mpya, Kata ya Azimio wilayani Temeke jijini Dar es Salaam ambapo warembo hao, Mariam Buruhani (39) na dada yake Nuru Tumwaga (42) (pichani) walikutwa wamekufa katika nyumba hiyo aliyopanga Mariam.
UWAZI LAFUATILIA
Uwazi kama lilivyo kawaida yake, baada ya kuipata taarifa za kuwepo kwa vifo hivyo vya usiku mmoja, lilianza kufuatilia hatua kwa hatua.Kwa mujibu wa ndugu mmoja, mchana wa kuelekea siku ya tukio ambayo ni Jumamosi usiku, marehemu wote walionekana wakiwa wazima wa afya ambapo Mariam alikuwa kwenye saluni yake ya kike na Nuru akiendelea na shughuli zake  za kuwaremba wanawake wenzake.
Ikadaiwa kuwa, nje ya saluni ya Mariam kulikuwa na gari dogo jeusi ambalo huwa linapaki maeneo hayo kila wakati ikisemekana mmiliki wake ni bwana wa Mariam ambaye jina halikufahamika mara moja.
Mariam Buruhani enzi za uhai wake.
GARI LAONDOKA
Ndugu huyo aliongeza: “Baadaye lile gari liliondoka na kwenda kusikojulikana, Mariam alibaki saluni.
MARIAM AFUNGA SALUNI
“Ilipofika saa moja usiku, Mariam alifunga ofisi na kwenda nyumbani kwake akiwa ameongozana na Nuru ambaye alikuja jijini Dar kwa Mariam akitokea Mtwara. Mariam ni mtoto wa mama mkubwa wa Nuru.“Baada ya kufika nyumbani, Mariam alitoka kwenda dukani kwa ajili ya kununua mahitaji ambapo alinunua juisi chupa tatu, mafuta ya taa na mahitaji mengine.”
INAVYODAIWA
Habari zaidi kutoka kwa ndugu huyo zilidai kuwa, wiki moja nyuma marehemu Mariam aliomba hati ya nyumba yake iliyoko Tandika kwa lengo la kuiuza kwa vile alipata mteja.
“Siku ya tukio, ilikuwa mteja wake afike kwa ajili ya ununuzi wa nyumba hiyo lakini kwa bahati mbaya hakufika, alikuwa na matatizo.
Wanafamilia wakiwa na nyuso za simanzi.
“Kesho yake, Jumapili saa sita mchana yule mteja alifika nyumbani kwa kaka wa marehemu aitwaye Abdallah ambapo ni jirani na alipopanga Mariam, kaka akamtuma mtoto wake kwenda kumwita shangazi yake (Mariam).“Lakini cha kushangaza, mtoto huyo alichelewa kurudi ndipo kaka mtu na watu wale waliamua kufuatilia,” alisema ndugu huyo.
MSIKIE KAKA MTU
“Tulipoona mtoto harudi tukafuata, kufika tulishtuka sana kumkuta Mariam amelala sebuleni amekufa, kuingia chumbani tukamkuta Nuru naye amelala kitandani amekufa,” alisema kaka mtu.
MAUZO YA NYUMBA YANATAJWA
Kaka wa Mariam aliendelea kusema: “Tunaamini muuaji alijua marehemu ameuza  nyumba  na pesa anazo ndani.”
VYANZO ENEO LA TUKIO.
Naye jirani na Mariam (aliomba jina lake lihifadhiwe) akizungumza na Uwazi kuhusu mazingira ya kunyongwa kwa warembo hao alisema:
Waombolezaji wakiwa msibani.
“Usiku wa tukio mimi nilichungulia dirishani baada ya kusikia mtu akitembea, nikamuona mwanaume amevaa taulo lenye weupe wa kufifia. Nilipomwangalia vizuri nikagundua ni bwana’ake da’ Mariam maana namfahamu.
“Baada ya muda nikasikia mngurumo wa gari, nikachungulia tena nje nikaliona gari ambalo ni la bwana’ke da’ Mariam likiondoka eneo hilo.“Sikujali, niliamini tuko salama. Nilipoamka asubuhi  nikawa namuona  mtu amelala sebuleni kwa Mariam, nikajua kwa vile ni Jumapili, huenda  amepumzika, sikujua ni marehemu Mariam mpaka kaka yake alipofika na watu wenegine na kubainisha kuwa, kumbe wote waliolala ndani humo walikuwa wameuawa, inauma sana.”
SERIKALI YA MTAA
Kwa upande wake Mwenyekiti wa  Serikali ya Mtaa wa Azimio, Wadudi Mlangwa akizungumza na waandishi wetu ofisini kwake alisema yeye ni kati ya viongozi wa mwanzo kufika eneo la tukio baada ya kupigiwa simu na kaka wa marehemu.
Mwili wa Nuru ukiswaliwa kwa ajili ya mazishi.
“Tulipofika tulikuta mwili wa Mariam uko sebuleni na mwili wa Nuru uko chumbani, wote wakiwa  wameaga dunia. Hapo ilikuwa saa saba na nusu mchana wa Jumapili Oktoba 26, mwaka huu,” alisema.Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, baada ya kuthibitisha hali hiyo aliagiza miili hiyo isiguswe  hadi  polisi  wafike kwa  hatua zaidi.
UCHUNGUZI WA  AWALI WA KIDAKTARI
Uchunguzi wa awali uliofanywa  na madaktari wa Hospitali ya Temeke jijini Dar ulibaini kuwa, marahemu hao walinyongwa kwani shingo zao zilikutwa zimepindia upande.
NINI KILIFANYIKA BAADA YA MAUAJI?
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa  baada ya mauaji hayo, chumba cha marehemu Mariam kilionekana kupekuliwa kila sehemu.  Baada ya upekuzi huo, mpekuaji alichukua redio, tivii na vitu  vingine ambavyo vinaendelea kufuatiliwa na polisi.
Mwili wa Mariam Buruhani ukiswaliwa kwa ajili ya mazishi.
MAZISHI YAO
Mariam alizikwa Jumatatu ya Oktoba 27, mwaka huu kwenye Makaburi ya Wailesi Temeke, Nuru alisafirishwa  siku hiyohiyo na kwenda kuzikwa kwao, Mtwara Jumanne ya Oktoba 28, 2014.
KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, SACP  Kihenya wa Kihenya alithibitisha kutokea kwa  tukio hilo, “Tunamtafuta mtu aliyehusika na mauaji hayo ambaye anatajwa alivaa taulo,” alisema

CHANZO: GPL

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!