Wednesday, 19 November 2014

VIBANDA 189 VYATEKETEA KWA MOTO ARUSHA

Vibanda 189 vyateketea Arusha
MOTO mkubwa umeteketeza vibanda 189 vinavyouza bidhaa za asili zinazotengenezwa kwa ngozi, shanga na vinyago vya kuchonga vilivyoko eneo la Mount Meru curios & crafts maarufu kama Maasai Market.


Baadhi ya wafanyabiashara hao walionekana kupoteza fahamu na kuanguka huku kukiwa na taarifa za wengine kupelekwa hospitali kutokana na mshituko walioupata wa kuunguliwa bidhaa zao ambapo inadaiwa hali hiyo inatokana na wengi kuchukua mikopo benki kwa ajili ya kuendesha biashara hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Musa Kahulula alisema kuwa moto huo ulianza juzi kati ya saa 3:30 na 4:00 usiku ambapo hakuna kibanda hata kimoja kilichonusurika.
Alisema kuwa moto huo ulianzia eneo la nyuma ambapo kuna uzio na ulisambaa kuelekea eneo la mbele ambapo vibanda vyote vilivyokuwa kwenye eneo hilo linalomikiliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Arusha, vimeteketea kabisa pamoja na bidhaa zilizokuwa ndani.
” Kwa kweli bado hatujajua chanzo cha moto huu kwani hapa hatuna umeme wala hatukuutaka kwa ajili ya usalama wa eneo hili tulilojenga kwa mbao na mabati na eneo la mgahawa lililojengwa kwa matofali lililokuwa likitumika kupika wala halijafikiwa na moto.
“Hatukuwa tunaruhusu hata matumizi ya sigara ili kuhakikisha tuko salama ndiyo maana tunasema kwa sasa hatujui chanzo mpaka vyombo vya usalama vitakapotoa maelezo,” alisema Kahulula.
Alisema kuwa walihamia kwenye eneo hilo kuanzia mwaka 2004 ambapo walikuwa wanalipa kodi ya sh. 40,000 kwa mwezi.
“Kwa sasa tumeitwa na kamati ya siasa ya CCM kwa ajili ya kujadili suala hili ila hapa tumekuwabaliana tuongee viongozi kwa sababu hapa watu wengine bado hawako vizuri kutokana na hasara tuliyopata,” alisema Kahulula huku akielekea kwenye kikao.
Kwa upande wao wafanyabiashara waliounguliwa na mabanda wakiongea na mwandishi wa habari hizi kwa sharti la kutoandikwa majina yao magazetini, walisema kuwa walikuwa na mvutano ya CCM kwa miaka sita sasa kutokana na uamuzi wao wa kuwanyima mikataba.
“Hapa wengi tumechanganyikiwa kwa sababu tuna mikopo kutoka benki mbalimbali, Serikali ingeangalia uwezekano hata wa kutujengea vibanda vingine ili tuweze kuendelea na biashara tulipe mikopo ili kuepusha nyumba na vitu vingine tulivyoweka kama dhamana za mikopo benki visiuzwe,” alisema mjasiriamali mwingine.
Mwananchi mwingine Musa Mollel alisema amefika eneo hilo kumwakilisha rafiki yake, Ally Shaban ambaye ana kibanda eneo hilo na amelazwa hospitali ya mkoa Mount Meru kutokana na mshituko alioupata baada ya kufika na kuona namna eneo hilo lilivyoteketea kwa moto.
Hata hivyo wafanyabiashara wengine walitupia lawama kikosi cha uokoaji walichodai kuwa kilishindwa kuzima vibanda vyao licha ya kuwa umbali ya chini ya mita 200 kutoka eneo hilo.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa (RPC), Liberatus Sabas, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ingawa chanzo chake bado hakijafahamika.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, kamanda huyo alisema kuwa hakuna mwanadamu aliyepata madhara yoyote kutokana na moto huo ambapo dhamani ya vitu na mabanda hayo bado haijafahamika

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!