Sunday 23 November 2014

UNAJUA MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI UNAPOWEKA MALENGO KATIKA MAISHA

Je una malengo uliyoweka katika maisha yako? Kama unayo uliyaweka lini na una hakika kama uliyaandaa inavyostahili? Kama huna malengo ama unayo lakini huna hakika kama yameandaliwa inavyopasa usisikitike kwa sababu hii ni changamoto inayowakabili watu wengi katika maisha. Kuna watu wengi wanaosuasua katika maisha bila kuwa na malengo. Hivyo, hawana furaha wala maendeleo katika maisha yao.


Kuna wakati nilijaribu kuwauliza baadhi ya marafiki na jamaa zangu kama wana malengo. Nilistaajabu kugundua kuwa siyo tu hawakuwa na malengo, lakini hawakuwa wakijua kama ni lazima wawe na malengo, yanatakiwa yawe yanahusu nini na yanaandaliwa vipi.
Lakini nilipoendelea kuwauliza maswali mawili au zaidi niligundua karibuni kila mmoja alikuwa nayo lakini hakuwa na yakini kama hayo ndiyo malengo ya maisha yake. Nilihuzunika kwa sababu mtu kuwa na lengo ambalo hujalitafakari na kulibuni na hata kulitambua ni kama huna lengo. Hii ni kwa sababu wala hakuna chochote utakachofanya kuhusu lengo kama hilo.

Tunapotafakari swali kuwa tuandae malengo ya maisha kuhusu nini jibu ni rahisi. Kwa hakika malengo yetu yatahusiana na mambo tunayoyatarajia katika maisha yetu. Watu wengi wana matarajio yanayofanana. Wanatamani kuwa matajiri, wawe na nyumba nzuri, wawe na karibuni vitu vyote muhimu na vya starehe vinavyohitajika katika maisha. Watu wanapenda watoto wao wawe na fursa ya kupata elimu na afya bora na wawe na furaha na shangwe wakati wote. Wanapenda kuwa na maisha ya furaha na starehe kwa kuwa na fedha zozote wanazohitaji ili kupata aina ya maisha wanayoyataka. Tena watu wanatarajia wapendwe na wawe na manufaa kwa binadamu wenzao.
Muhimu zaidi ni kila mtu kuwa na sababu au kusudi la kuishi. Hivyo, malengo yetu yanabidi yalenge katika nyanja mbalimbali kama vile malengo katika kazi, malengo katika riziki, malengo katika kipato, malengo katika afya, malengo katika dini na nyanja nyingine muhimu kadha wa kadha katika maisha. Hata hivyo, kwa sababu haya ni mahitaji, hatu budi kuyaandalia malengo na kuyafanyia kazi ili tuweze kupata mafanikio. Ni lazima tukumbuke kuwa mafanikio huwa hayaji yenyewe mpaka yapangiwe malengo. Kuna mambo mengi yakuzingatiwa katika kuandaa malengo.
Mambo ya kuzimgatiwa katika kuandaa malengo.
(a) Kuwa na hakika na matarajio
Jambo la muhimu katika maisha yako ni kujua kile unachokihitaji. Kutokujua unachokitaka ni kama kuanza safari bila kujua mahali uendako. Katika safari ya aina hiyo wala hatajua upande gani uelekee, yaani barabara gani uifuate na uende umbali gani. Kumbuka unakoelekea katika maisha yako ndilo lengo lako. Tunaposema malengo katika kazi tuna maana unakusudia kuelekea wapi katika kazi yako na unatarajia ikufikishe wapi.
Unapoandaa malengo huna budi kujibu maswali Nini? Wapi? na Vipi? Mathalani kama unaandaa lengo kuhusu jambo lolote jiulize maswali haya makuu matatu yaani kama linahusu kipato, kutokee nini? Matokeo haya yafanyike wapi na yafanyike vipi ili upate hali inayotarajiwa katika lengo lako.
Kumbuka wewe kama mtu mzima na mwenye akili kamili unapaswa kushika dhamana kamili ya maisha yako. Tena ni lazima ukubali wajibu ulionao kwa maisha yako na kwamba hakuna mtu mwingine yeyote mwenye wajibu wa maisha yako kama vile baba na mama wanavyokuwa na wajibu kamili kwa maisha ya mtoto wao. Wewe ndiwe unayetakiwa kujua vitu unavyovitaka katika maisha yako na uviwekee malengo.
(b) Weka malengo sahihi
Ninakumbuka katika utafiti wangu niliwahi siku moja kukaa na watoto wadogo wa umri wa kuanza shule za chekechea. Nilikuwa nawauliza watakapokuwa watu wazima watapendelea kufanya kazi gani. Nilipata majibu mazuri na ya kufurahisha sana ila kuna mtoto mmoja alinipatia jibu lililonishangaza sana yeye alisema atakapokuwa mtu mzima atapendelea kuwa jambazi kwa sababu kazi hiyo itaweza kumpatia fedha nyingi na kuweza kupata kila anachokitaka katika maisha. Ingawa nilijitahidi kumfahamisha akaelewa madhara ya ujambazi lakini hilo ndilo lililokuwa lengo lake.
Huyu alikuwa mtoto lakini hatutazami kuwa mtu mzima atajiwekea lengo lisilo sahihi kama hili. Unapoamua kuweka malengo ya maisha yako inakubidi ufikiri kwa umakini zaidi kuliko unavyoweza kufikiria kitu chochote katika maisha yako. Unatakiwa kufanya kile ambacho wanasaikolojia hukiita; “Mtu kuzungumza na akili yake yeye mwenyewe” Ataweza kufanya hivyo tu iwapo ataondoa mawazo mengine yote katika kichwa chako na kubaki peke yako na nafsi yako ili uweze kuchagua malengo bora na sahihi.
Huna budi kukumbuka kuwa kila jambo utakalolichagua uhakikishe halitakuwa na athari kwako mwenyewe au kwa watu wengine. Unaweza kuchagua jambo ambalo kwa haraka litaweza kuonekana kuwa ni zuri lakini kwa upande mwingine likawa na madhara. Kuna ukweli kuwa kila jambo linaweza kuwa zuri kwa wote lakini likawa silo linalomfaa kila mtu.
(c) Unda lengo chanya
Dhamira ya mtu huweka katika maneno. Unapoingia kitandani usiku kama kuna jambo ambalo unakusudia kulifanya utakapoamka siku ya pili, utaweza kuweka nia kwa kutamka maneno peke yako “Kesho asubuhi nitakwenda benki kufungua akaunti” Hivi ndivyo tunavyounda malengo yetu. Matamko ya malengo yako usiyaweke katika mfumo hasi bali yote yaweke katika mfumo chanya. Kwa mfano ukisema lengo “Niache kususua katika kufanya shughuli zinazoniletea riziki” huu ni mfumo hasi. Mfumo chanya wa lengo hili ungeweza kuandikwa “Kuongeza ujasiri katika kufanya shughuli zote zinazonipatia riziri”
(d) Kuandaa matamko ya matarajio yaliyo mafupi na wazi
Mtu anapobuni tarajio lake ahakikishe lisiwe refu kwa kuwekewa maneno mengi bali liwe fupi na lenye maana iliyo wazi.
(e) Malengo yawe ya kweli na yenye changamoto
Watu wengine wanapoandaa malengo hubuni yale tu ambayo wanafikiria wanaweza kuyatekeleza kwa urahisi na kuyaacha yale ambayo huwa wanahisi huenda wakashindwa kuyatekeleza hata kama ndiyo malengo muhimu zaidi kwa maisha yao. Kipimo chetu katika kuandaa malengo kiwe kuweka yale yatakayotuwezesha kupata mafanikio tunayoyahitaji ili kuendelea na kupata kile tunachokihitaji katika maisha. Ugumu wa kutekelezeka kwa lengo ndizo changamoto ambayo ni sifa muhimu sana katika malengo yanayofaa.
(f) Matamko ya malengo yataje viashiria vya mafanikio
Matamko ya malengo yanayoandaliwa yawe yanataja viashirio vitakavyomwezesha aliyeyaweka kutambua kama matokeo yaliyotarajiwa yanapatikana. Ni vyema unapoandaa tamko lako la lengo litaje pia mambo kama vile mafanikio yanayotarajiwa yatakuwa ya aina gani, yatatokea lini na katika mazingira gani. Kwa mfano tamko la lengo linaweza kuandikwa kama hivi “Katika mkesha wa kuamkia mwaka 2016 mimi na familia yangu tuwe katika nyumba ya kisasa tuliyojenga wenyewe katika sehemu za nje ya Jiji la Dar es Salaam yenye vyumba vya kutosha na viwanja vya kuchezea watoto wetu”
Tamko kama hili linaviashiria vya matokeo kama vile; muda (mwishoni mwa mwaka 2016); sifa ya kilichotaraji (nyumba ya kisasa yenye vyumba vya kutosha na viwanja vya kuchezea); mahali: (Nje ya Jiji la Dar es Salaam).
Hitimisho
Katika makala hii tumejifunza kuwa mafanikio ndilo lengo kuu la binadamu lakini ni mara chache watu wanajaribu kufafanua waziwazi kile wanachikitaka katika maisha. Njia sahihi ya kuweza kufikia matarajio katika maisha ni kuweka malengo yaliyobuniwa na kuandaliwa vyema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!