Friday, 14 November 2014

ULAJI USIOZINGATIA LISHE BORA ONGEZEKO LA KISUKARI



ULAJI usiozingatia lishe bora na unene uliopitiliza kutokana na kutofanya mazoezi, kumeelezwa kuwa chanzo cha ongezeko kubwa la ugonjwa wa kisukari hapa nchini.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa taasisi inayoshughulikia masuala ya kisukari, Prof. Andrew Swai.


Prof. Swai, alisema ugonjwa huo unazidi kuenea kwa kasi hapa nchini na utafiti uliofanyika mwaka 1980 , wastani wa mtu mmoja kati ya 100 wenye miaka zaidi ya 25 alikuwa na ugonjwa wa kisukari.
“Mwaka 2012, kisukari kimeongezeka kufikia watu tisa kwa kila 100 walio na umri zaidi ya miaka 25, ugonjwa wa shinikisho la damu kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 25, tatizo limeongezeka kutoka watu watano hadi 27 kwa kila watu 100,” alisema.
Aliongeza kuwa, inakisiwa mwaka 2020 magonjwa hayo yasiyo ya kuambukiza yatasababisha asilimia 73 ya vifo vyote duniani na asilimia 60 ya ukubwa wa tatizo la magonjwa duniani.

“Sababu za ongezeko la magonjwa hayo makuu yasiyo ya kuambukiza ni kutokana na ulaji usiofaa, lishe na milo kubadilika, kula kuzidi mahitaji ya mwili na hivyo kunenepa, kula nafaka zilizokobolewa, juisi, keki, maandazi, ‘ice cream’, chocolate na vingine jamii ya hivyo,” alisema na kuongeza.

Sababu nyingine ni kula chumvi nyingi, vyakula vya makopo, nyama choma, samaki wakavu, soseji, mafuta mengi, nyama nono, vyakula vya kukaanga, maandazi, vitumbua, sambusa, kutokula mbogamboga na matunda kiasi cha kutosha, matumizi ya pombe kupita kiasi, kutojishughulisha sana, kukaa muda mrefu darasani, ofisini, kuangalia runinga, kutumia lifti, kupanda magari na kutoshiriki michezo na ngoma za utamaduni.
Akizungumzia ukubwa wa tatizo hilo hapa nchini, Prof. Swai alisema utafiti wa mwaka 2012 uliojumuisha Wilaya 50 nchini Tanzania kuhusu watu wenye miaka 25 na kuendelea, ulionyesha kuwa asilimia 7.5 hawajishughulishi vya kutosha, ambako asilimia 32.4 ni wale wasiojishughulisha kwa nguvu, asilimia 26.0 uzito uliozidi (BM1-25kg/m2), na asilimia 8.7 kiribatumbo (BM1-30kg/m2.)
Alisema kutoshughulisha mwili kumetafsiliwa kama kisababishi cha nne kinachoongoza kwa vifo duniani kote ikiwa ni asilimia 6 na inakadiriwa kunachangia kwa takriban asilimia 17 katika ugonjwa wa moyo na kisukari na asilimia 12 ya vifo kwa watu wenye umri mkubwa, asilimia 10 ya saratani ya matiti na ya utumbo mkubwa.
Prof. Swai, alisema zoezi ni jambo lolote linalohusisha misuli na kusababisha kuongezeka kwa mapigo ya moyo na kasi ya kupumua, kiwango kinachoweza kuleta faida ni mazoezi yasiyopungua dakika 30 kwa siku angalau siku tano kwa wiki na kuhakikisha angalau jasho linatoka kwa dakika dakika 150 kwa wiki.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!