Thursday 13 November 2014

SIASA ZIWEKWE KANDO MGOGORO WA KITETO

Wakati mgogoro kati ya wafugaji na wakulima wilayani Kiteto, mkoani Manyara ukipamba moto kwa kuongezeka kwa matukio ya mauaji ya kutisha na uharibifu wa mali, Serikali imekuwa ikichukua hatua kwa mwendo wa taratibu, huku wanasiasa wakitumia fursa hiyo kujinufaisha kwa kuutumia mgogoro huo kufikia malengo ya kisiasa.

Tunashuhudia sasa mgogoro huo ukichukua sura ya kisiasa kwa baadhi ya wahusika kulitumia jukwaa la Bunge kutimiza malengo hayo.
Tukio la juzi ndani ya Bunge halikutokea kwa bahati mbaya na pengine ndiyo maana baadhi ya watu wanasema lilipangwa.
Ni ukweli usiopingika kwamba suala hilo limekuwa likijitokeza bungeni kila wakati pale Naibu Spika Job Ndugai, ambaye anahusishwa na mgogoro huo, anapokuwa akiongoza vikao vya Bunge.
 Katika tukio la juzi, Mbunge wa Viti Maalumu, Moza Abeid Said (CUF) alisimama na kuomba mwongozo kuhusu mauaji yanayoendelea Kiteto na kutaka kujua hatua ambazo Serikali imechukua.
Kauli ya Serikali ilikuwa kwamba suala hilo lingejadiliwa baadaye wakati taarifa ya Kamati Teule iliyoundwa kuchambua sera kuhusu masuala ya ardhi itakapowasilishwa bungeni. Lakini kwa mshangao wa wengi, Naibu Spika alisimama na kusema kwamba hata yeye alishalizungumzia suala hilo bungeni, huku akisisitiza kwamba Kiteto watu wanauana kama vile haipo Tanzania.
Alisema mauaji yanafanyika kama vile Serikali haipo, huku akifafanua kwamba silaha katika eneo hilo la Kiteto ni kama ilivyo huko Somalia, kwani watu wanamiliki SMG, SR na nyinginezo na akaitaka Serikali kuchukua hatua.
Itakumbukwa kwamba Januari, mwaka huu Naibu Spika huyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa ambalo ni jirani na Kiteto alisema mgogoro huo una sura ya kikabila, huku akiwataka viongozi wa wilaya na mkoa kujiuzulu kwa madai kwamba wanachochea mgogoro huo kwa kuwabagua wapigakura wake wanapokwenda Kiteto kwa shughuli za kilimo.
Madai hayo yalifuatiwa na mengine aliyoyatoa wakati akiongoza kikao cha Bunge, Mei mwaka huu, kwamba Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Martha Umbula ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, ndiye chanzo cha mgogoro huo.
Madai hayo pia yaliwahi kuungwa mkono bungeni na baadhi ya wabunge, akiwamo Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby ambaye pia wapigakura wake wengi wanafanya shughuli za kilimo wilayani Kiteto.
Umbula amejitetea kwamba kama mkuu wa Wilaya amekuwa akifanya mikutano na wakulima na wafugaji, lakini mamluki kutoka Kongwa wamekuwa wakifika na malori na matrekta na kuvuruga mikutano hiyo.
Anasema haoni kama kuwataka wavamizi waondoke kwenye mikutano hiyo ni ubaguzi, kwani hawezi kuzungumza na wananchi wa wilaya nyingine kwa kuwa anawajibika tu kwa wakazi wa Wilaya ya Kiteto.
Polisi wilayani Kiteto wanasema mgogoro huo hautaisha iwapo wanasiasa hawataacha kuuchochea.
Tunajiuliza kama kweli Naibu Spika Ndugai haoni kwamba Bunge siyo jukwaa sahihi kuzungumzia suala ambalo siyo tu ana masilahi binafsi, bali pia kuzungumzia suala hilo pasipo kutoa nafasi kwa upande wa pili kujibu tuhuma dhidi yake.
Pamoja na watu wengi kupoteza maisha na wengine mali zao kuharibiwa, Serikali imebaki kuwa mtazamaji kama vile ina masilahi fulani katika mgogoro huo.
Tusubiri tuone kama taarifa ya Tume Teule itakayowasilishwa katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma hivi sasa itaonyesha njia kuhusu namna ya kutatua mgogoro huo wa muda mrefu
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!