Saturday, 15 November 2014

SERIKALI YA TANZANIA NA MAREKANI ZATILIANA SAINI MKATABA YA KUANDAA MIRADI YA SEKTA YA NISHATI

images


Na Beatrice Lyimo- Maelezo-DSM.
Serikali ya Marekani na Tanzania zimetiliana saini kwa ajili ya kuandaa miradi katika sekta ya nishati itakayofadhiliwa katika awamu ya pili ya Mkataba wa Millennium Challenge Corporation (MCC).



Utiaji saini wa mkataba huo ulifanyika katika Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam ambapo Makamu wa Rais wa MCC Bw. Kamran Khan  anayeshughulikia Mikataba na Uendeshaji wake pamoja na Waziri wa Fedha  wa Tanzania , Mhe. Saada Mkuya ukishuhudiwa na Balozi wa Marekani nchini Mark Childress.
Akiongea wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Mkuya alisema kuwa MCC imeipatia Serikali ya Tanzania shilingi bilioni 17 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa MCC II ambapo mraadi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa hapo mwakani ukiwa na lengo la kusaidia miundombinu ya umeme nchini.
Makubaliano hayo ni muendelezo wa ubia imara kati ya Marekani na Tanzania kati ya mwaka 2008 na 2013 ambapo MCC ilitekeleza mkataba wa miradi mikubwa ya uwekezaji katika sekta za maji, barabara, na nishati ya umeme nchini.
Miradi hiyo iligharimu jumla ya Dola za kimarekani milioni 698, chini ya mkataba huo mtandao wa nyaya za umeme wenye zaidi ya kilometa 3,000 ulijengwa.
Kwa kuzingatia mafanikio hayo katika utekelezaji wa wa programu zilizokuwa chini ya mkataba wa kwanza kuwahi kutolewa na MCC, taasisi hiyo iliichagua tena Tanzania kuingia katika mkataba wa pili utakaolenga sekta ya Nishati katika miundombinu pamoja na mageuzi ya kisera na mifumo ya udhibiti na kitaasisi.
Aidha, upembuzi yakinifu utaiwezesha Tanzania kuandaa miradi itakayoleta mageuzi katika sekta ya Nishati ikiwa ni pamoja na kuboresha utendaji wa shirika la ugavi wa umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) katika maeneo ya kiufundi, usimamizi wa fedha na uendeshaji na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya umeme katika maeneo ya vijijini.
Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) ni Taasisi ya Serikali ya Marekani inayotoa misaada kwa nchi zinazoendelea, shughuli zake zinajengwa katika misingi kwamba msaada utaleta ufanisi na matokeo makubwa pale unapoimarisha utawala bora, uhuru wa kiuchumi na uwekezaji katika watu ambao unakuza uchumi na kuondoa umaskini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!