Saturday 8 November 2014

PAPA FRANCIS ATANGAZA UAMUZI MZITO

Vatican. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis anafikiria kufanya mabadiliko makubwa katika kanuni za ndoa zinazozuia wanandoa kutengana bila kibali cha kanisa hilo.

Katika mafundisho ya kanisa hilo, wanandoa hawaruhusiwi kutengana hadi kifo, labda iwe kwa sababu chache, zikiwamo zinaa.
Hata hivyo, juzi Papa Francis alieleza uamuzi huo unatokana na ugumu mwingi ambao wanandoa wanaofikiria kutengana wanaupata kwa sasa.
Kwa sasa, waumini wa Kikatoliki wanakumbana na vikwazo vingi katika kutengua ndoa zao kisheria.
Kikanuni, ndoa ni sakramenti ndani ya kanisa hilo ambayo ikishafungwa basi haifunguliwi.
Papa Francis alieleza ugumu huo umewafanya baadhi ya maofisa wa kanisa hilo kujinufaisha kwa ada zinazofikia maelfu ya dola, wanazotoza kama gharama za kusimamia kesi zinazohusu kutenguliwa kwa ndoa.
Aliwaambia maofisa wa kanisa hilo wanaoshughulikia utenguaji wa ndoa hizo wanaohudhuria semina maalum mjini Vatican kwamba akiwa askofu wa Buenos Aires, Argentina aliwahi kumtimua kazi ofisa aliyedai dola ili kushughulikia suala la kutengua ndoa.
Alieleza kuwa wakati ule alishangaa kuona baadhi ya waumini wakipata shida kushughulikia ndoa zao, wakisafiri umbali mrefu, kupoteza muda kwenda kwenye mahakama za kanisa.
Alifichua jinsi alivyomtimua kazi ofisa aliyedai dola 10,000 kushughulikia suala hilo.
“Lazima tuwe makini, mchakato huu usigeuzwe kuwa biashara kwa wengine,”alieleza Papa Francis.
Uamuzi huo ni mtihani kwenye mafundisho ya kanisa hilo kuhusu ndoa ambayo ni sakramenti inayoheshimika, isiyoruhusiwa kufunguliwa kwa njia ya talaka.


Waumini wengi wa Kikatoliki ambao wamekuwa wakitaka ndoa zao zitenguliwe, hulazimika kuomba kibali, kanuni ya kanisa ambayo lazima ibatilishe kwanza muungano wao, kwamba ulikuwa wa lazima au haukuwapo.
Sababu za kutenguliwa ndoa zimekuwa ni pamoja na wanandoa kutokuwa waaminifu katika ndoa, yule aliyeolewa kwa kulazimishwa, umri mdogo, kuumizwa kisaikolojia.
Baada ya ndoa kutenguliwa, waumini hao wanaruhusiwa kuoa tena ndani ya kanisa.
Papa Francis alieleza kuwa kwa sasa anafikiria maombi yaliyofikishwa Vatican wakati wa sinodi ya maaskofu kuhusu familia wakipendekeza mchakato wa kutengua ndoa uharakishwe, uendeshwe bila gharama.
Majimbo mengi ya kanisa hilo yamekuwa yakitoza fedha kwa wanandoa wanaotaka ndoa zao zitenguliwe kwa kulipisha maelfu ya dola kama gharama za uendeshaji, ingawa mengine yameanza kupunguza ada hizo, kama ilivyotokea India na Marekani mwezi mmoja uliopita.
Kwa upande wake, Papa Francis alirejea msimamo wake kwamba mchakato wa kutengua ndoa ambao wakati mwingine huchukua muda mrefu, gharama utazamwe upya kwani unawakatisha tamaa wengine.
Kwa sasa, Wakatoliki waliotengana bila kibali cha kanisa hilo, kisha wakaoa au kuolewa hawapokei komunio, badala yake wanaonekana kama wazinzi, watu wanaoishi kwenye dhambi.
Wengi wameuona uamuzi huo wa Papa Francis kama hatua ya kulifanya Kanisa Katoliki liwe kweli la msamaha, wakiwa na matumaini kwamba wataruhusiwa kupokea komunio.
Wakatoliki wanasemaje?
Hatua hiyo ya Papa Francis imeungwa mkono na waumini mbalimbali wa Kanisa Katoliki nchini.
Waumini hao wamesema kuwa hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba, wengi wa wanandoa wametengena licha ya kuwepo kwa sheria hiyo, jambo linalowafanya baadhi yao kuwa na uhusiano wa kimapenzi na watu wengine wasio washirika wao wa ndoa.
“Sheria hiyo imekuwa kikwazo kisicho na maana kwa kuwa Wakatoliki wametengana licha ya kuwepo kwa sheria hiyo. Ni bora kanisa likaruhusu kutengana kwa kufuata taratibu, kuliko kuzuia wakati watu bado wanatengana,” alisema Agness Jacob wa jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa kanuni hiyo imekuwa ikisababisha kuongezeka kwa uzinzi na uasherati kwa waumini wa kanisa hilo waliotengana, jambo ambalo siyo tu chukizo kwa Mungu, bali pia ni linasababisha kuenea kwa maambukizi ya magonjwa ukiwamo Ukimwi.
“Nimeona watu wengi tunasali pamoja lakini wametengana na kanisani wanahudhuria japo hawapati huduma za kiroho. Sasa hii haiwasaidii Wakristu hawa kwa sababu mmoja wao anaweza kuwa amegundua kuwa alifanya makosa ya kuchagua mwenza,” alisema.
Naye James Rwezaula alisisitiza kuwa ni muhimu kwa Kanisa Katoliki kuendana na mabadiliko ya nyakati ili kuwahudumia waumini wake wanaoishi kuendana na wakati uliopo na siyo kwa mtindo wa maisha yaliyopita.
Alisema kuwa na sheria zisizobadilika hata wakati mwingine kuwafunga waumini na kuwanyima uhuru, ambao pengine husababisha waumini kujihusisha na vitendo vilivyo kinyume na amri za Mungu.
“Wenzetu wa nchi za Magharibi wanajua kusoma alama za nyakati, najua Papa Fransis atalichukulia hatua jambo hili kwa sababu limeonekana kuwa kero kwa Wakatoliki wengi,” alisema muumini huyo wa Parokia ya Segerea Dar es Salaam.
Rwezaula aliongeza kuwa siyo dhambi kubadilisha kanuni zilizokuwepo kwa muda mrefu, lakini dhamira kuu ikabaki pale pale kuwafanya waumini kukua kiroho na baadaye waweze kuingia mbinguni.
Hata hivyo, Albert Simwanza alipendekeza Sheria za Ndoa za Kanisa Katoliki zibaki kama zilivyo kwa sababu zimesaidia ndoa nyingi kudumu mpaka sasa na kuwasaidia wanandoa kumaliza tofauti zao.
Alisema ingekuwa ruhusa kwa ndoa kuvunjwa, kungekuwa na ndoa chache zilizodumu. “Ndoa nyingi ni sawa na kuti linaloanguka, likazuiliwa na kitu na kulifanya liendelee kusimama. Sheria hii ya kanisa inawapa nafasi wanandoa kutafakari tofauti zao na kujirudi,” alisisitiza Simwanza ambaye pia ni mwalimu.
Dondoo muhimu kuhusu Papa Francis
Papa Francis ni mfuasi wa Shirika la Majesuits, tangu miaka ya 1960 amekuwa akifanya kazi na jamii hiyo na kuwa mtiifu hadi alipoteuliwa kuliongoza Kanisa Katoliki duniani.
Papa Francis ana pafu moja jambo ambalo linaweza kusababisha uchaguzi mwingine wa kiongozi wa kanisa hilo iwapo afya yake itazorota kama ambavyo Papa Benedict aliomba kupumzika baada ya afya yake kuzidi kuzorota.
Pia ni mwanaharakati anayepinga ndoa za jinsi moja. Mwaka 2010 akiwa nchini kwake Argentina, alieleza wazi kuwa yeye hana shirika na sheria za jinsi moja nchini kwake.
Kabla ya kuwa Mjesuits alikuwa anapenda kuwa mkemia, mtalaamu wa maabara. Mwaka 1969 alianza kufanya kazi za Mjesuits.
Papa Francis anapenda kujipikia mwenyewe. Akiwa Argentina aliacha kukaa nyumba ya makardinali akaenda kukaa nyumba wanazokaa mapadri.
Pia, Papa Francis hunapanda usafiri wa umma.

Imeandaliwa na Ndyesumbilai Florian kwa msaada wa mtandao. Nyongeza na Peter Elias

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!