MTOTO wa mwanamuziki nguli wa DR Congo, Kofii Olomide (Ahmed Jan Olomide), juzi aliungana na mamia ya wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake katika mazishi ya kiongozi na mwimbaji wa bendi ya Ruvu Stars, Khamis Kayumbu ‘Amigolas.’
Amigolas aliyezikwa siku hiyo katika makaburi ya Kisutu, alifariki Jumapili iliyopita akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taufa ya Muhimbili ya jijini Dar es Salaam akisumbuliwa na maradhi ya moyo tangu mwaka 2010.
Akizungumzia kifo cha Amigolas katika makaburi ya Kisutu, Ahmed Jan Olomide ambaye yupo nchini kwa ziara ya kutangaza albamu yake mpya ya ‘Amore,’ alisema ni pigo kubwa katika tasnia ya muziki wa dansi nchini.
Alisema japo yeye ni raia wa DR Congo, kwa muda mrefu amekuwa akifuatilia muziki wa Tanzania akiamini ni nchi mbili zenye uhusiano wa karibu ikiwemo kupitia muziki, hivyo anawapa pole watanzania kwa msiba huo mkubwa.
Mwingine aliyezungumzia msiba huo ni mwimbaji wa zamani wa Twanga Pepeta, Deo Mwanambilimbi aliyesema kifo hicho ni pigo katika tasnia ya muziki wa dansi nchini.
Mwanambilimbi ambaye ni mmiliki wa bendi ya Kalunde, alisema Amigolas alikuwa alikuwa ni mwanamuziki aliyejaalia kipaji na uwezo wa aina yake akijizolea mashabiki wengi tangu akiwa Bendi ya Twanda alikodumu kwa miaka mingi kabla ya kujiunga na Ruvu Stars. “Amigolas alikuwa mwanamuziki mwenye uwezo mkubwa kiasi ncha kuwa kipenzi cha mshabiki wengi wa muziki wa dansi, hivyo kifo chake kimeacha pengo kubwa katika tasnia hii,” alisema Mwanambilimbi.
Mwingine aliyemzungumzia Amigolas, ni Ahmed Jan Olomide, akisema ameguswa sana na kifo cha mwanamuziki huyo aliyefanya mengi katika tasnia ya muziki wa Tanzania, hivyo akiwa mmoja wa wadau wa tasnia hiyo ndio maana ameungana na wengine kumzika.
Kwa upande wake Haji Ramadhani msanii wa Twanga Pepeta, alisema amepokea msiba huo kwa mshtuko mkubwa kwani ameondoka wakati bado tasnia ya muziki wa dansi ilikuwa bado inahitaji mchango wake.
“Nashindwa kuamini kabisa kama kweli Amigolas ndio basi tena, alikuwa mtu wa mfano kwa wasanii wengi wa muziki nchini. Lakini tusiseme sana kwani Mungu amemaliza kazi ya uumbaji wake,” alisema Ramadhani.
Wadau wengine wa masuala ya muziki na burudani walishiriki mazishi hayo ni Steven Nyerere, Jacob Steven ‘JB’, Visent Kigosi ‘Ray’ Ali Choki, Charles Baba, Mtitu na wengine wengi.
TZ-DAIMA
No comments:
Post a Comment