Saturday 15 November 2014

LHRC: HAKI ZA AJIRA HAZITEKELEZWI KIVITENDO

IMEELEZWA kwamba baadhi ya makapuni na mashirika mbalimbali bado haki za ajira hazitekelezwi kivitendo na hivyo kusababisha wafanyakazi kufanya kazi katika mazingira magumu.


Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Emelda Lulu Urio, katika warsha ya siku tatu iliyowakutanisha wadau wanaoshughulika na ajira hapa nchini.
Urio alisema utafiti walioufanya mwaka jana walibaini mapungufu lukuki ikiwemo suala la kukosa likizo, ujira mdogo na kujiunga katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Alisema kwa kulitambua hilo wameamua kuwaleta wadau hao pamoja ili kuweza kuweka mikakati ya namna gani haki hizo zitaweza kutekelezwa.
Kwa mujibu wa Urio matarajio yao ni kujenga uelewa kuhusu haki zihusuzo ajira na namna ya kuzidai pale zinapokiukwa aidha kwa makusudi au bahati mbaya.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Migodini, Shigela Aloyce, alisema bado katika maeneo ya kazi hakuna usalama wa kutosha.
Aloyce alisema matajiri wamekuwa wakiangalia zaidi katika kupata faida huku wakisahau kuwa hata afya za wafanyakazi wao ni suala la kupewa kipaumbele.
Kaimu Kamishna wa Ajira kutoka Wizara ya Kazi na Ajira, Hawa Wenga, alisema kupitia mpango wa Matokeo Makubwa(BRN), Serikali imejipanga kuongeza watumishi na kuboresha mazingira ya kazi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!