Sunday 16 November 2014

KWANINI NI VIGUMU KUACHA UKEKETAJI?

MKATABA wa Haki ya Mtoto unasema kwamba Maendeleo ya mtoto yanahusu ukuaji wake kimwili, kiakili, kimaadili na kiroho. Haki ya Elimu, Watoto na Ajira, Elimu ya Uhusiano wa wasichana na wavulana ambayo yanapaswa kuangaliwa ili kumlinda mtoto dhidi ya ukatili wa Kijinsia na kuhakikisha anapata elimu na kuwa salama kiafya.


Katika mfululizo wa Makala zetu katika tafakuri huko nyuma tumejadili kuhusu upatikanji wa Katiba mpya na uzingatiwaji wa haki za msingi za kijamii ikiwepo kuwalianda watoto wa kike dhidi ya mila potofu ambazo zinawapelekea kukosa huduma za msingi kama afya, elimu, maisha bora na endelevu na kufifisha ndoto yao ya maisha.
Hatuwezi kuwa na watu wastaarabu na wenye uelewa  wasiokumbatia mila potofu kama viongozi wetu hawana uwajibikaji. Tulijadiliana kwa kina juu ya tatizo la mimba za utotoni na jinsi ambavyo zimeharibu kabisa ndoto ya wasichana wengi wa vijijini.
Wiki hii tunajadili kuhusu ukeketaji kwa wasichana ambao unasababisha madhara makubwa kwa wanawake na pengine pia huchangia kutokea kwa mimba au ndoa za utotoni.
Ni jukumu la viongozi wetu kupambana na tatizo hili, kama linakua inaonesha wazi kwamba viongozi wamelala au hawapo kazini.
Kwa sasa mkoa wa Mara unatajwa kama kinara wa ukeketaji  lakini tujiulize ni kwanini? Kuna tatizo gani? Hawana viongozi? Wameshawakamata wanaofanya hivyo vitendo?
Novemba hadi Disemba mwaka huu ni msimu wa ukeketaji huko Tarime, maelfu ya wasichana watakeketwa, huku na vijana wa kiume nao wakiandaliwa kwa tohara, baada ya shughuli hii nzito kwa jamii hiyo, zitafuata sherehe za kuwapongeza  na kuwatoa ndani kama ishara ya ukuaji. 
Ni kipindi cha nderemo, ngoma ya jadi aina ya Ritungu inapata umaarufu kwenye msimu huu. Tunyamaze kimya? Tuseme au tuwaachie wahusika waamue?
Mwaka 2004 hali halisi ya ukeketaji mkoani Mara ilikuwa asilimia 38.1,  Hata hivyo kufikia mwaka 2010 vitendo hiyo viliongezeka hadi kufikia asilimia 39.9,  ambalo ni ongezeko la asilimia1.8. Kuongezeka kwa vitendo vya ukeketaji hadi kufikia asilimia 1.8  kunaonesha kuwa bado hakuna jitihada za dhati na za makusudi za kukomesha ukatili huu.  Tujiulize ni kwanini tatizo haliishi?
Mabinti watatu katika kata ya Remagwe wanasema wazazi wao hawaungi mkono ukeketaji, wameweza kutimiza umri wa miaka 19 hadi 22 bila kukeketwa na bado hawajaolewa, wanajishughulisha na ushonaji, wanajisikia fahari kutokeketwa kwani maisha yao ni nafuu sana kulinganisha na waliokeketwa.
“Wengi wamezaa watoto mfululizo (watoto 3-4) wamechakaa, wamezeeka, wanakabiliwa na vipigo na kazi nyingi,” anasema Bhoke Chacha mmoja wa washiriki wa utafiti wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kutoka Tarime.
Kwa muda mrefu katika jamii ya Wakurya binti asipokeketwa alitengwa na wenzake wa rika lake, alidharauliwa na jamii, alionekana mchafu, aliitwa majina ya kunyanyapaa kama vile “Msaghane” na hakuweza kupata mchumba.
Mwanamke alikeketwa ili ajitulize kwa mume wake. Kwahiyo kazi ya kujenga mahusiano ni ya wanaume na sio wanawake, yote hii ilichangiwa na mila potofu zinazoambatana na mfumo dume
Machi, mwaka huu TGNP ilifanya utafiti shirikishi katika kata ya Nyamaraga Tarime, moja ya masuala ambayo yaliibuliwa ni kwamba ukeketaji pia umeathiri wafanyakazi wa serikali ambao ni wanawake.
Mfanyakazi akijulikana anatoka kabila ambalo hawakeketi, utendaji wake utakuwa mashakani. Kwa mfano katika shule ya Ng’ereng’ere mwanafunzi alikataa kuadhibiwa na mwalimu akamwambia “Siwezi kuadhibiwa na msaghane, mtu hajakeketwa anichape mimi? Haiwezekani”.
Mwaka 2004 serikali ilianza kampeni ya kupinga ukeketaji lakini matokeo yake mabinti 4,000 walifanyiwa ukeketaji. Hata hivyo Serikali haijawahi kutenga rasilimali za kutosha na kutafuta mbinu endelevu katika kukomesha ukeketaji.
Kwa mfano bajeti ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 inalenga kuziwezesha kamati za ulinzi za wilaya na ya taifa pekee katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia,  Hakuna ushirikishwaji wa jamii husika.
Ukifika Tarime, ukakaa na kuwasikiliza wahusika utagundua kwamba ukeketaji umechangiwa na suala la uchumi. Baadhi ya ndugu katika jamii hushawishi mabinti kukeketwa kwa kuwaahidi zawadi, mabinti huwatoroka wazazi wao na kwenda kukeketwa.
Zawadi hufikia thamani ya sh 500,000 au zaidi. Wakati mwigine mangariba na wazee wa mila wanalazimisha kuendelea kwa vitendo hivyo kwa sababu wanapata fedha ambazo ni tozo kwa kazi hiyo.
Katika kukomesha ukeketaji ni muhimu kujifunza kwa nchi jirani kama Kenya iliona izitambue sherehe za ukeketaji wa jamii hizo kwa msingi kuwa ukeketaji kama jambo la kimila ufanyike lakini damu isimwagike na binti asipate maumivu yoyote na usilete madhara kwa mabinti (sherehekea bila kuchanja binti).
Katika sherehe hizo hualika viongozi wa serikali kama Gavana na viongozi wengine wakubwa. Hii ilisaidia sana kupunguza vitendo vya ukeketaji ambapo kumekuwa na njia mbadala ya ukeketaji. Wasichana hukusanywa kambini na kufundishwa maadili mema.
Baadhi ya mabinti ambao wamepata elimu ya madhara ya ukeketaji kupitia baadhi ya asasi za kiraia, na klabu mbalimbali shuleni wamekuwa wakikimbilia polisi, makanisani au zaidi ya hapo ili kujinusuru na ukeketaji.
Taasisi ya Masanga pia kwa kiasi kikubwa imekuwa kimbilio kubwa kwa wasichana wengi wakati wa msimu wa ukeketaji.  TGNP kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA) wameandaa kambi ya kuwafunza vijana wa kike na kiume huko Tarime ambayo inaendelea wakati wote huu wa msimu wa ukeketaji. 
Ni jukumu letu, kupigana kuhakikisha mila hizi zinapotea, tutafute njia mbadala za kuwafunda na kuwakuza wasichana wetu lakini sio hii. Serikali kuanzia ngazi za vijiji/mitaa/ vitongoji ni wahusika muhimu kwenye kudhibiti au kukomesha kabisa vitendo hivi

1 comment:

Anonymous said...

aziz bilal21:53


1
Reply

Loo hili suala ni gumu sana kuliacha hata wenzetu baadhi ya waarabu kule north Africa limewashinda kulipiga vita na mpaka hii leo bado wanaliendeleza libeneke,nimewahi kuona on tv binti wa kimisry about 13yrs old walimuonyesha siku yake ya kukeketwa,looh siwezi rudia angalia machungu ka yale tena ktk maisha yangu tena,yule mtoto wa kike baada ya kukatwa alipiga kelele kubwa ya uchungu,binafsi nikigunduwa mtu kamfanyia kitendo hicho binti wangu hiyo itakuwa ni vita kubwa sana.

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!