Tuesday 18 November 2014

JOTO ARDHI KUZALISHA MEGAWATI ZAIDI YA 5000 ZA UMEME



Kupatikana kwa joto ardhi kwenye maeneo ya pembezoni mwa Bonde la Ufa, ni ugunduzi unaoelezwa kuwa chanzo tajiri cha nishati ambayo haijaanza kuvunwa nchini.

Licha ya teknolojia hii ya kupata nishati kutokana na joto ardhi kuwa ghali, lakini ni ya uhakika kuliko njia nyingine za kuzalisha umeme . Na ikianza kutumiwa haitarajiwi kuisha.
Baada ya kubaini utajiri huu, Serikali imeanzisha Shirika la Taifa la Maendeleo ya Joto Ardhi (TGDC) ili kurahisisha mchakato wa kuanza uwekezaji katika sekta hii.
Katika mahojiano na Mwananchi, meneja mkuu wa TGDC, Mhandisi Boniface Njombe anazungumzia kuhusu ugunduzi huu.
Swali: Tanzania inatajwa kuwa ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye hazina kubwa ya joto ardhi, suala hili lina ukweli?
Jibu: Ni kweli kuwa Tanzania tuna hazina kubwa ya joto ardhi na tayari kuna maeneo zaidi ya 50 ambayo utafiti wa awali umefanyika na kubanika yanaweza kutumika kuzalisha nishati.
Maeneo haya yapo katika kingo ya Bonde la Ufa, kuanzia ndani ya kreta ya Ngorongoro, Ziwa Manyara na Eyasi, maeneo ya Kisaki Morogoro, Maji Moto Mara, Mtanga Kagera, Amboni Tanga, Maji moto Katavi, Ushirombo Geita, Rock of Hahes Rukwa hadi maeneo ya Iringa.
Maeneo kama Kreta ya Ngorongoro, Ziwa Manyara na Eyasi ni maeneo ya hifadhi, lakini utafiti wa awali unaonyesha katika maeneo hayo pekee, tunaweza kupata megawati 1,000.
Swali: Miradi hii ikianza, haiwezi kuibua malumbano makubwa na wanaharakati wa mazingira na uhifadhi?
Jibu: Kabla ya kuanza miradi lazima ufanyike utafiti wa mazingira kuona kama kuna athari za kimazingira na ni za kiasi gani.
Eneo kama kreta ya Ngorongoro, siyo lazima mitambo kufungwa, panaweza kuchimbwa eneo dogo, bomba zikawekwa kuvuta joto hadi sehemu nyingine ambazo mitambo itawekwa. Miradi kama hii ipo katika maeneo ya hifadhi, mfano Kenya, tayari wameanza kuzalisha umeme huu.
Swali: Bila shaka miradi hii ni ya gharama kubwa, je, nchi inaweza kumudu?
Jibu: Ni kweli mitambo hii ni ya gharama na kwa wastani kisima kimoja kinaweza kugharimu hadi Dola 20 milioni za Marekani, lakini kama mradi ukifanikiwa haitarajiwi joto kuisha. Hivyo ni mradi wa milele. Miradi kama hii inafanywa kwa ushirikiano na Serikali hasa katika hatua za utafiti wa awali na kujiridhisha ni kiasi gani cha joto ardhi kinachoweza kupatikana katika eneo husika.
Kwa mfano, Rwanda walitumia Dola 40 milioni, lakini mwishowe hawakupata kiasi cha kutosha cha joto ardhi, hivyo utaona jinsi hadhari inavyotakiwa kuchukuliwa kwenye miradi hii.
Swali: Maeneo yaliyobainika kuwapo joto ardhi, mengi yanalindwa na sheria za uhifadhi mazingira, mnashirikiana vipi na taasisi nyingine ili miradi ifanikiwe?
Jibu: Ni kweli maeneo haya yamehifadhiwa, lakini kama nilivyosema mwanzo lazima upembuzi yakinifu ufanywe wa athari za kimazingira katika kila mradi kabla ya kuanza.
Swali: Joto ardhi linaweza kuzalisha nishati za aina gani?
Jibu: Joto ardhi linaweza kuzalisha umeme, hewa ya baridi, hewa ya joto kwa ajili ya viwanda na mashamba ya maua na nishati nyingine kulingana na mahitaji.
Swali: Kuna mpango wa kushirikiana na mashirika ya kimataifa?
Jibu: Sisi ni wanachama wa umoja wa nchi zilizopo katika bonde la ufa, tuna chama chetu na tumekuwa tukipata misaada ya kitaalamu kutoka wahisani na mashirika ya kimataifa ikiwamo Umoja wa Afrika, Shirika la Mpango wa Mazingira la kimataifa (UNEP) na mashirika mengine.
Pia tumekubaliana kuwa na kituo cha utafiti kitachokuwa Nairobi, Kenya. Wataalamu wetu watakuwa wakienda huko na kukutana na wengine kubadilishana uzoefu.
Swali: Shirika unalolisimama ni jipya, mmejipanga vipi kuhakikisha elimu juu ya joto ardhi inawafikia wananchi na wadau wengine?
Jibu: Ni kweli suala hili ni jipya, ila tumejipanga kutoa elimu kwa kushirikisha vyombo vya habari kufika katika maeneo yenye joto ardhi na kuelimisha manufaa yake.
Naamini ndani ya miaka michache kabla ya kuanza uwekezaji rasmi, Watanzania wengi watajua juu ya joto ardhi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!