Tuesday, 11 November 2014

JE NI MUDA GANI SAHIHI WA KUMPATIA MTOTO MCHANGA MAJI YA KUNYWA?


Mara nyingi sana nimesikia kinamama wakijadiliana juu ya hili na kubadilishana uzoefu. Ingawa nimesikia wengi wakiliongelea kinachoshangaza ni kwamba sijawahi kusikia jibu moja ambalo naweza sema ndilo jibu sahihi au laa basi kuambiwa kwamba hili ndilo jibu sahihi na kupewa sababu za kuridhisha .


Kwakua lengo langu ni kuhakikisha afya ya umma na  familia kwa ujumla iko vizuri, nimeamua kufanya Utafiti  binafsi kwa kusoma vitabu ,majarida na kuongea na baadhi ya madaktari wa watoto ninaowafahamu.
Si kuishia hapo tu, nimeongea na akina mama waliolea watoto miaka ya zamani na wanaolea watoto hivi sasa. Na haya ndio majibu niliyopata.
Majibu kutoka taasisi za afya.
Taarifa za wataalam wa afya kutoka kwenye  taasisi zinazoaminika duniani kama World health organization na Association of American Pedietrisions, zinasema Mtoto mdogo kati ya siku moja hadi miezi sita (1-6)  
Hatakiwi kupewa maji wala chakula kingine chochote zaidi ya maziwa ya mama au maziwa maalum ya watoto(baby formula) au maziwa ya Ngombe.
 
W.H.O shirika la afya Wameelezea kwamba kiasi cha maji mtoto anachopata kwenye maziwa kinatosha kabisa.
Kumpa mtoto maji si salama kwani yataharibu uwezo wa mwili wa mtoto kunyonya virutubisho kutoka kwenye maziwa.
Maji pia yatafanya mtoto ashibe na ashindwe kunywa maziwa kwa kiasi kinachohitajika, Mbaya zaidi ni kwamba maji mengi kwa mtoto wakati mwingine huweza kuleta hali iitwayo water intoxication,
Hali hii huweza kumfanya mtoto azimie na wakati mwingine kuingia katika  coma. Hali hii huja pale ambapo wingi wa maji mwilini utapunguza kiasi cha sodium mwilini(low sodium concentration).
Taarifa inasema kwamba, ingawa unaweza kumpa mtoto maji baada ya miezi 6, wanashauri mtoto apewe maji kidogo na kwa kipimo maalum hadi pale atakapo timiza mwaka mmoja ambapo anaweza kunywa maji kwa kiasi atakacho.

Majibu  kutoka kwa madaktari wetu.
Madaktari wanne tofauti niliyobahatika kuongea nao, majibu yao yalifanana kwa kiasi kikubwa.
Kwanza waliunga mkono taarifa za World health organization (taarifa hapo juu) . Lakini pili walikua na yao yakuongeza.
Walisema kwamba maziwa ya mama na formula zinamtosha mtoto endapo tu mtoto huyo anapewa maziwa yanayomtosha kushiba na yenye virutubisho vyote.
Walieleza kwamba kina mama wengi hawanyonyeshi mtoto hadi akashiba. Si kwasababu hawana maziwa au hawataki bali ni kwasababu hawajui mtoto anaitaji maziwa kiasi gani ili ashibe na anyonyeshe kwa muda gani ili mtoto apate kiasi hicho cha maziwa.
 Na kwa sababu wakati mwingine maziwa  ya mama yenyewe hayana virutubisho vyakutosha kwani mama mwenyewe hali, au mwili wake hauna virutubisho vyakutosha na wakati mwingine anapungukiwa baadhi ya virutubisho .
Walisema kua hali hii hufanya maziwa ya mama yasitoshe kabisa kwa mtoto na kulazimu mtoto aanze kupewa uji mwepesi mapema kabla ya miezi sita ili kufidia lishe yake. Na Pale tu unapoanza kumpa mtoto chakula zaidi ya maziwa basi  ni vyema ukaanza kumpa maji kwani uji na vyakula kama hivyo huesabika kama vyakula vigumu kwa mtoto.
Moja alisema kwamba endapo mtu analazimika kumpa mtoto uji mapema basi  ni vyema mtoto afikishe angalao miezi minne.
Mwingine alisema kwamba, moja ya sababu zinazochangia kabisa kuwakataza kina mama kuwapa watoto maji ni pamoja na uwezekano mkubwa wa mtoto kupata magonjwa kutoka kwenye maji ya kunywa.
Mara nyingi maji hayawi safi na salama. Alinieleza kwamba, magonjwa ya tumbo yanayoleta kuhara kwa mtoto ni moja kati ya magonjwa yanayosababisha vifo vya watoto  kwa haraka.

Majibu ya Mama aliyelea watoto miaka ya 60 –  80
Mama huyu aliyeanza kulea mtoto wake wakwanza mwaka 1967 alikua na haya yakusema.
Alisema enzi zile walikua wanafundishwa namna ya kulisha mtoto kila wanapoenda kliniki.
Alisema Walikua wakipewa karatasi yenye  picha za vyakula na majina ya vyakula hivyo na kuambiwa zaidi ya kunyonyesha ni lazima wawape watoto wao vyakula hivyo. Wakati mwingine walienda kwenye vikundi vya akinamama na kufundishwa namna ya kuandaa vyakula hivyo kwaajili ya mtoto.
Alinieleza kua vyakula hivyo viliwekwa kwa makundi,na kulikua na kundi lenye maji ya kunywa na maji ya matunda. Hivyo wao waliwapa watoto maji na maji ya matunda kama kadi ilivyoelekeza, aliniambia kua walikua wakipewa karatasi hizo miezi  miwili baada ya kujifungua. (akimaanisha mtoto akiwa na miezi miwili).
Kwa maana hiyo, walianza kuwapa watoto uji, maji na maji ya matunda wakiwa na miezi miwili.
Majibu ya Mama anaelea watoto  hivi leo.
Niliongea na mama wawili tofauti, mmoja ana watoto wanne na mwingine ana wawili.

Mwenye watoto wanne, alisema watoto wake wote walianza kunywa maji na uji mwepesi wakiwa na miezi miwili. Alisema kwamba ingawa watoto wake walikunywa maziwa bila shida aliona wazi kabisa kwamba hawashibi na ndipo alipoamua kuongeza uji mwepesi kwenye lishe yao.
Alinieleza kwamba huandaa uji huo na kisha kuuchuja na kuhakikisha ni mwepesi kama maziwa na kisha kumpa mtoto kwenye chuchu kama anavyompa maziwa.
Uji huo huandaliwa kwa maziwa,maji na unga.
Mwenye watoto wawili, alikua na haya yakusema.
Alisema kwamba watoto wake walikunywa maziwa tu hadi walipofikisha miezi 6. Pale alipoona maziwa ya mama hayatoshi aliongeza maziwa ya ng’ombe ili kuhakikisha mtoto anashiba.
Alinieleza kwamba, ili kuhakikisha mtoto anakunywa maziwa kwa kipimo sahihi, alikamua maziwa yake kwa kutumia pampu maalum na kuyaweka kwenye chupa ili apime kipimo sahihi. Na kwakua mtoto wake hushiba vizuri na wataalam husema mtoto asipewe maji basi hakua na sababu yoyote ya kumpa mtoto maji kabla ya wakati uliothibitishwa.


Mtizamo wangu
Baada ya kukusanya yote haya na kutafakari, nimegundua kwamba pale ambapo mtoto anapewa chakula chochote zaidi ya maziwa basi ni sawa apewe maji  kwa kiasi Fulani,
kwani tayari mwili wake unapokea chakula kigumu na huitaji maji zaidi.
Kwa upande mwingine, sioni sababu ya kumpa mtoto maji endapo anapata maziwa katika kiasi kilicho sahihi kwa mwili wake na anashiba.
Ila kinachonitia wasiwasi ni uwezekano wa  mtoto kupata maziwa yakutosha.
Kwa maisha yetu ya kitanzania Gharama ya kumlea mtoto kwa kumpa  maziwa ya kopo ni kubwa sana na wazazi wengi hawawezi kumudu gharama hizo.
Gharama za maziwa ya ng’ombe pia ziko juu na maziwa niyashida hasa kwenye miji mikubwa hivyo ni ngumu kwa mwananchi wa kipato cha kawaida na cha chini kufidia lishe ya mtoto kwa kuongeza maziwa hayo yakununua.
Hii humlazimu mzazi kumuanzisha mtoto uji mapema ili kufidia lishe yake. Jambo linalopelekea mtoto kula chakula kigumu na kunywa maji akiwa chini ya miezi sita .
Hata hivyo ni vyema kujua kwamba ingawa kuna kiasi au kipimo Fulani cha maziwa ambacho mtoto anatakiwa kupewa si kweli kwamba watoto wote hushiba kwa kipimo hicho.
Watoto hutofautiana ukubwa wa mwili kitu ambacho hufanya hata kula yao itofautiane.
Kwa mantiki hiyo basi ni wazi kwamba watoto wa rika moja si lazima wapewe kipimo sawa cha maziwa, tofauti ya hatua tano juu ya kipimo cha kawaida huruhusiwa.

Ushauri
Wangu ni kwamba pale ambapo mtoto anapewa chakula chochote zaidi ya maziwa basi ni sawa apewe maji  kwa kiasi Fulani,
kwani tayari mwili wake unapokea chakula kigumu na huitaji maji zaidi ili kusaidia
uyeyushwaji wa chakula katika mwili.
Kwa upande mwingine, sioni sababu ya kumpa mtoto maji endapo anapata maziwa katika kiasi kilicho sahihi kwa mwili wake na anashiba.
 
Kumbuka tu kwamba ukosefu wa maji mwilini pia huzaa matatizo makubwa ya afya kwa mtoto.
MAJI NI UHAI

Special thanks to Manyandahealthy.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!