Tuesday 18 November 2014

IJUE HISTORIA FUPI YA MAMA YETU MAMA SALMA KIWETE!



MAMA SALMA 
Swali: Ni ipi historia fupi ya maisha yako?
Jibu: Mimi naitwa Salma Rashid. Nilizaliwa katika wilaya ya Lindi Mjini, Novemba 30, 1963. Baba yangu anaitwa Rashid Yussuf Mkwachu na mama yangu ni Mwanapaza binti Shariff.
Kwa asili, baba yangu anatoka Sarai, Rufiji mkoani Pwani na mama yangu anatoka Lindi.



Katika familia yetu, upande wa mama, tulizaliwa watoto saba, wasichana watatu na wavulana wanne. Mimi ni wa sita, ila kwa baba ni wa pili, nina kaka yangu na mdogo wangu. Nina wadogo zangu wengine watatu ambao tunachangia baba, kati yao wavulana ni wawili na msichana mmoja.
Baba yangu alikuwa mfanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977 na kituo chake cha kazi kilikuwa Mtwara, wakati baba anafanya kazi, mama alibaki Lindi, hali ambayo ilinifanya nipate elimu yangu ya msingi kuanzia mwaka 1973 katika shule nne tofauti; Nnaida ya Mikindani, Mtwara, Rahaleo ya Lindi, Ligula (Mtwara) na Stadium, Lindi ambapo nilimalizia elimu yangu ya msingi.
Ingawa wakati ule nafasi za kujiunga na sekondari zilikuwa chache, namshukuru Mwenyezi Mungu nilikuwa miongoni mwa waliochaguliwa.
Swali: Wewe unatoka Lindi na Mheshimiwa Rais anatoka Pwani, mlikutana wapi na mlifunga ndoa lini? Jibu: Kila jambo hupangwa na Mwenyezi Mungu. Nilikutana na mume wangu mwaka 1985 nikiwa katika Chuo cha Ualimu Nachingwea, yeye akiwa ni Katibu wa CCM wa Wilaya ya Nachingwea.

Tulipokutana kwa mara ya kwanza kitu ambacho aliniambia ni kwambanakupenda na nataka nikuoe kusema kweli hakusema anataka awe rafiki yangu au vipi, sijui kama huo ndio utaratibu wa kina baba wote, lakini nasema kutoka moyoni, hicho ndicho alichoniambia na mimi kwa sababu nilimpenda, nilimkubalia, ingawa uamuzi wangu sikuutoa papo hapo.
Tulifunga ndoa Machi 30, 1989 wakati huo yeye akiwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini. Swali: Baada ya kufunga ndoa ikawaje? Jibu: Baada ya kufunga ndoa nilifanya taratibu za uhamisho kwa mujibu wa taratibu za kikazi.
Kwa hiyo nilihamia Dar es Salaam ambapo niliungana na mume wangu na tukawa tunakaa Mikocheni mtaa wa Ursino.
Swali: Katika miaka yenu hii 20 ya ndoa mmejaaliwa kupata watoto wangapi na wako wapi?
Jibu: Tunamshukuru Mwenyezi Mungu tumejaaliwa watoto watano kati yao wanne ni wa kiume na mmoja wa kike. Wote wanasoma, wa kwanza yuko kidato cha sita, wa pili cha nne, wa tatu cha pili, wa nne yuko darasa la tano na wa mwisho yuko darasa la tatu.

Lakini kwa ujumla tuna watoto wanane, ikiwa ni pamoja na watatu ambao mume wangu alipata na mke wake wa kwanza.

Hawa wakubwa mmoja ni Mbunge, mwingine ni daktari na mwingine ni mtaalamu wa Teknohama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano).

Ila siku zote napenda kusema tuna watoto wanane kwa sababu hata hawa wakubwa nimewalea mimi tangu wakiwa na umri mdogo sana. Kwa hiyo hawa ni watoto wangu sawa sawa na hawa niliowazaa mimi.

Swali: Una mipango gani ya baadaye?

Jibu: Kwa jumla mipango yetu katika taasisi ya WAMA ni mikubwa sana. Sasa ndio tumeanza, tuna shule moja tu, lakini tunatarajia kuongeza shule nyingi zaidi katika maeneo tuliyoyakusudia kwa sababu watoto wanaohitaji msaada wako wengi sana

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!